NCHIMBI: Zile sita za Simba bado hazijafutika kichwani

Monday April 27 2020
Nchimbi pic

ACHANA na ile hat trick pekee aliyoipata mbele ya Yanga wakati akikipiga Polisi Tanzania, straika Ditram Nchimbi anasema mabao yake yaliyoibeba Taifa Stars kukata tiketi ya michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2020 kabla ya kuahirishwa kwake ndio kila kitu.

Straika huyo anayekipiga Jangwani baada ya kusajiliwa kwenye dirisha dogo, anasimulia kwa nini anakumbuka tukio hilo la kuipeleka Tanzania kwa mara ya pili katika fainali za Chan, lakini amefunguka pia juu ya kipigo cha 6-1 alichowahi kupewa na Simba.

Je wajua kipigo hicho alipewa na Simba akiwa na timu gani? Nini alichokiona ndani ya Yanga kinachotofautiana na klabu nyingine alizowahi kuzichezea? Endelea naye...!

SAFARI YA CHAN

Taifa Stars ilifuzu mara ya kwanza fainali za Chan 2009 zilizofanyika Ivory Coast, kipindi hicho ikiwa chini ya Mbrazili, Marcio Maximo na ilikaa kwa miaka karibu 10 bila kuzinusa tena mpaka bao la Nchimbi kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Sudan waliowachapa 2-1.

Baada ya kipigo cha bao 1-0, asilimia kubwa ya wadau wa soka waliamini safari ya Stars kwenye michuano hiyo ilifikia tamati, lakini mambo yalibadilika kule jijini Khartoum, Sudan, huku Nchimbi akiwa ndio kwanza ameitwa kikosini baada ya kuitesa Yanga alisakamwa kuliko nyota wote.

Advertisement

Wadau walimponda Kocha Etienne Ndayiragije kwa kumuita Nchimbi kwa sababu ya kuifunga Yanga kwenye mechi kubwa na ngumu kama hiyo ya kuwania kufuzu fainali hizo za CHAN, lakini Nchimbi aliwajibu kwa vitendo kwa kuandika rekodi ya kuwa miongoni mwa nyota waliopeleka timu hiyo fainali za pili tangu kuasisiwa kwa michuano hiyo.

Nchimbi anasema kufuzu kwa Stars kucheza CHAN naye akiwa mhusika mkuu wa safari hiyo, ni faraja kwake na heshima kubwa na wachezaji wote walioshiriki kuandika historia hiyo iliyokuja baada ya Tanzania kufuzu na kushiriki pia fainali za Afcon 2019 ikiwa ni mara ya pili.

“Kwangu ni historia ya pekee maana ndio mara ya kwanza nilikuwa nimeitwa Stars, nilibezwa sana, lakini nikamaliza vizuri kinyume na matarajio ya wengi. Hili halitafutika kichwani na ninawashukuru walioniunga mkono,” anasema.

Katika mchezo huo, Nchimbi alihusika na mabao yote, akifanyiwa madhambi na kusababisha Erasto Nyoni afunge bao la kwanza la Tanzania kabla mwenyewe kufunga akimaliza kazi nzuri ya Shaaban Idd Chilunda na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2 na Tanzania kubebwa na bao la ugenini.

MZUKA ULIANZA HAPA

Kwa wanaokumbukwa Nchimbi alipondwa kwenye uteuzi wake ndani ya Stars naye anasema hilo ndilo lililompa mzuka zaidi wa kutaka kuwaonyesha tofauti.

Nchimbi anasema alijua ana kazi ya ziada ya kutomuangusha Ndayiragije na Watanzania walioniamini ndio maana alipuuza kelele za mitandaoni na baadhi ya wachambuzi wa soka na kupambana uwanjani.

“Kama mtu utaamua kufuata mitandao ya kijamii inachokisema, unaweza kupoteza mwelekeo, nami nipo katika mitandao hivyo nilikuwa naona yaliyokuwa yakiendelea. Sikujisikia vibaya wala kunivunja moyo, nafahamu Watanzania tulivyo na niklitaka kuwajibu kwa vitendo na Mungu alikuwa upande wangu.”

Anasema, ni kawaida ya Watanzania hawawezi kuamini mpaka waone mtu kafanya kitu fulani na kwamba, hadi Mtanzania akubali kazi ya mwenzake lazima ufanye kazi ya ziada.

Straika huyo mwenye mabao matano, yakiwamo mawili aliyofunga akiwa Yanga, anasema pia maneno aliyoambiwa na kocha wake kabla ya mchezo yalimpa moyo na kumfanya aingie vitani akiwa na hasira zaidi ya kutoka na mafanikio na kufichua Mungu ndiye kila kwake kwake.

