STRAIKA WA MWANASPOTI : Soka la wanawake lazima likuzwe ukanda huu

Tuesday November 19 2019

Soka - wanawake -lazima- likuzwe- ukanda -kimataifa - Brazil- England- Japan

 

By Boniface Ambani

Katika nyanja za soka duniani, tumekuwa tukishuhudia timu za kimataifa za Brazil, England, Japan na kadhalika zikitawala duniani kisoka. Mara kwa mara zimekuwa zikifanya vyema sana.

Kwenye kanda yetu hii ya Afrika Mashariki inaonekana kwa kiasi fulani tumelala kwa upande wa soka la wanawake. Ingawa kwa miaka ya sasa angalau matumaini yameweza kuamka kwa upande wa soka la wanawake.

Njia pekee ambayo inaweza kuokoa soka la wanawake ukanda huu ni kuweka mikakati thabiti ya kulishughulikia mapema.

Michuano ya Cecafa kwa soka la Wanawake inaendelea Tanzania kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na timu mbalimbali za mataifa ya ukanda huu zinashiriki.

Kwa kuzingatia ukuaji wa soka la wanawake, mfano mzuri ni kwa soka lililotandazwa na kikosi cha Harambee Starlets. Iwapo kikosi hiko kitawekwa pamoja na kutunzwa vizuri ni wazi kitakuja kufanya vyema na kuitikisa Afrika na kuzifikia au hata kuzipita timu za taifa za Zambia, Nigeria na Afrika Kusini Banyana Banyana ambazo zimejidhatiti kisoka.

Hii yote itawezekana kama tu juhudi zitafanyika kuitengeneza ligi ya wanawake iwe nzuri.

Advertisement

Ligi ya wanawake ya Tanzania inaonekana kukua hasa kutokana na misingi iliyowekwa na ndio maana hata kikosi cha taifa kinafanya vizuri na kutwaa taji la Cecafa mara mbili mfululizo, wakiliwania kwa mara ya tatu sasa.

Kenya kuna klabu kadhaa za wanawake, Thika, Eldoret Falcons, Vihiga Queens, Makolanders, Oserian, Kisumu na kadhalika.

Hata hivyo, shida kubwa ambazo zinakumba soka la wanadada ni ufadhili, usafiri umekuwa tatizo kubwa mno, huku ligi yenyewe ikikosa wafadhili.

Klabu zinategemea michango kutoka kwa mashabiki na watu binafsi hapa na pale. Shirikisho la soka Kenya limepata ufadhili ambao sio mkubwa sana. Inakuwa ni vigumu kwa klabu hizi kuweza kujimudu kisoka.

Klabu zinakosa vifaa vya kawaida tu kama mipira na kadhalika. Ukumbuke hawa ni wanadada. Wanadada wako na mahitaji ya kiafya mengi zaidi kuliko wanaume.

Kwa hivyo, matumizi yao ni makubwa sana. Kupata ufadhili ama mfadhili wa ligi hiyo inakuwa ni balaa, kisa na maana miundombinu ya ligi haiko vizuri.

Ukosefu wa uwazi pia umeleta balaa katika ligi hiyo. Ukiangalia ligi kuu Kenya ya wanaume, haina mfadhili. Inakuonyesha mambo ni magumu. Ni magumu kivipi.

Kukosa kuwajibika upande wa hela za wafadhili umeleta shida kubwa sana, ndio maana wafadhili wengi wamesepa na tumeshindwa kuvutia wafadhili katika soka letu.

Mashabiki hao pia wengi wameondokea soka letu. Kwa mfano tu, msomaji wa Kenya, jaribu tu wikendi moja utembelee viwanja ambavyo vinaanda ligi za wanawake.

Utafahamu kwa sababu gani inakuwa ni vigumu wafadhili kuwekeza hela zao katika soka. Wafadhili mkumbuke wanaenda na umati. Wanataka kuuza bidhaa zao. Ni wafanyabiashara na lazima hela zao za ufadhili zirudi.

Halafu pia wanataka uwazi wa jinsi hela hizo zilitumika. Wakikupa Sh1000, lazima uwaeleze vile hizo hela zilitumika. Lakini shida kubwaa ni kwamba hizo hela asilimia 70 huwa zinaliwa na viongozi.

Inakuwa balaa tupu. Kwa hivyo mikakati lazima iwekwe vizuri ndio angalau dada zetu waanze kujiskia soka linalipa. Kwa wakati mwingi nawahurumia sana.Klabu nyingi hazilipi.

Kitambo kidogo, nilipata klabu fulani ya kinadada imekwama Eldoret. Hawana chakula, hawana malazi, hawana usafiri wa kurudi Mombasa. Ilibidi nichukue kikosi kizima hadi viongozi wao, niwapeleke kwangu.

Ndio nikaanza kusaka viongozi wa klabu hiyo. Baada ya siku tatu ndio walipatikana. Wakatuma nauli za kinadada hao zaidi ya kumi na sita warejee Mombasa. Balaa tupu. Hebu fikiria vile walikuwa wanateseka. Kwa hivyo jambo hili lazima lifanywe tu ili tukuze soka letu kikamilifu. Hatujui maana ya kutengeneza soka letu.

Siku moja mimi huomba mambo yawe mazuri. Tupate viongozi wenye akili ya mpira. Sio wale walafi. Shirikisho la soka kandaa hili, limeandaa mashindano ya CECAFA ya kinadada Tanzania.

Natumai kuona madaliko makubwa mwakani. Kwa Sasa ni kuombea dada zetu wazidi kuhumudu viwanjani.

Advertisement