Diamond, Zari na Zuchu wangojewa kideoni!

UKIACHANA na kazi yao ya muziki, filamu, urembo na mitindo, mashabiki wengi duniani kote wamekuwa wakipenda sana kufuatilia na kufahamu maisha binafsi ya watu wao wenye ushawishi, umaarufu na wanaowahusudi kwenye sekta hizo.
Kwa kulitambua hilo, baadhi ya mastaa Bongo wamewahi kuja na Reality TV Show na Documentry ambazo zinazungumzia na kuangazia maisha yao halisi, pia ikiwa ni sehemu nyingine ya kuwaingizia kipato kwa kuuza maudhui hayo.
Hizi ni baadhi ya 'reality show na documentary' ambazo mastaa hao tayari wametangaza kuzifanya au watakuwepo ambazo zinangojewa kwa hamu na mashabiki wao ili kupata uhondo uliyopo ndani yake.
1. Diamond na Zari (Young, Famous & African)
Msimu wa kwanza wa reality show, Young, Famous & African ulioruka Netflix kuanzia Machi 18, 2022 ulikuwa wenye mafanikio makubwa, huku Diamond Platnumz na mzazi mwenziye, Zari The The Bosslady wakishiriki pamoja na watoto wao, Tiffah na Nillan.
Shoo hiyo inasimamiwa na Netflix tawi la Afrika Kusini inasubiriwa kwa hamu msimu wa pili na tayari wahusika wameanza kushuti tangu muda ingawa tarehe rasmi ya kurejea kwake haijatangazwa bado na Netflix.
Mastaa wengine Afrika walioshiriki msimu wa kwanza ni Khanyi Mbau (Afrika Kusini), Nadia Nakai (Zimbabwe), Annie Macaulay-Idibia (Nigeria), Naked DJ (Afrika Kusini), Swanky Jerry (Nigeria), Andile Ncube (Afrika Kusini) na wengineo.
2. Kajala na Paula (Mom & Daughter Like Twins)
Msanii wa filamu Bongo, Kajala Masanja pamoja na Binti yake wa pekee, Paula, Juni 2022 walitangaza wapo mbioni kuja na reality show yao waliyoipa jina la Mom & Daughter Like Twins.
Kwa mujibu wa Kajala, shoo hiyo itakuwa na mkusanyiko wa matukio mbalimbali ya nyuma ya pazia katika shughuli zao za kila siku ambazo mashabiki wao watafurahia kuziona na kushangaa uhalisia wa maisha yao.
"Kila kitu kitachokuwepo kwenye reality show ni ukweli wa maisha yetu na watu wote wanaotuhusu kwenye maisha yetu wataonekana" alisema Kajala.
3. WCB (The Real Life of Wasafi)
Hapo Juni 2018 Diamond alitangaza kuanza kwa kipindi cha televisheni 'The Real Life of Wasafi' kitakachokuwa kinaonyesha maisha ya watu wote wanaohusikana na WCB Wasafi na bidhaa zake, lakini hadi sasa hakijawahi kuonekana.
Wengi walivuta picha kuwa wanaweza kupata uhondo kama ilivyokuwa katika shoo ya Kim Kardashian na familia yake, Keep Up With the Kardashians iliyosumbua kuanzia mwaka 2017.
"Tungependa kuwatangaza rasmi kwamba Ijumaa hii ile TV Show yetu ya The Real Life of Wasafi inakuwa rasmi tayari kuanza, kwa hiyo waliyoko nyumbani tutawaambia itaanza kuruka saa ngapi," alisema Diamond wakati anazunguma na Wanahabari.
4. Irene Uwoya (I Am Every Woman)
Kwa mara ya kwanza Oktoba 2019, Irene Uwoya alifanya uzinduzi wa reality show yake na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Diamond Platnumz, hata hivyo haikuweza kuonekana popote pale.
Akaja kuizindua tena Agosti 2020 ikiwa tayari na jina la 'I Am Every Woman' na kuweka wazi ni lini hasa itaanza kuruka na kituo gani cha televisheni na kuachia kabisa kionjo chake, lakini pia haikuweza kuonekana hadi sasa. Inasubiriwa!.
Utakumbuka Irene Uwoya ambaye aliigia tano ya bora ya Miss Tanzania 2006, mwaka aliyoshinda Wema Sepetu, amekuwa na ushawishi katika filamu na mitindo ya maisha (life style) miongoni mwa vijana.
5. Zuchu (Life of Zuchu)
Tangu Septemba 2021, Staa wa WCB Wasafi, Zuchu alisema maandalizi ya documentary inayoelezea maisha yake imefikia asilimia 70 na kinachosubiria ni uongozi wake wa lebo kukamilisha vitu vichache. Hadi sasa nayo inangojewa.
"Nasubiria uwepo wa Mabosi wangu watoe ushuhuda wao kisha itakuwa tayari kwa asilimia 100, humu kuna maisha yangu ya kabla na baada ya muziki, nimeweka safari yangu nzima hadi hapa nilipo sasa," alisema Zuchu.
Utakumbuka Mbosso mara baada ya kusaini WCB Wasafi mwaka 2018 aliweza kuachia documentary yake, Life of Mbosso, pia Miss Tanzania 2006 Wema Sepetu aliwahi kufanya reality show yake, In My Shoes, huku Lady Jaydee akiwa na yake pia, Diary ya Lady Jaydee.
Hata hivyo, shoo ya Wema na Lady Jaydee zimesimama kwa kukosekana wadhamini ambao ndio hasa wamekuwa wakichangia gharama za uandaaji na faida nyingine, Jide aliwahi kusema udhamini ukipatikana basi, Diary ya Lady Jaydee itarejea!.