Ben Pol : Nina pesa za kumtunza Anerlisa, silelewi mjue

Muktasari:
Mengi yamezungumza kuhusu penzi la Ben Pol na mrembo huyo wa mtoto wa bilionea mmoja pale jijini Nairobi, Kenya. Lakini, juzi kati Ben Pol akatia timu ndani ya ofisi za Mwananchi Communications Ltd, ambako magazeti ya Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizen yanazalishwa na kukutana na timu ya waandishi, na bila kupepesa macho akafunguka kila kitu.
UKIISIKIA sauti ya msanii wa Bongo Fleva, Benard Paul ‘Ben Pol’ ni nyororo, inayovuta hisia ya moyo kusikiliza anachokiimba. Neno moja baada ya lingine, kutokana na kipaji alichojaaliwa na Mungu.
Ben Pol, ambaye alitamba na ngoma kama Moyo Mashine, Nikipata, Ntalala Nawe na sasa ukipata mtaani habari ya mjini ni Ebeneza inayotamba kila kona. Kwa sasa jamaa amezama kwenye penzi la mrembo kila mmoja w Kenya, Anerlisa Muigai.
Mengi yamezungumza kuhusu penzi la Ben Pol na mrembo huyo wa mtoto wa bilionea mmoja pale jijini Nairobi, Kenya. Lakini, juzi kati Ben Pol akatia timu ndani ya ofisi za Mwananchi Communications Ltd, ambako magazeti ya Mwanaspoti, Mwananchi na The Citizen yanazalishwa na kukutana na timu ya waandishi, na bila kupepesa macho akafunguka kila kitu.
Mara baada ya kutua na kupokewa na timu ya waandishi wa Mwanaspoti, Ben Pol alikuwa na sura iliyojaa tabasamu huku kinywani akiwa amejaa maneno ya hekima na yenye kumtukuza Mungu.
Kama huwezi kujua kwamba, jamaa anaishi maisha Fulani ya kishua sana. Yaani kwa kifupi Ben Pol ni bonge la mfalme, lakini hana mbwembwe kabisa kama ilivyo kwa straika mpya wa Aston Villa, Mbwana Samatta.
Hata hivyo, Ben Pol anafichua kuwa hana sababu ya kuweka hadharani maisha yake na siku zote anapenda kuonekana ni mtu wa kawaida na mwenye kuishi maisha ya ukweli.
“Watanzania wanafahamu hili, naishi kawaida sana na sipendi mtu anakuja kwangu anaanza kujipanga namna ya kuzungumza, wasifanye hivyo, napenda tuwe tunapiga stori za kawaida,” anasema.
USTAA ULIVYONYANYASA
Ben Pol anafunguka namna anavyonyanyasika pindi anapotaka kujichanganya na jamii yake. Jina lake lilianza kutamba kila kona ya Bongo kabla ya mafanikio kuchukua nafasi yake hivyo, alipitia kwenye mazingira magumu.
Mwaka 2010, Ben Pol aliachia ngoma mbili za Pata Raha na Nikikupata na hapo jina lake likapanda. Kila shabiki wa muziki akataka kumfahamu na kusikiliza ngoma za Ben Pol na hapo ikawa shida kubwa.
“Sikuwa na mkwanja licha ya kuwa na jina, sasa nilizoea kutumia usafiri wa daladala kwa mizunguko yangu ya hapa na pale. Sasa nilikuwa napanda zangu daladala nashikilia bomba na hapo nikawa nalipiwa sana nauli.
“Haaaaa nakumbuka hayo maisha yalinipa tabu sana, jina lilikuja haraka kuliko pesa. Lakini bado mama alikuwa ananipa nauli ya kwenda studio, niliteseka kama miezi sita,” anasema.
ALIANZA KUIMBA TANGU SHULE
Anasema ameanza kuimba tangu anasoma shule ya msingi Vingunguti mwaka 1997 hadi 2003, ambapo alijiunga na Dar es Salaam sekondari ya Dar es Salaam mwaka 2004 mpaka 2007.
“Nilikuwa na akili sana shuleni, nilipenda hesabu na biashara, kidato cha nne nilipata daraja 2 na kidato cha sita nilipata daraja la tatu, lakini akili yangu ilikuwa imejaa muziki tu.
“Baadaye nikajiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), lakini bahati mbaya sana nikasimama shule kwa sababu shoo zilianza kumiminika.
“Kama nisinhetoka kimuziki basi ningekuwa mhasibu ndio kazi ninayoipenda kwa sababu mimi ni mtaalamu wa mahesabu mpaka kesho,” anasema.
RUGE ALIMJENGEA UJASIRI
Anasema baada ya kumaliza kidato cha sita alikwenda kujiunga na THT ambapo, marahemu Ruge Mutahaba alikuwa mkurugenzi na kitu kikubwa alichojifunza kwake ni kupangilia sauti na ujasiri.
“Nilipita kwenye mtihani mingi, nikaweka nguvu katika sauti na ujasiri…wenzangu walijifunza vitu vingi. Ruge amenisaidia sana hapa nilipo,” anasema.
HII NI PESA NDEFU KWAKE
Kila mwenye mafanikio ni lazima awe na matukio ya kukumbuka na hilo kwa Ben Pol haliwezi kumtoka kichwani mwake.
“Nakumbuka nilienda kufanya shoo ya kwanza Njombe na ngoma zangu za ni Pata Raha na Nikikupata, zilikuwa gumzo kinoma. Menejimenti yangu ikanilipa Sh 150,000 ambayo nilitumia kununulia nguo.
