TASWIRA YA MLANGABOY : Simba isipobadilika kimbinu wataonewa sana na Yanga

Muktasari:

Simba inahitaji kushinda mechi tano na sare moja ili kutwaa ubingwa, wakati Yanga inahitaji kushinda mechi zake zote huku wakiomba Simba wapoteze mechi tano kati kumi ilizobaki ili kuwa bingwa.

HUKO Yanga kila kitu ni Morrison, Morrison... Ndiyo. Hakuna namna ni mafanikio makubwa kumfunga mtani wako wa jadi akiwa na kikosi bora.

Yanga inayoonekana ya kuunga unga imefanikiwa kukata mzizi wa fitna kwa kuwafunga Simba bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Machi 8, na kufanikiwa kuondoka na pointi nne msimu huu dhidi ya vinara wa Ligi Kuu, Simba ambao unaweza kuwaita mabingwa wateule wanachosubiri sasa ni kuapishwa tu.

Simba inaongoza Ligi kwa pointi 71, wakifuatiwa na Azam (54) Yanga ipo nafasi ya tatu (na pointi 50 kabla ya mechi ya jana) kabla ya msimu kusimama kwa muda wa mwezi mzima kupisha maandalizi ya Taifa Stars kwa mechi ya kuwania ushiriki wa fainali za Afcon dhidi ya Tunisia pamoja na kwenda kushiriki fainali ambazo tumeshafuzu za CHAN2020 nchini Cameroon zitakazoanza Aprili 4.

Ukiweka hesabu za magazijuto unaweza kuona Yanga au Azam wanaweza kuchukua ubingwa huo, lakini kwa uhalisia ni vigumu kwa Simba kushindwa kutetea ubingwa wake msimu huu.

Simba inahitaji kushinda mechi tano na sare moja ili kutwaa ubingwa, wakati Yanga inahitaji kushinda mechi zake zote huku wakiomba Simba wapoteze mechi tano kati kumi ilizobaki ili kuwa bingwa.

Ukiangalia hesabu hizo ndiyo maana kocha wa Luc Eymael tayari amejitoa katika mbio za ubingwa kwa kusema lengo lake ni kumaliza nafasi ya pili pamoja na kuhakikisha anatwaa ubingwa wa Kombe la FA ili kupata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Pamoja na Yanga kukubali kuacha ubingwa furaha yao pekee ni kumfunga Mnyama na kuondoka na pointi nne (ukijumlisha na sare ya raundi ya kwanza), lakini hata Simba wenyewe wamenyong’onyea.

Ukitaka kujua Simba wamekuwa wa pole ndiyo maana hata Mwenyekiti wa Bodi yao Mohamed Dewji ‘Mo’ baada ya mechi ya watani alitumia mitandao ya kijamii kuipongeza Yanga huku akisema anatamani wakutana naye katika Kombe la FA.

Akimini hiyo ndiyo itakuwa nafasi yao Simba kulipa kisasi kwa kuifunga Yanga na kujiondoa katika unyonge huu wa sasa.

Hilo ni kosa kubwa walilofanya Simba kuanzia viongozi wachezaji, wanachama na mashabiki wao kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Yanga.

Kila Mwanasimba alikuwa akiamini kwamba Simba inakwenda kuifunga Yanga kwa sababu Wanajangwani hao hawakustahili sare ile ya 2-2 waliyopata Januari 4, 2020.

Ukiingalia Simba inavyocheza katika mechi zake za Ligi Kuu na uwezo wa ufungaji wa wachezaji wake ni wazi inakupa sababu nyingi za kuamini kwamba inastahili kushinda mechi yoyote ya mbele yake.

Hata mimi kabla ya mechi hii niliamini Simba ingeshinda mchezo wake wa watani wa jadi kwa sababu ina kikosi bora kilichosheheni wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kukaa na mpira na kufunga.

Lakini baada ya mchezo wa Machi 8, 2020 nilipata nafasi ya kutazama mechi hiyo na kurudi ile ya Januari 4 kutaka kujua nini tatizo la Simba ni kipi kinachowashinda kwa Yanga.

Jibu ni moja tu ni uwezo mkubwa wa mbinu za makocha wa Yanga kwa kujua ubora wa Simba upo wapi na wao kujaza viungo wengi wenye kujua kukaba.

Tatizo la Simba ikicheza inakuwa kama mwili wa baunsa juu ni mkubwa chini mwembamba hasa unakosa viungo wakabaji.

Kocha wa Simba, Sven alimtumia Jonas Mkude kama kiungo pekee mkabaji huku akiwa na Clatous Chama, Luis Miquissone, Francis Kahata wakaingia Deo Kanda, Hassan Dilunga hawa wote si wazuri katika kukaba bali kushambulia.

Yanga iliwatumia Feisal Salum ‘Fei Toto’, Papy Tshishimbi walikuwa na kazi ya kusaidia ulinzi wakati Balama Mapinduzi na Haruna Niyonzima na Bernard Morrison walikuwa na kazi moja ya kumsaidia Ditram Nchimbi aliyesimama kama mshambuliaji pekee.

Ukiingalia Yanga muda mwingi walikuwa nyuma ya mpira na kuwaacha Simba watawale mpira huku wao wakishambulia kwa kushtukiza wakitumia udhaifu wa safu ya kiungo wa Simba.

Uchezaji huu wa Yanga ndiyo waliofanya hata katika mchezo wa kwanza wakiwaacha Simba wamiliki mpira lakini wao wanakuwa hatari zaidi wanapofanya mashambulizi yao ya kushtukiza.

Simba ili wapate matokeo dhidi ya Yanga kwa sasa wanalazimika kubadilisha mbinu yao ya uchezaji hasa katika safu ya kiungo mkabaji na ulinzi kwa ujumla, lakini jambo jingine ni lazima wawe na mchezaji mwenye uwezo wa kupiga chenga ili kupenya ukuta wa Yanga.

Hakuna ubishi nidhamu ya ulinzi na heshima ambayo Yanga wanawapa Simba kwa ubora wao imekuwa ni silaha kubwa ya mafanikio yao katika michezo yao ya Ligi Kuu.

Hii ndiyo inaonyesha kwamba benchi la ufundi la Yanga linafanya kazi kubwa kujua udhaifu wa Simba kuliko wenzao wanavyofanya.