Simba, Yanga zinapaswa kumsoma Mwarabu

Muktasari:

Wakati mataifa hayo yakithibitisha kuwa na mafanikio ya soka kupitia idadi ya klabu kutoka katika hatua za robo fainali na nusu fainali hadi fainali yenyewe. Hatua hiyo kwa klabu kutoka Afrika Kaskazini kinaendelea kujenga uimara wa soka la nchi za ukanda huo na kuendelea kutengeneza wasifu kwa klabu hizo.

KUNA usemi wa Kinyamwezi ambao kwa tafsiri ya Kiswahili unasomeka “Wanaume wanaweza kudanganya na wanawake pia wanaweza kudanganya lakini namba haziwezi kudanganya.”

Mantiki ya usemi huo ni kwamba katika masuala mengine ni rahisi kudanganya kutokana na kiwango cha ushawishi atakachokuwa nacho mdanganyaji, lakini katika masuala ya namba ni vigumu kudanganya kwa kuwa moja inahesabika ni moja na mbili inahesabika ni mbili, kama ambavyo tatu itakavyoonekana na kuwa ni tatu tena kwa kila mtu aliyekuwapo na hata atakayekuwepo baadaye.

Tukiuangalia usemi huo kisha tukarejea katika matokeo ya mechi za Afrika nikimaanisha Ligi ya Mabingwa na Shirikisho ambazo zote zinasimamiwa na CAF tunaweza kuwa na kitu cha kujifunza kupitia namba.

Klabu zinavyoonekana kufanya vizuri vimeendelea kuonekana kufanya vizuri, hivyo kuendelea kuthibitisha ubora wake katika soka la Afrika.

Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika msimu huu tumeshuhudia katika timu nane zilizotua ya robo fainali kulikuwa na timu mbili tu kutoka katika mataifa yaliyo nje ya nchi za Afrika Kaskazini yaani Mamelody Sundowns kutoka Afrika ya Kusini na TP Mazembe ya DR Congo huku timu zote sita zilizobakia ambazo ni sawa na asilimia 80 yaani Zamalek, ES Tunis, Raja Casablanca, Al Ahly, Waydad Casablanca, Etoile Du Sahel zikitokea Afrika Kaskazini Misri, Algeria, Tunisia na Morocco.

Lakini baada ya mechi za robo fainali tumeshuhudia pia timu ni kutoka mataifa ya Morocco na Misri za Waydad Casablaca na Raja Casablanca kutoka Morocco na Zamalek na Al Ahly kutoka Misri zikiingia katika hatua ya nusu fainali, hivyo mataifa hayo kuendelea kuthibitisha mafanikio waliyonayo katika soka kupitia Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Wakati mataifa hayo yakithibitisha kuwa na mafanikio ya soka kupitia idadi ya klabu kutoka katika hatua za robo fainali na nusu fainali hadi fainali yenyewe. Hatua hiyo kwa klabu kutoka Afrika Kaskazini kinaendelea kujenga uimara wa soka la nchi za ukanda huo na kuendelea kutengeneza wasifu kwa klabu hizo.

Klabu hizo zimewahi kutwaa ubingwa mara 18 kwani Al Ahly imetwaa kikombe hicho mara nane, Zamalek mara tano, Raja Casablanca mara tatu na Waydad Casablanca mara mbili.

Hali hii ambayo inabeba taswira ya maendeleo ya soka katika Bara la Afrika kwa kulinganisha klabu kutoka ukanda mmoja kuonekana na kuthibitika kuwa na mafanikio kuliko klabu za soka kutoka katika ukanda mwingine inatakiwa kutoa somo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi na mataifa kutoka katika kanda nyingine tukiwemo Tanzania.

Ni fundisho kwa sabau klabu zote hizo zilizoingia katika hatua hiyo zilianza michuano hii tangu mechi za hatua ya kwanza zikiwa na lengo la kutwaa kikombe na sio kufika hatua ya 16 bora au robo fainali, hivyo mafanikio hayo hayajapatikana bila ya maandalizi ya awali.

Hivyo, kwa ushindani unaoendelea kuonekana upo uwezekano mkubwa wa klabu hizo kutoka Afrika Kaskazini zikaendelea kuweka rekodi na kufanya vema katika mashindano hayo kwa miaka mingi ijayo na kutwaa mataji iwapo mataifa mengine kutoka katika kanda mbalimbali za Afrika hayatakuwa na mikakati ya pamoja ya maendeleo.

Hivyo kama ambavyo katika fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya zinakutanisha timu mbili kutoka taifa huku Afrika upo uwezekano timu mbili sio tu kutoka katika taifa moja bali timu pinzani kutoka katika taifa moja zikakutana katika mchezo wa fainali.