AKILI ZA KIJIWENI: Kijiwe kinamuaga Mzee King Kikii

Muktasari:
- Wasanii wengi wa muziki wametangulia mbele za haki lakini kuna wale ambao wamegusa hisia za wengi kama akina TX Moshi William, Marijani Rajabu, Mbaraka Mwinshehe, Maalim Muhidin Gurumo na huyu mzee King Kiki.
MSIBA wa mzee Kikumbi Mwanza Mpango umetuachia majonzi hapa kijiweni na kiukweli tumeguswa sana.
Wasanii wengi wa muziki wametangulia mbele za haki lakini kuna wale ambao wamegusa hisia za wengi kama akina TX Moshi William, Marijani Rajabu, Mbaraka Mwinshehe, Maalim Muhidin Gurumo na huyu mzee King Kiki.
Hawa niliowataja, vifo vyao vimegusa wengi kwa vile wameacha alama ambazo zitadumu vizazi hadi vizazi maana mwanamuziki mahiri ni yule anayeacha nyimbo zinazorithiwa vizazi hadi vizazi.
Ndiyo kama alichokifanya Mzee wetu Kiki ambaye ameacha nyimbo mbalimbali zinazogusa hisia za mamilioni ya Watanzania japo aliziimba zamani sana na miaka mingi imeshapita tangu wakati huo hadi sasa.
Mfano ni wimbo wa ‘Kitambaa Cheupe’ ambao leo unajulikana na kupendwa na vijana na wazee, wanaume kwa wanawake, watoto na wakubwa na watu wa makabila, rangi na imani tofauti.
Mzee katika utunzi wa ile nyimbo na nyinginezo inaonekana alikaa na kutulia na kushusha vitu ambavyo leo vikipigwa vinaweza kuwainua hata viongozi wakubwa wa nchi na watu wa kada nyinginezo.
Kuna fundisho kubwa ambalo vijana wa sasa hasa ambao wamejikita katika tasnia ya muziki, wanaweza kulipata kutoka kwa maisha ya marehemu Mzee King Kikii nalo ni nidhamu, juhudi na ubunifu katika kazi.
Wasiimbe kwa kutazama masilahi yao binafsi bali wahakikishe wanatoa nyimbo ambazo zitagusa kundi kubwa la watu na kuacha alama katika jamii kwa miaka mingi na kuwajengea heshima inayodumu kwa muda mrefu.
Tumejipa dakika moja ya kusimama hapa kuomboleza msiba wa gwiji wa muziki Tanzania ambaye aliziacha nyimbo zake zimpe heshima badala ya kujisifu yeye mwenyewe.