Bifu la Diamond na Ali Kiba lilianzia hapa?

Muktasari:
- Aprili 2016 Alikiba katika mahojiano na kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio alieleza jinsi alivyokuwa na wakati mzuri kufanya kazi na Queen Darleen na kusema anatamani kumuona tena kwenye muziki.
Ingawa hakuna ajuaye hasa bifu kati AliKiba na Diamond lilianzia wapi, lakini yapo maneno mengi mitaani yanayozungumzwa. Hayo yote yanabakia kuwa nadharia tu ya tofauti zinazodaiwa kuwapo kati ya wakali hao wawili wa Bongofleva waliojizolea mashabiki wengi ndani na nje ya nchi. Ukweli wa mambo wanaujua wao wenyewe.

Hata hivyo, mwaka 2006 Mwanahawa Abdul Juma maarufu kama Queen Darleen aliachia wimbo wake maarufu 'Najua Nakupenda' akimshirikisha Alikiba ambaye naye alikuja kumpa shavu katika ngoma yake 'Ndio Yule' kutoka kwenye albamu yake ya pili, Ali K 4Real (2009) chini ya G Records.
Wakati hayo yanajiri Diamond Platnumz ambaye ndiye mmiliki wa WCB Wasafi alikuwa bado hajatoka kimuziki. Utakumbuka Diamond alitoka mwaka 2009 baada ya kuachia wimbo 'Kwamwabie' uliobeba jina la albamu yake ya kwanza.
Aprili 2016 Alikiba katika mahojiano na kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio alieleza jinsi alivyokuwa na wakati mzuri kufanya kazi na Queen Darleen na kusema anatamani kumuona tena kwenye muziki.
“Alikuwa mkongwe katika gemu na tulikuwa na ukaribu sana. Kiukweli muda mwingi huwa ninammisi sababu mimi na yeye kuna vitu vingi tulikuwa tukiendana kama washikaji, muda mwingine akili yangu na yake ni kama sawa," alisema Alikiba.
Miezi miwili mbele yaani Juni 2016 Queen Darleen akatambulishwa WCB Wasafi. Tangu hapo ukaribu wa mwimbaji huyo na Alikiba ukawa ndio mwisho kutokana na kile kinachotajwa kukosekana kwa maelewano kati ya Diamond na Alikiba.
Baada ya kusaini WCB Wasafi miongoni mwa mambo yaliyoacha maswali huko mbeleni ni kitendo cha Queen Darleen kutotumbuiza wimbo aliofanya na Alikiba (Najua Nakupenda) kwenye jukwaa la Wasafi Festival na kuibua hisia huenda lebo hiyo imemkataza.

Hata hivyo, Queen Darleen akizungumza na show ya Block 89 ya Wasafi FM hapo Juni 2019 alikanusha hilo kwa kueleza muda anaopewa kwenye tamasha hilo hamruhusu kutumbuiza hadi nyimbo za zamani wakati anazo mpya zinazofanya vizuri.
Ukaribu wa Queen Darleen na Alikiba kwa kipindi cha nyuma uliwafanya watu kuhisi wawili hao ni wapenzi, lakini Darleen Januari 2017 alikanusha tena hilo katika mahojiano na EATV na kusema hakuna kingine kati yao zaidi ya urafiki.
“Alikiba alikuwa mshikaji wangu, yaani ni ndugu kabisa, hivyo watu waliweza kuona natoka naye kwa kuwa nilikuwa karibu naye. Nazunguka naye mara kwa mara karibu sehemu zote, ila hajawahi kuwa mtu wangu," alisema Queen Darleen.
Hata hivyo, Alikiba kupitia wimbo wake, Mediocre (2020) unaoaminika na wengi kuwa unamlenga Diamond kwa njia moja ya nyingine, kuna mstari anasema: "Sichezi na dada zangu, nacheza dada yako".
Kauli hiyo ndio ikatoa picha halisi kuna kitu katikati ya Alikiba, Diamond na Queen Darleen kwani hata mistari mingine katika wimbo huo inaonyesha hivyo.
Ikumbukwe hapo awali Diamond alimchana vilivyo Alikiba kupitia wimbo wa Fid Q, Fresh Remix (2017) ambapo alishirikishwa pamoja na Rayvanny.
Hivyo Alikiba akaja kujibu kupitia Mediocre, mathalani katika ngoma hiyo Alikiba anajiita mtoto wa Kariakoo ambaye kwake ushamba ni mwiko. Ukirudi kwenye Fresh Remix, Diamond anajiita Simba kutoka Mbuga ya Tandale.
Pili; kupitia Fresh Remix, Diamond anajitambulisha kama Baba Tiffah na Nillan, halafu ukirudi kwa Mediocre, Alikiba anasema unaweza kumuita King Kiba, Baba Keyaan, mtoto wake wa kwanza na mkewe Aminah kutoka Mombasa, Kenya.
Ushindani huo unazidi kutoa picha huenda Diamond alimsaini Queen Darleen ili kumuweka mbali na hasimu wake kimuziki, Alikiba ambaye angeweza kumtumia kupambana naye, hivyo huenda hakuwa na mpango kazi wa kumfikisha mbali kimuziki.
Kuna wanaohisi hivyo kwa sababu ni takriban miaka minne sasa bila Queen Darleen kutoa wimbo wowote ule. Mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa Aprili 1, 2020 alipoachia ngoma, Bachela akimshirikisha Lava Lava.
Huyu ndiye msanii pekee wa WCB Wasafi ambaye hajatoa albamu wala EP. Hata D Voice ambaye alitambulishwa Novemba 2023 tayari ametoa albamu 'Swahili Kid' yenye nyimbo 10, huku akiwashirikisha Diamond, Mbosso, Lava Lava na Zuchu.
Ajabu zaidi kwa muda huo hajashirikishwa na msanii yeyote yule wa Bongofleva na hata wale wa WCB Wasafi ambao wameachia albamu na EP zenye nyimbo zaidi ya 60. Hawampi kabisa kolabo.
Tangu Queen Darleen yupo WCB Wasafi zimetoka albamu nne; A Boy From Tandale (2018) yake Diamond, Sound From Africa (2021) yake Rayvanny, Definition of Love (2021) yake Mbosso, Swahili Kid (2023) yake D Voice lakini hakuna hata moja aliyoshirikishwa.
Vilevile zimetoka EP nane 'Afro Bongo' yake Harmonize, 'Flowers', 'New Chui' na 'Flowers II' zake Rayvanny, 'I Am Zuchu' yake Zuchu, 'Promise' yake Lava Lava na 'First of All (FOA)' yake Diamond na 'Khan' yake Mbosso, huku nako kote hajaambulia kitu.
Kwa ujumla Queen Darleen ndiye msanii wa WCB Wasafi aliyetoa nyimbo chache zaidi kuliko yeyote yule licha ya kuwepo katika lebo hiyo kabla ya Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice. Hadi sasa chini ya lebo hiyo Darleen ameachia nyimbo saba yaani hadi Voice kamzidi!