Diamond kicheko kuonana na wanae

Muktasari:
Zari na Diamond Platnumz waliacha mwaka 2018, kwa kile Zari alichosema kuwa msanii huyo amekuwa akimsaliti.
JANA Alhamis Novemba 5, 2020 itakuwa siku ya historia kwa msanii wa Tanzania Diamond, Platnumz, baada ya kukutana na watoto wake, ambao hakuonana nao kwa miaka miwili.
Watoto hao ni Nillan na Latifa ambao alizaa na mjasirimali kutoka Uganda, Zarina Hassan maarufu Zari.
Zari na Diamond kwa muda wa miaka miwili hawakuwa katika mahusiano mazuri ambayo pia yaliathiri ukaribu wa watoto na baba yao.
Wawili hao mahusiano yao yalikufa tangu Februari mwaka 2018, na hii ni baada ya Zari kutangaza jambo hilo kupitia ukurasa wake wa Instagram, kwamba msanii huyo amekuwa akimsaliti kwa kuwa na wanawake wengine.
Hata hivyo mawasiliano ya wawili hawa yalionekana kurejea Aprili, 2020 na hii ni baada ya Zari kumnanga Diamond kwa hatua yake ya kutangaza kuzilipia familia 500 kodi ambapo mama huyo wa watoto watano, alisema msanii huyo anafnya hivyo kwa watu huku akiwa hajui watoto wake Afrika Kusini wanakula nini.
Unaweza kusema kampeni hiyo ndio ilirejesha amani kati yao, kwani Diamond alipohojiwa na moja ya vituo vya televisheni nchini alikiri ujumbe huo wa mama watoto wake kumuumiza kiasi cha kutaka kumjibu vibaya lakini uongozi wake ulimsihi asifanye hivyo.
Badala yake waliyazungumza kidiplomasia na kuyamaliza na kuanzia hapo amani kati yao ikareje huku akieleza kuwa baada ya janga la corona kuisha watu watawaona wakiwa sawa na familia yake hiyo, na kutua kwao nchini ndio kukamilika kwa ahadi hiyo.
Kuanzia jana usiku, video mbalimbali zilisambaa katika mitandao ya kijamii, zikionyesha kuanzia mapokezi aliyoyafanya Diamond kwa familia yake mpaka walipokuwa nyumbani kwake Mbezi Beach.
Ukiachilia mbali kuonekana anaogelea na watoto wake katika bwawa la muda la kutengeneza, pia asubuhi ya leo Ijumaa Diamond ameonekana akiwa anawafundisha kucheza 'pulltable' watoto wake.
Alichokisema Zari
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwasili nchini, Zari amesema amekuja Tanzania kwa ajili ya watoto kumuona baba na bibi yao, kwa kuwa walikuwa na hamu ya kufanya hivyo muda mrefu.
Mbali na watoto hata baba yao amesema alikuwa na hamu ya kuwaona watoto wake, lakini kutokana na kubanwa na ratiba alishindwa kufanya hivyo.
Wakati wapi atalala, amesema anachoangalia ni yeye yupo hapa kwa ajili ya watoto, hata akilala nyumbani kwa Diamond haoni kama kuna shida kwa kuwa wao ni wazazi.