TIMUA VUMBI : Tumebaki na AFCON moja tu ya Taifa Stars

Thursday April 25 2019

 

By Mwanahiba Richard

TIMU ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ iliondolewa kwenye michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U17) ambayo inamalizika Aprili 28 yaani wikiendi hii.

Serengeti Boys walicheza mechi tatu na kupoteza zote dhidi ya Nigeria 5-4, dhidi ya Uganda 3-0 na ya mwisho dhidi ya Angola 4-2. Hiyo ilimaanisha kwamba Serengeti imeondolewa kwenye michuano hiyo ikiwa timu pekee ambayo haikuambulia pointi hata moja kati ya timu nane zilizoshiriki, huku ikibebeshwa mzigo wa mabao 12. Hapakuwa na timu nyingine iliyofungwa zaidi ya jumla ya mabao matano katika hatua ya makundi mwaka huu.

Serengeti Boys ni timu ambayo maandalizi yake yalianza kufanywa muda mrefu ikiwa na maana ya zaidi ya miaka miwili hadi kufikia hatua hiyo ambayo iliipata bila ya jasho baada ya Tanzania kupewa uenyeji wa kuandaa michuano hiyo.

Matarajio ya wengi ilikuwa ni kuona timu hiyo ikifanya mambo makubwa zaidi kwa maana ya kupata matokeo mazuri na kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana ambayo itafanyika baadaye nchini Brazili.

Matarajio hayo yalitokana na timu hiyo kushiriki mashindano mbalimbali ya maandalizi ya kimataifa ingawa haikufanya vizuri lakini matokeo hayo hayawakuwakatisha tamaa wakiamini kwamba makosa yanafanyiwa kazi kabla ya kuanza michuano hiyo mikubwa.

Serikali, wanasiasa, wanamuziki na wadau wengine wa soka nchini walikuwa bega kwa bega na timu hiyo ingawa jitihada kubwa zilionekana mwishoni kama kuhamasisha ikiwamo kuwahidi zawadi za pesa na magari.

Advertisement

Hata hivyo, zawadi hizo zimekwenda na maji kwani hawajafuzu wala kufika popote kwenye michuano hivyo hivyo huenda watakachopata ni posho zao za kawaida ama malipo kama yapo ambayo wamewaandalia kama kifuta jasho chao ingawa lengo kubwa ilikuwa ni kufuzu Kombe la Dunia ama kutwaa ubingwa wa AFCON.

Hili sasa limekwisha, halipo tena, timu imesambaratika. Kuna watakaorudi nyumbani kupambana na maisha yao, wengine huenda watabahatika kupata timu za kuwasajili iwe ndani ama nje ya nchi, hiyo ni wale tu ambao wameonyesha viwango vya juu.

Sasa hivi wadau wa soka wamebaki na tumaini moja pekee kwenye michuano ya kimataifa kwa timu za taifa ‘Taifa Stars’ ambayo inajiandaa kushiriki fainali za AFCON zinazotarajiwa kufanyika Juni nchini Misri.

Fainali hizi ni kubwa mno kwa Afrika. Zinashirikisha timu zenye wachezaji wengi wenye vipaji na wazoefu wa mechi kubwa, wanaocheza soka la kulipwa katika klabu kubwa duniani.

Ni mastaa wakubwa wanaocheza soka la kiwango cha dunia ambako hakuna longolongo kama hapa Bongo ambako soka bado linaendeshwa kiujanjaujanja na kubebana huku sheria na kanuni zikisiginwa.

Huko hakuna mbeleko. Huko Stars itaaminika kwamba imefiha pale kutokana na uwezo wake hivyo wapinzani wataikazia msuli uwanjani katika kila mechi. Hamna mambo ya ganda la ndizi.

Na baada ya Watanzania kusubiri kwa miaka 39 kuiona timu yao ya Taifa kwenye jukwaa hilo kubwa la kimataifa, juhudi binafsi zinatarajiwa kuonyeshwa na watakaokuwamo katika kikosi kitakachoiwakilisha nchi huko.

Mwezi Juni siyo mbali kabla ya kwenda kuwakabili Senegal, Nigeria, Algeria na Kenya ambazo zimepangwa kundi C pamoja na Tanzania.

Stars ilifuzu hatua hiyo baada ya kuifunga Uganda mabao 3-0 katika mechi ya mwisho ya kuwania kufuzu hatua hiyo.

Japo Uganda katika mechi hiyo walikuwa wameshafuzu na walikuwa wakicheza kukamilisha ratiba tu, Tanzania ilishaonyesha kwamba inawamudu The Cranes pale ilipoenda kutoka nao sare ya 0-0 katika mechi yao pili ya hatua ya makundi ya kufuzu Septemba 8, 2018 kwenye Uwanja wa Mandela, mjini Kira, Uganda.

Ni furaha na jambo kubwa kwa Tanzania kushiriki fainali hizo ambazo kwa muda mrefu haijashiriki, lakini sasa Stars inapaswa kuandaliwa zaidi kuliko hatua iliyopita.

Advertisement