Wanasiasa acheni wasanii wachukue fomu

Muktasari:
- Sasa wakati wasanii wamechachamaa kuchukua fomu za kugombea ubunge na udiwani, mara wanaibuka wanasiasa kadhaa na kulaani kitendo hicho. Wanasema “oooh! Wasanii wanachukulia ubunge kitu cha mzaha.” Wengine wanasema, “jamani mnajidanganya. Huku kwenye ubunge wala hakuna pesa” huku wengine wakisema, “kila mchekeshaji anataka kuwa mbunge.”
MWANETU Gabo kachukua fomu. Dogo Stan Bakora kachukua fomu. Mshikaji wetu Mkojani kachukua fomu. Madevu wa Jua Kali kachukua fomu na shangazi yetu Aunt Zai wa Jua Kali naye kachukua fomu. Shishi Baby almaarufu Shilole kachukua fomu. Baba Levo kachukua fomu. Jaku Boy Mwijaku naye kachukua fomu. Konde Boy ilikuwa chupuchupu achukue fomu naona akajishtukia akasema sichukui, nimeambiwa nikiwa mbunge sitakiwi kusema ‘Bomboclat’.
Sasa wakati wasanii wamechachamaa kuchukua fomu za kugombea ubunge na udiwani, mara wanaibuka wanasiasa kadhaa na kulaani kitendo hicho. Wanasema “oooh! Wasanii wanachukulia ubunge kitu cha mzaha.” Wengine wanasema, “jamani mnajidanganya. Huku kwenye ubunge wala hakuna pesa” huku wengine wakisema, “kila mchekeshaji anataka kuwa mbunge.”
Yaani wanasiasa wanajiongelesha kama vile wao pekee ndio wenye akili, ndio wenye haki ya kuwa viongozi kwenye taifa hili. Na unajua nini, wanachosema kina ukweli ndani yake - ubunge sio kitu rahisi. Wabunge ndio wanasaidia kupitisha sheria za nchi hii. Ndiyo watu wanaokwenda kutuwakilisha na kutusemea bungeni. Ndio watu wanaotakiwa kuwa namba moja kuiwajibisha serikali. Sasa ukimpata mtu kama braza'angu Mkojani sijui kama ataweza kumudu kujenga hoja nzito za kututetea wananchi. Sema hata kama mimi na wewe tunajua kwamba wasanii wengi waliochukua fomu hawana uwezo wa kuzibeba hizo nafasi wanazozitaka, lakini mi' naona wachukue tu - tena wachukue kwa wingi. Ikiwezekana kila msanii achukue fomu kama inawezekana. Kwa sababu hao wanasiasa wanaoponda wasanii kuchukua fomu tuliwapa miaka 60 ya kuwafanya wasanii wasitamani hizo nafasi, lakini miongoni mwao wakashindwa. Badala yake wanatengeneza mazingira ya kila mtu kuona anaweza na anafaa kuchukua nafasi ya uwakilishi.
We' unadhani nani asiyetaka kupata mkwanja kila akiingia kwenye kikao cha Bunge? Nani asiyetaka ndinga shangingi kali na kiwese juu. Nani asiyetaka mikopo mikubwa? Nani asiyetaka mamilioni mengi kila baada ya miaka mitano Bunge linapomalizika? Nani asiyetaka mambo mazuri hivyo? We' Mkojani anaigiza mchana - usiku, kila siku ana-aplodi video Youtube, mabasi ya mikoani yanaonyesha muvi zake kwa fujo, mtaani watu wanampenda balaa, lakini usikute mpaka leo hii hana uwezo wa kununua gari kama analopata mbunge - kwanini asiutake ubunge?
Jaku Boy Mwijaku kila kukicha ni kutengeneza kontenti za kichawa, Mara anafuta viatu vya mabosi. Mara anagalala chini akitaja majina ya mabosi. Mara asifie mabosi wamepoa ili akusanye laki mbili tatu za kujenga ghorofa lake la ‘BILIONI’. Sasa kama kuna njia ya kumfanya ajenge ghorofa lake bila kujidhalilisha namna hiyo kwa nini asiende? Mkiambiwa wasanii ni kioo cha jamii, basi ndio hii sasa. Mkiona wasanii wamedharau nafasi za uongozi za kisiasa zenye kubeba mustakabali wa taifa kama ubunge na sasa kila mtu anachukua fomu - ni sawa na kusema jamii pia imedharau nafasi zenu, inaona hakuna cha maana mnachofanya zaidi ya kujipigia mipande tu.
Mnachukua mihela halafu mkikutana na wasanii baa mnataka wawapapatikie nd'o muwanunulie vi-moet kwa masimango - tena mbele ya warembo. Sasa wasanii wamechoka na wao wanazifuata hizo fursa hukohuko bungeni. Msiwaambie hakuna fursa kama kweli hakuna fursa basi msiwazuie, waacheni waje waone wenyewe. Wanangu wasanii, hakuna kusikiliza mtu aluta kontinyua. Chukueni fomu. Bungeni lazima tufike. Na mkifika msitusahau washkaji zenu.