Anko Lao... Majibu Konkii

1. ANKO Lao, kijana miaka 23, sina lingine kwako ila kukushukuru kwa ushauri uliowahi kunipa kupitia hapa, kwani kwa sasa nimenunua kiwanja nataka kujenga shule ya chekechea! Ubarikiwe!
Chid Tate Ulaya, Mbezi
Jibu: Kama unachosema ni kweli, nawe ubarikiwe na Mungu akufanikishie ndoto ulizonazo, kwani huu ndo msingi wa kona hii kuona mayanki na wengine mnatoboa na kuacha uduwanzi! Asante!
2. ANKO Lao, binti miaka 27 nina mume tunapendana na ananitimizia kila kitu nikitakacho na kunijali sana, ila tatizo lake ni ulevi tu, nimezungumza naye aache bila mafanikio Nifanyeje?
Fatuma, Mombo
Jibu: Sina hakika huyo jama'ako kama ni mlevi kweli, nahisi ni mtu mwenye stresi zinazomtesa, kwa vile hakuna mlevi anayeweza kutimiza na kuijali familia kwani akili hutawaliwa na pombe. Huyo ni mnywaji na huenda kampani aliyonayo ni tatizo. Shirikisha wazee atakaa sawa. Hivyo tu!
3. ANKO Lao, kijana miaka 21 nina mpenzi tunapendana, ila akija geto huwa amevaa nguo nyingi na huwa hataki kabisa tulicheze rhumba akidai eti pipi ipo katika mfuko. Nifanyeje?
Shadow, Luponde Njombe
Jibu: Wewee jamaa buana, kwa hilo baridi la huko Njombe ulitaka bibie aje na khanga moko? Kama unatamani kula pilau nyama nyingi, we harakisha kuoa, mambo ya kuvizia yatakutokea puani bure. Kazi kwako!
4. ANKO Lao, binti miaka 21 kuna boy tunapendana, lakini ameniambia hawezi kuishi nami hadi kwanza niwe na kazi ya kujishughulisha nayo, kwani kwa sasa hali ni ngumu kwake. Nifanyeje?
Latifa Hakimu, G'Mboto Dar
Jibu: Kwa hali ilivyo ni vyema nawe uwe na chochote cha kujishikiza hata kama ni ususi wa nywele badala ya kuwa golikipa tu, halafu kwa mtoto wa kike sio sifa kutaka kujipeleka kwa msela kabla ya ndoa, utakinaiwa mapema. Jitulize kwenu, kwani hiyo njemba yako ni muoga wa maisha! Hivyo tu.
5. ANKO Lao, kijana miaka 34 napiga kazi ya uvuvi, lakini mambo hayaendi kabisa kwani vyuma vimekaza sana. Nifanyeje?
Hamis Juma, Zanzibar
Jibu: Inategemea uvuvi unaendeshaje na unakitumiaje kile unachokipata katika shughuli hiyo, kama unaingiza kidogo ila unatumia kingi, ujue unajifelisha! Pia iwapo unaendesha uvuvi kienyeji fanya chapu uendeshe kisasa utoboe...ukiona mambo hayaendi, nenda wewe, kaushia uvuvi, upige mishe nyingine maisha yaendelee au ni kazi ya kurithi, hivyo unaogopa kuwaudhi wazee! Wee vipi!
6. ANKO Lao, binti hapa nimezaa na mtu ninayempenda sana, lakini tatizo lake ana mademu wengi, kiasi anashindwa hata kuleta matumizi nyumbani. Naomba ushauri wako, nifanyeje?
Winifrida, Morogoro
Jibu: Hili ndilo tatizo lenu mabinti wa 2000, yaani mnajirahisisha sana na kukubali kuzalishwa kabla hamjaolewa na mwishowe kuwapa mzigo wazazi kuwalea nyie na vitoto vyenu...kilichokuharakisha kuwa mama ni kitu gani, hasa kwa mtu uliyemjua hajatulia? Unalo hilo, pambana na hali yako!
7. ANKO Lao, binti miaka 22 nilichwa na mtu nikiwa na mtoto ana miezi mitatu tu, leo dogo kawa na miaka mitatu huyo mwanamume anapiga simu na kunipa vitisho akimtaka mtoto wake. Nifanyeje?
Julieth Nicolaus, Tanga
Jibu: Ulibugi sana kubebeshwa mzigo kabla ya ndoa tena na mtu asiye na mipango nawe...huyo jamaa kuibuka sasa akileta vitisho ni dhahiri ni kunguru... huyo muoga wa maisha ndo maana alilala mbele kukwepa mzigo. Kwa vitisho anavyotoa mfikishe katika vyombo vya dola akili zimkae sawa. Hivyo tu!
8. ANKO Lao, kijana miaka 33, tatizo langu huwa napenda sana mishangazi, ila baadhi yao ni miyeyusho kwani huwa hawajatulia na sidumu nao. Nifanyeje?
Francis P.A, Tandika
Jibu: Wee bro una hatari...katika dunia hii ya maradhi bado tu unaneng'eneka na mishangazi, badala ya kutafuta mtu wa kumuoa na kujituliza! Ukiendelea na huo uduwanzi wako, ujue mapema huna muda mrefu utarejeshwa kijijini kama kifurushi! Usione sifa kubadili mademu...Shauri yako!
9. ANKO Lao, mama wa watoto watatu wote vidume, ila mume wangu hajatulia, kila mwanamke aliyeachika anapita naye akifikia hatua ya kumpangia mmojawao chumba, wakati mwenyewe hana maisha ya kuitunza familia..natamani kuachana naye, kwani sina mzuka naye kabisa. Nifanyeje?
Amina, Tanga
Jibu: Nilichogundua una wivu na unamfuatilia sana mumewe, kiasi cha kujipa stresi za bure, kwani nahisi hata hayo mengine ni hisia zako tu...ila kama ni kweli mumeo ni kicheche wa sampuli hiyo, ni bora umfikishe kwa wazee muwekane sawa, muhimu ni watoto mlionao, ikishindikana kila mtu ale kona yake, hapo ndoa hakuna tena! Lakini kama unamzushia utakuwa unamkosea sana. Hivyo tu!
10. ANKO Lao, nimetokea kupendwa na mwanamume anayetaka kunioa kabisa na tunapendana kweli, ila wazazi hawataki niolewe naye? Nifanyeje?
Maimuna, Kilosa
Jibu: Sijajua umri wenu ni upi? Ila kama mmepevuka akili, hilo goma ni lenu la kulicheza wenyewe. Lakini ebu kaa na wazazi udodose ujue kipi kinachowafanya wamkatae jamaa, inawezekana kuna siri na pengine wanajua mengi kuhusu yeye kuliko umjuavyo. Usilazimishe ndoa, isije ikakupalia.