“Niliiona kubwa kwa kipindi kile, nikanunua nguo ili nionekane vizuri nikiwa napanda jukwaani,” anasema.
JINA LAKE HALISI APEWA GEREZANI
Anasema wakati mama yake ana mimba yake baba yake mzazi alifungwa Gereza la Keko mwaka 1989 na mwaka 1990 akiwa bado yupo ndani, jambo lililomfanya kukaa siku 40 bila jina.
“Nilikaa siku 40 bila kupewa jina, nasimuliwa kuwa mama alinibeba mpaka Gereza la Keko ambako baba alifungwa ndipo nikapewa jina la Majuto, wakati nabatizwa nikabadilisha nikaitwa Benard Paul.
“Ingawa mpaka sasa baba yangu hajawahi kuniambia ni kosa gani lilimpeleka jela zaidi yakumuona akijutia sana, ananipenda nakujivunia mimi licha ya kuzaliwa na changamoto ila Mungu kaniinua,” anasema.
Hata hivyo, anafichua kuwa staili yake ya upambanaji ameiga kwa baba yake, ambaye alikuwa mfanyabiashara.
“Baba alianza kutumia gari kabla ya mimi kuwa staa, alijenga mjengo wake na nilichofanya ni kuwaboreshea tu baadhi ya vitu,” anasema ambaye anamiliki ndinga tano matata zikiwemo Range Rover, Mercedes Benzi ambazo huzitumia kwa misele yake ya town.
MZUKA KABLA YA KUPANDA JUKWAANI
Kila msanii ana kitu anakifanya kabla ya kupanda jukwaani kuimba kwa upande wake anasali, ana kunywa chai kwa wingi na kufanya mazoezi kidogo kujiweka freshi.
BATA LA DUBAI SASA
Juni 19, mwaka jana zilisambaa picha za Ben Paul na mchumba wake Anerlisa wakiwa kwenye kiwanja maarufu cha maraha maarufu kama kwa Salt Bae, kinachomilikiwa na Nusret Gökçe. Kiwanja hicho ni maarufu kwa mastaa kibao wa soka Ulaya, ambao wamekuwa wakienda hapo kwa ajili ya kupata nyama choma na starehe zingine.
Baadhi ya mastaa ambao wamewahi kuonekana kwa Salt Bae ni Cristiano Ronald, Lionel Messi, Paul Pogba, Jodan Sancho, Frank Ribery na Diego Maradona. Lakini, kwa hapa Bongo aliyewahi kutia maguu pale ni Ben Pol.
Hata hivyo, anafichua kuwa kuingia kwenye kiwanja hicho ni lazima ujipange kinoma. Anasema ni viwanja kama vingine, lakini starehe zake ndio gharama hasa kama unataka kuhudumiwa na Salt Bae mwenyewe, lakini uvunje akaunti kimtindo.
“Ingawa sipendi kuzungumza sana matukio yangu ninapokuwa mapumzikoni, lakini pale kwa Salt Bae aliteketeza kama Sh5 milioni.
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa anatumia mkwanja wa mchumba wake, Ben Pol alijibu:
“Nashangaa sana na sijui kwanini watu wanajifanya hawajui ninachofanya, yule ni mchumba wangu na ninawajibika kumhudumia…nalipa mwenyewe ndi sababu natafuta pesa.”
NDEGE BINAFSI
Hivi karibuni Ben Pol alionekana akiwa ametulia kwenye ndege binafsi akiwa kwenye safari zake kwenye miji ya New York na Miami, Marekani.
“Ni kweli nilitumia ndege binafsi, nilichelewa ndege niliyokuwa nisafiri nayo na nilitakiwa kuwahi vikao vya kazi hivyo, nikatafuta njia mbadala nayo ni kukodi ndege ili niende na muda. Kuna watu wananiona kama vile nakula bat asana, hapana niko kwenye majukumu,” anasema.
BONGE LA MKULIMA MJUE
Kuna watu wanamchukulia poa Ben Pol mjue na mwenyewe anawaangalia tu kwani, kuna mambo mengi kuhusu yeye hawafahamu. Sasa anafunguka kuwa, kwanza anampenda sana mchumba wake, Anerlisa na sio kwa sababu ya pesa.
“Kuna watu hawaelewi kabisa, nje ya muziki mimi nina kazi nyingi sana nafanya. Ninauza muziki wangu kwenye mtandao na ni Balozi wa UN, WWF na Will AIDS, hivyo mambo yote haya yananipa pesa za kujikimu kimaisha.
“Hata washkaji zangu wananiona kama nipo na Anerlisa kwa ajili ya mali zake, hapana kwa sababu wanafahamu tangu zamani kuwa nafanya biashara kibao ikiwemo kuuza nafaka na zabibu.
“Pia, shoo zangu za nje ya nchi zinanipa pesa za maana, ninafanya shoo kwenye nchi za Italia, Ufaransa, China, Uingereza, Marekani na kwingineko.
“Hii ni tabia mbaya kwamba tuogope kuwapenda wanawake wanaojituma sio sahihi, kila mtu anastahili kupendwa kulingana na mtu anachokuvutia,” anasema.
Kesho Jumamosi, Ben Pol ataeleza kuhusu penzi la Ebitoke na nini kilitokea. Ataeleza kuhusu mijengo yake na mikakati ya ndoa na Anerlisa. Hakikisha hukosi.