MTU WA PWANI : Azam imeshindwa kumtengeneza Allan Okello?

Friday December 20 2019

Azam FC -zam imeshindwa -kumtengeneza-Allan Okello-Klabu ya KCCA- Lugogo-mshambuliaji Allan Okello-

 

By Charles Abel

MABOSI wa Azam FC siku kadhaa zilizopita walitua kibabe jijini Kampala, Uganda na kwenda moja kwa moja katika makao makuu ya Klabu ya KCCA pale maeneo ya Lugogo kuulizia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji Allan Okello.

Inaonekana benchi la ufundi na vigogo wa Azam FC wamefuatilia kwa karibu nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 tu ambaye amekuwa tishio kwa sasa katika Ligi Kuu ya Uganda na hata katika mashindano ya Chalenji ambayo yamehitimishwa jana Alhamisi.

Inatajwa kuwa Azam FC ilikwenda na ofa ya Dola 100,000 (Shilingi 230 milioni) ikiamini kuwa dau hilo lingetosha kuishawishi klabu hiyo ya Uganda kuwauzia nyota huyo ambaye aliibukia katika kikosi cha vijana cha timu hiyo inayomilikiwa na Jiji la Kampala.

KCCA inatajwa kuhitaji kitita cha kuanzia Dola 400,000 (Sh 920 milioni) ili imuachie Okello, kiasi ambacho kimeifanya Azam FC kurudi nyuma na kuachana na mipango ya kumsajili mshambuliaji huyo.

Hapana shaka kwamba Okello ni miongoni mwa wachezaji bora na wenye kiwango kizuri Afrika Mashariki na Kati kwa nyakati za hivi karibuni na ni wazi kwamba hakuna klabu ambayo isingependa kuwa na kijana huyo katika kikosi chake.

Ana uwezo mkubwa wa kuichezesha timu, kupiga pasi za mwisho na krosi, kufunga mabao, chenga za maudhi, kasi na ana utulivu na akili ya hali ya juu katika kusoma mchezo kwa haraka na pia ni mchezaji anayeweza kuwafungua mabeki kutokana na namna alivyo na ubunifu pindi anapokuwa na mpira.

Advertisement

Sio dhambi kwa Azam FC kuonyesha nia ya kumsaka Okello lakini kitendo cha kuwa tayari kutoa kiasi kinachokaribia Sh 230 milioni kwa ajili ya mshambuliaji huyo kinashtua kidogo kutokana na kwamba kinaweza kuibua maswali ambayo ni Azam wenyewe ndio wanaoweza kuyajibu.

Miongoni mwa maswali ambayo tunaweza kuiuliza Azam FC ni kwamba Tanzania nzima wamekosekana wachezaji wanaocheza kwa staili ile ya Okello hadi wakaamua kuvuka mipaka na kukubali kutoa zaidi ya Sh 230 milioni ili kuishawishi KCCA iwauzie mchezaji wao?

Bila shaka, jibu la swali hili ni hapana kwa sababu ndani tu ya kikosi cha Azam wapo wachezaji ambao ukiangalia namna yao ya uchezaji haitofautiani sana na ile ya Okello.

Wapo wachezaji wengi wa mfano wake kama vile kina Iddi Kipagwile na kinda wa kikosi chao cha vijana, Tepsi Evance.

Hawa ni wachezaji ambao wanaweza kucheza pembeni na kuingia ndani kama vile Okello amekuwa akifanya.

Naamini wachezaji hao ambao wako ndani ya Azam FC kama wakiongezewa vitu vichache tu vya kiufundi, maana yake wanaweza kutimiza mahitaji ya kiufundi kama yale ambayo yangefanywa na nyota huyo wa Uganda.

Azam ingeweza kuokoa pesa kibao kwa kuwatengeneza wachezaji hao ambao wanaweza pia kuwa na msaada mkubwa kwa taifa kuliko kwenda kumchukua Okello kwa pesa zote hizo.

Lakini pia kitendo cha Azam kuwa tayari kuvunja benki na pia kuvunja rekodi yake ya usajili kwa kutoa kitita kikubwa kwa ajili ya kumnasa Okello kinaweza kuibua hisia kwamba kikosi cha vijana na ‘akademi’ ya Azam imeshindwa kuzalisha nyota bora wenye umri mdogo ambao wanaweza kutoa mchango na kuisaidia timu hiyo kama ambavyo nyota huyo wa KCCA anafanya kwa klabu yake.

Ukiangalia na kufanya tathmini ya thamani ya timu hizo mbili, utabaini kuwa Azam FC imeizidi KCCA kwa uwekezaji na thamani, kuamua kumwaga fedha kumsajili nyota wa timu nyingine ambaye ana umri mdogo kuliko baadhi ya wachezaji ulionao maana yake, inatoa ishara kuwa ‘akademi’ au timu ya vijana imeshindwa kuwa na faida na badala yake inazalisha wachezaji ambao hawana ubora.

Okello ni matunda ya uwekezaji na usimamizi mzuri wa KCCA katika soka la vijana ambao umekuwa ni mpango wa muda mrefu wa klabu hiyo ikiamini kwamba ni njia sahihi ya kuweza kupata wachezaji bora ambao wataipa mafanikio timu hiyo lakini pia kuwa chanzo cha mapato kupitia mauzo yao kwenda klabu nyingine.

Kama Azam ingekuwa na mpango mkakati thabiti wa kuweka nguvu katika soka la vijana, leo hii isingekuwa inahangaika kutumia zaidi ya Sh 230 milioni kumsajili mchezaji ambaye hajafikisha hata umri wa miaka 20.

Wakati Azam FC inapanda Ligi Kuu mwaka 2008, ndio kwanza Allan Okello alikuwa anafikisha umri wa miaka minane na ndio kwanza alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Kipindi hicho cha miaka 11 tangu walivyopanda Ligi Kuu hadi sasa wangekitumia vizuri, leo hii wasingekuwa wanaenyeshwa na KCCA katika kumsaka Okello.

Wangeamua kwa dhati na wakawa na mipango imara, leo hii wangekuwa na idadi kubwa ya kina Okello ndani ya kikosi chake.

Advertisement