Diamond na rekodi zake katika uchawi wa namba - 1

Diamond na rekodi zake katika uchawi wa namba - 1

HIVI karibuni mwimbaji wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, Diamond Platnumz aliibuka mshindi katika Tuzo The Headies za Nigeria ambazo zilitolewa huko Georgia nchini Marekani ukiwa ni msimu wake wa 15.

Diamond alishinda katika kipengele cha Msanii Bora Afrika Mashariki baada ya kuwabwaga Harmonize, Zuchu, Meddy, Eddy Kenzo na Nikita Kering, huu ni mwendelezo wa kufanya vizuri na upande huo na kumfanya kuzidi kuwa mchawi wa namba.

Ikumbukwe hapa Tanzania, Diamond ndiye msanii wa muziki mwenye mafanikio zaidi katika tuzo za ndani, ameshinda tuzo 17 za Tanzania Music Awards (TMA) kati ya 29 alizochaguliwa kuwania tangu mwaka 2010 hadi 2015.

Baada ya kuachia wimbo wake uliomtoa kimuziki, Nenda Kamwambie uliobeba jina la albamu yake ya kwanza mwaka 2010, ulimuwezesha kuandika rekodi kwa kushinda tuzo tatu za TMA katika vipengele vya Msanii Bora Chipukizi, Wimbo Bora wa Mwaka na Wimbo Bora wa R&B.

Rekodi hiyo ilikuja kuvunjwa na 20 Percent mwaka 2011 aliyeshinda tuzo tano kwa mpigo ikiwa ni sawa na Alikiba mwaka 2015, mwaka 2013 Diamond akarejea tena na kushinda tuzo saba rekodi ambayo haijavunjwa hadi leo na msanii yeyote.

Wimbo wake, Number One ndio uliompatia tuzo nyingi zaidi ambazo ni tatu ni TMA; Wimbo Bora wa Afro Pop, Video Bora na Wimbo Bora wa Mwaka, huku remix ya wimbo huo akimshirikisha Davido ikimtangaza kimataifa zaidi hadi kushinda tuzo mbili za MTV Europe Music Awards (MTV EMA).

Tuzo za TMA zilirejea tena mwaka huu tangu ziliposimama mwaka 2015 lakini Diamond na wasanii wote wa WCB Wasafi walisusia kwa kile kilichoelezwa ni kutoridhishwa na mchakato mzima wa uandaaji tuzo hizo chini ya Baraza la Sanaa Taifa (Basata).

Kwa mwaka 2021 pekee Diamond alitajwa kuwania vipengele zaidi ya 20 katika tuzo za kimataifa kama BET, MTV EMA, All African Music Awards (AFRIMA), African Entertainment Awards USA (AEAUSA), Ghana Music Awards UK na African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA).

Hadi sasa Diamond aliyetoka kimuziki mwaka 2009 ameshinda tuzo za kimataifa kama Channel O, MTV, Soundcity, AFRIMMA, HeadiesAFRIMA, Kora, AEA, EAUSA, the HiPipo Music Awards na nyinginezo na kumfanya kuwa msanii pekee Bongo kufikia mafanikio hayo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Diamond ndiye msanii wa kwanza Bongo kuchaguliwa kuwania Tuzo za BET katika kipengele Best International Act, tayari amewania mara tatu (2014, 2016 & 2021) na kumfanya kuwa msanii pekee Bongo aliyewania mara nyingi ingawa hajawahi kushinda.

Kwa kipindi cha miaka 12 katika muziki wa Bongofleva, Diamond ameshinda na kutunukiwa tuzo zaidi ya 50 za ndani na za kimataifa na kuivunja rekodi ya Lady Jaydee mwenye tuzo zaidi ya 35 tangu alipoanza muziki mwanzoni mwaka 2000.

Novemba 2016, Diamond alishinda Tuzo Sub-Sahara Africa YouTube (SSA) ambazo zinatolewa na Google tangu mwaka 2007, alishinda katika kipengele cha Top Subscribed Creator in Tanzania, hii ni kutokana ndiye aliyekuwa anaongoza kwa subscribers YouTube upande wa wasanii.

Na hadi sasa Diamond ndiye msanii wa muziki mwenye subscribers wengi YouTube Tanzania na Kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa nao milioni 6.98, anafutiwa na Rayvanny (milioni 4.01) na Harmonize (milioni 3.45) ambao aliwatoa yeye kupitia lebo yake, WCB Wasafi miaka saba iliyopita.

Baada ya Diamond na vijana wake hao, ndipo wanafuata wasanii wengine wa Afrika kama Ckay (subscribers milioni 3.14), Davido (milioni 3.12), Burna Boy (milioni 3.09), Fally Ipupa (milioni 3.06), Mr. Flavour (milioni 2.72), Wizkid (2.52) na Tekno (2.14).

Ukirudi Tanzania baada ya Diamond, Rayvanny na Harmonize, wasanii wanaofuata kuwa na subscribers wengi YouTube ni Zuchu (milioni 2.17) na Mbosso (milioni 2.15) ambao nao kawatoa chini ya WCB Wasafi na bado wapo katika lebo hiyo.

Ikumbukwe Zuchu ndiye msanii wa kike Kusini mwa Jangwa la Sahara mwenye subscribers wengi YouTube, anafuatiwa na Yemi Alade wa Nigeria (milioni 2.06), Sinach wa Nigeria (milioni 1.93), Ada Ehi wa Nigeria (milioni 1.43) na Tiwa Savage wa Nigeria (milioni 1.13).

Kwa upande wa views YouTube bado Diamond ni namba moja Kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa na views bilioni 1.9, wanaomfuatia ni Burna Boy bilioni 1.5, Wizkid bilioni 1.4, Fally Ipupa bilioni 1.19, Davido bilioni 1.16, Mr. Flavour bilioni 1.03 na P Square bilioni 1.02.

Ukija kwa Tanzania pekee Diamond anafuatiwa kwa mbali na Rayvany views milioni 802.5, Harmonize milioni 780.5, Mbosso milioni 470.2, Zuchu milioni 364.5, Alikiba milioni 222.0, Lava Lava milioni 205.6, Aslay milioni 179.3, Nandy milioni 163.8 na Marioo milioni 118.6.

Kwa ujumla katika wasanii 10 Kusini mwa Jangwa la Sahara wenye subsribers wengi YouTube (most subscribed), watatu ni zao la WCB Wasafi ambayo ni lebo ya Diamond Platnumz, pia katika wasanii 10 wanaotazamwa zaidi YouTube (most viewed) nchini Tanzania, sita ni zao la WCB Wasafi, hao ni Dimond Platnumz, Rayvanny, Harmonize, Mbosso, Zuchu na Lava Lava.

Katika toleo la Ijumaa ijayo tutaangazia namna wasanii wa DR Congo na Nigeria walivyompatia Diamond namba kubwa Afrika. Usikose.