MKEKA WAKO : Jose Mourinho atawaongezea maumivu Chelsea

Friday December 20 2019

JOSE Mourinho -Tottenham Hotspur - Ligi Kuu England -Chelsea-

 

By Samson Mfalila

JOSE Mourinho anaikaribisha timu yake ya zamani ya Chelsea wakati atakapoiongoza Tottenham Hotspur kwenye mechi ngumu ya Ligi Kuu England kati ya timu hizo mbili itakayochezwa keshokutwa Jumapili.

Mreno huyo atakuwa atavaana na mashabiki wa Chelsea, ambao katika siku za karibuni ni kama amevunja nao urafiki baada ya kuondolewa kuinoa timu hiyo ya Stamford Bridge.

Kocha wa Chelsea, Frank Lampard naye atakuwa anavaana na Mourinho, ambaye aliwahi kucheza chini yake.

Chelsea itakwenda katika mchezo huu dhidi ya wapinzani wao wa jijini London wakati ikiwa katika kiwango cha chini.

Tofauti na Spurs, ambayo kwa sasa ipo moto kwenye ligi na ikishinda mchezo huu ina maana itawapita Chelsea

Tangu Mourinho ameanza kuinoa Spurs amesaidia timu hiyo kushinda mechi nne kati ya tano za Ligi Kuu England hivi karibuni.

Advertisement

Ina maana Tottenham imeshinda mechi nyingi zaidi chini ya Mourinho tofauti na ilipokuwa chini ya Mauricio Pochettino, ambaye chini yake Spurs ilikuwa imecheza mechi 12 za ligi.

Spurs ipo vizuri kwa sasa kwani angalau ina wastani wa kufunga bao moja katika mechi kila kwa sasa.

Ushindi wake wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves kwenye Uwanja wa Molineux, wiki iliyopita unadhihirisha kwa sasa timu hiyo ipo vizuri.

Chelsea kwa upande wake baada ya kuanza vizuri, katika siku za karibuni imeonekana kupotea.

Kuna wakati Chelsea ilikuwa inatishia amani kwenye ligi baada ya kushinda mechi sita mfululizo.

Hata hivyo, katika siku za karibuni imepotea kwani imejikuta mara kadhaa ikipoteza mechi hata kwa timu vibonde.

Chelsea imejikuta ikichezea vichapo kwa timu kama za West Ham na pia hivi karibuni ililala mabao 3-1 kwa Everton.

Pia, ilipigwa nyumbani bao 1-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge na Bournemouth.

Chelsea katika siku za karibuni imepungua uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga licha ya kucheza vizuri soka ya pasi.

Imekuwa inapata tabu sana likija suala zima la kusaka mabao dhidi ya timu pinzani.

Tottenham ya Mourinho nayo ina tatizo kwani kiungo wake Tanguy Ndombele ni majeruhi akikabiliwa na tatizo la nyonga.

Anatazamiwa kuwa nje kwa muda ingawa ana uwezekano wa kucheza mechi hii ya keshokutwa.

Pia, Tottenham inatazamiwa kuwa bila ya Ben Davies, Michel Vorm na Erik Lamela, ambao pia wote ni majeruhi.

Kiungo mkabaji Harry Winks amepona, ambapo sasa kuna uwezekano akarudishwa katika kikosi cha kwanza.

Mashabiki wa Tottenham sasa watakuwa wanasubiri jinsi ambavyo Mourinho atapanga safu yake ya kiungo.

Kocha Lampard kwa upande wakati naye ana majeruhi Ruben Loftus-Cheek na Fikayo Tomori.

Pia, kuna uwezekano mdogo kwa straika wa Chelsea, Oliver Giroud kucheza kutokana na kukabiliwa na maumivu ya enka.

Kiungo mwingine, Ross Barkley naye katika siku za karibuni amejikuta akipoteza namba katika kikosi cha kwanza cha Chelsea.

Hata hivyo, Christian Pulisic, Willian na Jorginho, ambao walitolewa mapema kwenye mechi na Bournemouth wapo vizuri kwa mujibu wa Kocha Frank Lampard.

Timu zinatazamiwa kuwa hivi:

Tottenham: Gazzaniga, Aurier, Sanchez, Alderweireld, Vertonghen, Sissoko, Winks, Lucas Moura, Dele Alli, Son, Kane

Chelsea: Kepa; Azpilicueta, Rudiger, Zouma, Alonso; Kante, Jorginho, Kovacic; Willian, Pulisic, Abraham

Advertisement