“Walimu walituambia kuwa mechi ni ya historia, hivyo tunatakiwa kupambana ili tuingie kwenye vita vya historia, hilo kila mmoja aliichukua kwa uzito wake, mapambano tuliyofanya ni juhudi za kila mmoja na dua za Watanzania,” anasema.

MALENGO YAKE

Nchimbi anasema matumaini makubwa ni kucheza soka la kulipwa nje kama ambavyo Mbwana Samatta na Simon Msuva wanavyopeperusha vyema bendera ya Tanzania.

“Maisha yangu yana-tegemea soka, namuomba Mungu anifikishe ninapotaka naamini nikijituma uwanjani nitafika ninapotaka. Kubwa ni nidhamu ya mchezo, kumheshimu mkubwa na mdogo vitaniongezea kufanya vizuri katika maisha yangu ya soka,” anasema.

Nchimbi anakiri licha ya kwamba anacheza nafasi ya ushambuliaji, lakini anamzimikia na kuukubali kinoma ufundi wa kiungo na staa wa Manchester United, Paul Pogba.

KIPIGO CHA SIMBA

Nyota huyu anasema, safari ya kisoka ni ndefu akipita timu mbalimbali kabla ya kuona na Yanga ambayo ni moja ya klabu ambazo kila mchezaji huota na kupenda kuzichezea.

Wakati anaibuka ndoto yake nayo ilikuwa kukipiga katika moja ya klabu hizo kubwa, yaani Simba na Yanga na kwa bahati ameangukia Jangwani, akidai hii imetokana na kubaini ukizichezea timu hizo ni rahisi kuonekana na kupata mafanikio makubwa kama unajitambua.

Hata hivyo, anasema hakuna kipigo kilichomganda kichwani mwake kama kile walichopewa na Simba msimu wa 2015-2016 katika Ligi Kuu Bara wakati akikipiga Majimaji.

Katika mchezo huo uliopigwa jijini Dar es Salaam siku ya Oktoba 31, 2015 Nchimbi na Majimaji yake walipigwa mabao 6-1 naye anasema hakisahau kipigo hicho kwa vile ilikuwa mechi yake kubwa ya kwanza dhidi ya vigogo hao.

“Kwa kweli zile sita za Simba mpaka sasa bado zipo kichwani, kwani tulikuwa tuna mwenendo mzuri na hata kama tulikuwa tunapoteza, lakini haikuzidi bao tatu, lakini Simba walitupiga 6-1,” anasema.

VITA YA NAMBA

Nyota huyu anasema, vita ya namba ni jambo la kawaida kwa kila mchezaji awapo ndani ya kikosi, hivyo naye inambidi kuongeza juhudi ili amshawishi kocha kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.

Anasema kikosi kinapokuwa na ushindani wa wachezaji zaidi ya wawili kila mmoja anatakiwa kuwa makini na kuongeza juhudi binafsi ambazo zitamfanya ajihakikishie namba naye anapenda ushindani huo.

“Ili niweze kutimiza malengo yangu ni lazima nipambane na nikutane na watu wa kunipa changamoto ambayo itanifanya nizidi kuwa bora,’’ anasema Nchimbi.

Anasema, hata ikitokea dirisha la usajili wakaongezwa nyota wengine katika eneo analocheza, itakuwa vyema zaidi kutokana na nafasi hiyo kuhitaji nyongeza ya watu ili kuzidi kuwa bora zaidi.

ALIKOTOKEA

Nyota huyo alizaliwa Machi 10, 1993, mjini Songea, Ruvuma alianza kucheza soka tangu akiwa mdogo, lakini alianza kufahamika zaidi akiwa Shule ya Sekondari Mabengo kabla ya kuwa sehemu ya wachezaji wa Chuo cha Ufundi Kiuma na baadaye kupita Jobe Kids ya Tunduru.

Anasema mwaka 2013 alicheza Town Small Boys, Mbinga United zote za Tunduru kisha kuanza kucheza soka la ushindani alipojiunga na Majimaji mwaka 2014 akiipandisha Ligi Kuu na kudumu yao kwa muda kabla ya 2015-2017 kukipiga Mbeya City.

Pia, amewahi kucheza Njombe Mji na kujiunga na Azam FC, waliomtoa kwa mkopo kwenda Mwadui FC ya Shinyanga na ligi ilipoisha akarudi Azam iliyompeleka tena Polisi Tanzania na sasa anakipiga Yanga iliyomsajili kwenye dirisha dogo akibebwa na hat trick aliyowapiga.

Advertisement