Babu Tale achungulia jela tena

What you need to know:

  • Baada ya kuponea chupuchupu kutupwa jela mwaka 2018, sasa mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Shabani Taletale, maarufu kama Babu Tale anachungulia tena jela baada ya mchakato kumtupa jela kuanza tena upya.

Dar es Salaam. Baada ya kuponea chupuchupu kutupwa jela mwaka 2018, sasa mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Shabani Taletale, maarufu kama Babu Tale anachungulia tena jela baada ya mchakato kumtupa jela kuanza tena upya.

 Babu Tale ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni inayojihusisha na shughuli za burudani, Tip Top Connections Company Limited yuko hatari kufungwa jela kutokana na kushindwa kumlipa mhadhiri wa dini ya Kiislam, Sheikh Hashim Mbonde, fidia ya Sh250 milioni.

Tayari Sheikh Mbonde ameshafungua maombi Mahakama Kuu akiiomba mahakama hiyo iamuru Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya (Bongo fleva), Abdul Nassib maarufu kama Diamond Platnumz akamatwe na afungwe kwa kushindwa kumlipa fidia hiyo.

Sheikh Mbonde amefungua maombi hayo dhidi ya Tip Top na Babu Tale baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali taarifa yao ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaamuru kulipa fidia hiyo, Agosti 17, 2022.

Mahakama hiyo iliitupilia mbali taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa, kufuatia maombi ya Sheikh Mbonde, baada ya kukubaliana na hoja zake kuwa kina Babu Tale hawakuweza kuchukua hatua muhimu ndani yaani kuwasilisha sababu za rufaa ndani ya muda.

Maombi hayo ya madai anuani namba 467 ya mwaka 2022 ya Sheikh Mbonde yaliyopangwa kusikilizwa na Jaji Obadia Bwegoge yamepangwa kutajwa mahakamani hapo Oktoba 29, mwaka huu.

Hata hivyo baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali taarifa yao ya kusudio la kukata rufaa, kina Babu Tale nao wamewasilisha maombi mengine ya kibali cha kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa nje ya muda.