ATM YA WIKI: Achana na skendo, Bieber na pesa

Muktasari:
- Ukiondoa yale yanayoendelea, Bieber ni mmoja kati ya wanamuziki matajiri waliofanikiwa kutengeneza pesa za kutosha kupitia muziki.
CARLIFONIA, MAREKANI: MOJA kati ya mambo yaliyoshika vichwa vya habari hivi karibuni ni mashtaka yanayomkabili msanii Puffy Daddy anayefahamika pia kama P Diddy anayedaiwa kuwafanyia unyanyasaji wa kijinsia watu mbalimbali waliotajwa kwenye kesi hiyo akiwamo mwanamuziki kutoka Canada, Justin Bieber.
Ukiondoa yale yanayoendelea, Bieber ni mmoja kati ya wanamuziki matajiri waliofanikiwa kutengeneza pesa za kutosha kupitia muziki.

ANAPIGAJE PESA
Kupitia muziki kwa mwaka anadaiwa kukunja karibia Dola 80 milioni hadi Dola 100 milioni ambazo zinatokana na shoo na matamasha mbalimbali anayoenda kutumbuiza.
Mbali ya mkwanja wa shoo, Bieber ana biashara zake binafsi na mikataba ya udhamini na kampuni mbalimbali ambazo amekuwa balozi wao.
Anafanya kazi na kampuni kama Nicole by OPI, Walmart, Adidas, Calvin Klein, na Schmidt’s Naturals. Pia ana kampuni yake inayouza manukato mbalimbali kama Someday, Girlfriend na Justin Bieber Collector’s Edition.
Mwaka 2019, alianzisha kampuni yake ya nguo iitwayo Drew House, pia mwaka 2020, alishirikiana na kampuni ya Crocs kuzindua viatu aina ya Crocs x Justin Bieber.
Pia mwaka huo alishirikiana na kampuni za Tim Hortons na Vespa. Mwaka 2022 alianzisha kampuni yake ya kuzalisha maji safi iitwayo Generosity.
Kwa ujumla ana utajiri unaofikia Dola 300 milioni ambazo ni majumuisho ya pesa anazopiga kutokana na shoo na matamsha pamoja na biashara zake binafsi.

MJENGO
Mwaka 2012, akiwa na umri wa miaka 18, alitoa Dola 6.5 milioni kununua mjengo wa kifahari huko Calabasas, California, lakini aliiuza 2014 baada ya majirani zake kumfungulia mshtaka kutokana na makelele yaliyokuwa yanapigwa kutoka nyumbani kwake mara kwa mara alipokuwa anafanya sherehe na marafiki zake.
Bieber alilipa faini ya Dola 80,000 na kuamua kuuza nyumba hiyo kwa Dola 7.2 milioni ambayo ilinunuliwa na Khloe Kardashian, ambaye ni dada wa Kim Kardashian.
Baada ya kuuza mjengo huo, alianza maisha ya kupanga katika mijengo mbalimbali ya kifahari kwa miaka mitano ambapo mwaka 2019 aliripotiwa kulipa karibia Dola 100,000 kwa mwezi kupanga nyumba huko Toluca Lake, California.
Machi 2019, aliamua kuachana na maisha hayo na akalipa Dola 8.5 milioni kununua mjengo huko Beverly Hills lakini aliiuza mwaka 2021 kwa Dola 7.995 milioni.
Agosti 2020, Justin alitoa Pauni 28.5 milioni kununua mjengo mpya maeneo ya Beverly Hills. Nyumba hiyo ya kitajiri ina karibia kila kitu ndani yake ikiwemo bwawa la kuogelea, studio, sehemu za kuangalia muvi na kufanyia mazoezi.
Majirani zake katika eneo hilo ni watu maarufu kama Denzel Washington, Eddie Murphy, Rod Stewart, na Sylvester Stallone.
Taarifa zinaeleza mwaka 2022 msanii huyu alinunua nyumba kwa Dola 42 milioni, na mbali ya nyumba pia kuna eneo kubwa lenye ukubwa wa heka 2.5. Pia ana mjengo huko Canada maeneo ya Ontario aliyoinunua kwa Dola 5 milioni.
MISAADA KWA JAMII
Bieber amekuwa akitoa misaada kupitia taasisi mbalimbali kama The Children’s Wish Foundation of Canada, Make A Wish Foundation na Believe Charity Drive.
Mwaka 2011 alitoa pesa kusaidia mradi wa kutengeneza miundombinu ya maji nchini Ethiopia.
Taarifa zinaeleza kwa mwaka staa huyu anatoa pesa kutoka kwenye mapato yake ya mauzo ya albamu.

NDINGA ZAKE
Mkali huyo anamiliki ndinga mbalimbali za kifahari kwenye maegesho ya magari. Ndinga hizo ni pamoja na Mercedes-Benz SLS AMG, Fisker Karma, Audi R8,
Bugatti Veyron Grand Sport, Hummer H2,
Cadillac CTS-V, Ferrari F430, Rolls-Royce Wraith,
Mercedes-Benz Sprinter na Lamborghini Aventador S.

MAISHA BINAFSI
Desemba 2010, aliingia kwenye uhusiano na Selena Gomez ambaye alidumu naye hadi mwaka 2018 na baada ya hapo alirudiana na Hailey Baldwin ambaye awali aliwahi kuwa naye kwenye uhusiano kati ya Desemba 2015 na Januari 2016, baada ya kurudiana naye mwaka 2018, wawili hao walivishana pete Julai 2018, kisha wakafunga ndoa Septemba 30, 2019.
Mapema mwaka huu wawili hawa waliripotiwa kupata mtoto wao wa kwanza wa kiume.