MTU WA PWANI : Tukumbushane kitu kuhusu Ngorongoro Heroes

Saturday October 12 2019

 

By Charles Abel

KUNA swali ambalo lazima ungeona likiulizwa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) mara kufuatia Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’, Jumamosi iliyopita, kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wa umri huo huko Uganda, Jumamosi iliyopita.

TFF imeandaa mkakati gani wa kuwatunza na kuwaendeleza vijana hao wa Ngorongoro Heroes mara baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo?

Kama sio swali hilo ambalo limeshazoeleka kuulizwa pindi timu zetu za vijana zinapofanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali, basi wadau wa mpira wangetoa ushauri kwa TFF kuwa lihakikishe linawatunza na kuwasimamia vizuri vijana hao ili baadaye waje kuwa na msaada kwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Swali au ushauri huo umeshakuwa sehemu ya utamaduni wetu kutolewa kila timu ya Tanzania iliyopo katika ngazi ya vijana ama chini ya umri wa miaka 17, chini ya miaka 20 au 23 inapotamba katika mashindano fulani.

Inaonekana wengi wanaamini kuwa ni TFF ndio inapaswa kuwajibika kwa wachezaji wanaochezea timu za taifa za vijana kwa kuhakikisha wanalinda ubora na viwango vyao ili baadaye waje kuwa hazina kwa taifa.

Labda ni kwa bahati mbaya au makusudi lakini sio dhambi kama tukakumbushana nani mwenye wajibu wa kuhakikisha vijana wanaochezea kwenye timu za taifa za umri mdogo iwe mara baada ya kufanya vizuri au hata pale inapofanya vibaya. Kwa kuanzia klabu za soka ndizo zenye jukumu kuu la kuendeleza wachezaji wenye umri mdogo ambao wanachezea timu za taifa kwa vijana kama vile zinavyofanya kwa wachezaji wa timu ya taifa.

Advertisement

Mashirikisho na vyama vya soka duniani kote huwa yanatoa mchango mdogo katika maendeleo ya soka kwa vijana wadogo kwa sababu hiyo ni kazi ambayo imekuwa ikifanywa na klabu za soka.

Mchezaji anakaa kwenye kikosi cha timu ya taifa kwa muda mfupi na muda mwingi anautumia akiwa klabuni ambako ndiko anapaswa kuandaliwa kimwili, kimbinu, kiufundi na kisaikolojia ili aweze kupevuka na kuwa aliyekamilika tayari kwa kuingia kwenye ushindani.

Ni klabu ambayo ndio inafanikiwa zaidi pindi inapoamua kuwaandaa wachezaji vijana waliokamilika na wenye ubora kwani wataitumikia na kuipa mafanikio kwa muda mrefu kulinganisha na timu ya taifa ambako huwa hawakai kwa siku nyingi.

Lakini mbali na kuitumikia pia inaweza kuwauza na kuingiza kitita kikubwa cha fedha ambacho kitasaidia kuendesha shughuli nyingine za klabu/timu kama vile usajili, ulipaji mishahara na posho, malazi, usafiri na pia matibabu kwa wachezaji wengine kikosini.

Ukiondoa klabu, mafanikio na maendeleo ya kila mchezaji kijana yatategemea zaidi jitihada na malengo binafsi ya kufika mbali na kupiga hatua kubwa zaidi kisoka.

Jitihada na ufanisi mkubwa ambao mchezaji husika atakuwa nao ndio itakuwa silaha kubwa kwake ya kuja kuwa nyota muhimu kwa klabu na timu ya taifa siku za usoni.

Turudi kwenye utaratibu sahihi na kuanza kuziwajibisha klabu za soka hapa nchini kwa kushindwa kubeba jukumu la kuwaendeleza wachezaji wenye umri mdogo badala ya kuilaumu TFF ambayo tayari imeshafanya kazi kubwa ya kuviweka sokoni vipaji vya vijana hao.

Mbali na klabu, wachezaji wenyewe husika wanapaswa kuonyeshwa na kuelekezwa njia sahihi za kupita kuweza kulinda na kuendeleza vipaji vyao mara baada ya kung’aa kwenye timu za taifa za vijana badala ya kuwaaminisha kuwa wanapaswa kulelewa na TFF.

Ukweli usemwe kwamba kuitwa kwenye timu ya taifa siku za usoni kwenye ngazi ya umri wa juu zaidi ya ule ambao waliibukia, hakutokani na historia ya kufanya vizuri nyuma, bali kiwango na ufanisi bora wa mchezaji katika wakati husika.

Nchi ina wachezaji wengi wenye vipaji na yeyote anaweza kuchezea timu ya taifa katika muda wowote pasipo kutazama kama alicheza katika timu ya taifa ya vijana au la.

Tunaposhidwa kuwaona wakiitumikia timu ya taifa siku za usoni, klabu zao au wao wenyewe ndio wanapaswa kuulizwa na kunyooshewa vidole kwa kushindwa kulinda kile walichokionyesha pindi walipokuwa kwenye vikosi vya timu za taifa za vijana.

Kuilaumu TFF pindi vijana hao wanaposhindwa kupiga hatua ni kuipa lawama ambazo haistahili kabisa. Inachoweza kufanya TFF ni kutoa muongozo tu kwa klabu juu ya namna bora ya kutunza vijana hao na baada ya hapo, wahusika ndio wanabaki na jukumu la mwisho kutekeleza kwa vitendo hilo.

Vijana hawa wanapaswa kulindwa na kutunzwa na klabu ambazo hata zenyewe zitapata mafanikio makubwa kutoka kwao.

Advertisement