Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Achana na AFL, Alikiba ni zaidi ya mnyama

STAA wa Bongofleva kutokea Kings Music, Alikiba anaizungusha dunia yake isiyokuwa na kelele nyingi, ni vitendo zaidi ndivyo vinachukua nafasi na kumfanya kuwa na rekodi zake za pekee ukilinganisha na washindani wake kimuziki. 

Utakumbuka Alikiba alivuma kimuziki baada ya kuachia albamu yake ya kwanza, Cinderella (2007) chini ya G Records, zilifuata albamu nyingi kama Ali K4Real (2009) na Only One King (2021) iliyoshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2021.

Ni wiki moja imepita tangu Alikiba ametumbuiza katika ufunguzi wa mashindano ya African Football League (AFL) uliofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kwa kukaribisha pambana kati ya Simba SC dhidi ya Al Ahly ya Misri. 

Alikiba ndiye msanii pekee wa Bongofleva aliyechaguliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutumbuiza katika mashindano hayo ambayo ni kwa mara ya kwanza yanafanyika kwa kushirikisha klabu nane za Afrika.

Wimbo aliyotumbuiza siku hiyo ni “Sumu” ambao waandaji ndio waliupendekeza, huu ni wimbo wa kwanza wa Alikiba wenye mahadhi ya Amapiano ambao aliurekodi baada ya kususia kwa muda mrefu aina hiyo ya muziki kutoka Afrika Kusini.

Sumu ya Alikiba inasikika katika tukio kubwa la AFL ambalo dunia nzima ya soka ililifuatilia, hayo yanajiri kipindi kifupi baada ya kuwepo mjadala kuhusu ni wimbo upi wa Amapiano Bongo uliofanya vizuri kimataifa, hapa Alikiba anachukua pointi zake tatu safi.

Ikumbukwe Alikiba ambaye ni shabiki wa Simba SC na Liverpool FC, sio mgeni katika soka na matukio yake, ndiye staa mkubwa wa kwanza wa Bongofleva kucheza Ligi Kuu Soka Tanzania Bara baada ya kusajiliwa na Coastal Union.

Alikiba ndiye msanii pekee wa Bongofleva aliyechaguliwa kushikiri katika mradi wa One8 (2010) uliotoa wimbo “ Hands Across The World” ulioandikwa na kutengenezwa na R. Kelly kutokea Marekani ambaye alisikika pia.

Ni mradi uliokusanya wasanii wengi wa Afrika kwa wakati mmoja, ukimtoa Alikiba, pia walikuwepo Amani (Kenya), Navio (Uganda), 2Face (Nigeria) 4x4 (Ghana), Fally Ipupa (DR Congo), JK (Msumbiji)  na Movaizhaleine (Gabon).

Alikiba ndiye aliimba verse ya kwanza ya wimbo huo, sio kwa bahati mbaya bali uwezo, R. Kelly ambaye alikuwa bado yupo juu kimuziki, alikubali uwezo wa Alikiba na ndiye alimpa kauli mbiu “Pap It In” ambayo amekuwa akiitumia katika nyimbo zake.

Ikumbukwe baada ya hapo ndipo Seven Mosha akawa Meneja wa Alikiba aliyekuja kumpatia mafanikio makubwa, Seven alikuwa akisimamia wasanii wa Afrika Mashariki katika mradi huo, hivyo baada ya kumalizika akamuomba waendelee kufanya kazi pamoja.

Chini ya Seven, Alikiba alishinda tuzo za kimatifa kama All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Aje) ft. M.I (Mr. Incredible), pia alishinda MTV Europe Music Awards  (MTV EMA) 2016 kama Msanii Bora Afrika. Mwaka 2017 Alikiba aliandika rekodi kama msanii wa kwanza aliyesainiwa Sony Music Entertainment Africa kwa video ya wimbo wake (Aje) kufikisha ‘views’ zaidi ya milioni 5 katika mtandao wa YouTube kitu kilichopelekea lebo hiyo kumpatia tuzo (plaque).

Huyu ndiye msanii pekee Bongo ambaye ameshinda tuzo zaidi ya tano na kuwa kinara katika misimu miwili tofauti ya tuzo za muziki Tanzania (TMA), alifanya hivyo mwaka 2015 akishinda tuzo sita na mwaka 2022 akiondoka na tuzo tano. Katika albamu yake, Only One King (2021) yenye nyimbo 16, Alikiba alifanya video za nyimbo nane ambazo ni Infidele, Ndombolo, Salute, Jealous, Oya Oya, Bwana Mdogo, Utu na Niteke, hivyo kuandika rekodi kama albamu iliyotoa video nyingi kwa mwaka huo.

Only One King ilizizidi albamu zilizotoka mwaka huo kama Sound From Africa (Rayvanny), Defination of Love (Mbosso), High School (Harmonize), Air Weusi (Weusi), 20 (Lady Jaydee), Asante Mama (Dogo Janja), Experience (Stereo), The Gift of Life (Best Naso) na kadhalika.

Na Alikiba amekuwa na uwezo wa kurudi katika muziki kwa kishindo baada ya ukimya wa muda mrefu, mathalani alipoachia wimbo wake, Seduce Me (2017) ikiwa ni baada ya mapumziko ya mwaka mzima alipata mapokezi makubwa.

Video ya wimbo huo ilifikisha ‘views’ milioni 1 ndani saa 37 na kuweka rekodi kama video iliyotazamwa zaidi YouTube Bongo kwa muda mfupi, huku ikivunja rekodi ya wimbo, Salome (2016) wake Diamond Platnumz uliopatata ‘views’ milioni 1 kwa saa 48.

Na tangu mwaka huu umeanza wimbo wa Alikiba ‘Mahaba’ ndio wimbo wenye mafanikio mkubwa zaidi YouTube Bongo bila kuwa na video rasmi (official video). Wimbo huo umefikisha ‘views’ zaidi milioni 18 ndani ya miezi nane na kushika nafasi ya tatu katika orodha ya nyimbo za Alikiba zenye mafanikio katika mtandao huo kwa muda wote.