JAMVI LA KISPOTI : Karibu Kasongo, maradhi ya soka letu unayajua

Muktasari:

Mpira wetu bado uko nyuma hasa wakati huu tukiwa na bodi inayosimamia kutoka katika mikono ya TFF. Hatuna kasi nzuri inayotokana na mipango thabiti yenye misingi ya mpira.

Pale Bodi ya Ligi Tanzania kuna mgeni ameingia hana hata mwezi tangu atambulishwe akija kuchukua nafasi ya mtu.

Aliyeingia pale ni Almasi Kasogo akiwa sasa ni mtendaji mkuu mpya wa Bodi ya Ligi akichukua nafasi ya Boniface Wambura aliyerudi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kasongo anaweza kuwa mgeni katika bodi ya ligi hasa katika jukumu alilopewa lakini sio mtu mpya katika mpira wa nchi.

Kasogo amefanya kazi pale Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kwa takribani miaka isiyopungua saba.

Kudumu kwake kwa muda huo DRFA kunampa nafasi nzuri ya kujua kipi kinahitajika kufanyika katika Bodi ya Ligi ambayo kwa sasa amekwishaanza kuihudumia.

Mpira wetu bado uko nyuma hasa wakati huu tukiwa na bodi inayosimamia kutoka katika mikono ya TFF. Hatuna kasi nzuri inayotokana na mipango thabiti yenye misingi ya mpira.

Kuna wakati tunaona kama mung utu ameamua kutubariki kwa kupata mafanikio, lakini uhalisia ni kwamba bado hatuna njia sahihi ambazo zinahitajika kuwa kama kipimo cha kuangalia hatua ya maendeleo.

Sasa mpira upo kwa Kasongo katika wakati ambao bado bodi yetu haina nguvu ya kuweza kujisimamia yenyewe na kuacha muingiliano ambao upo sasa.

Waliomtangulia Kasongo walishindwa kulifanya hilo nadhani hata mwenyekiti wa bodi naye ameonyesha bado yuko katika usingizi mzito wa kulisimamia hilo.

Hakuna ambacho kitaweza kufanikiwa kama Bodi ya Ligi iwapo itaendelea kufanya kazi zake kwa kusimamiwa na mamlaka zingine na watu wengine.

Bodo lazima iache kuishi maishas ya kuendeshwa kwa maelekezo ya kutoa taasisi nyingine hili sasa limetua kwa Kasongo.

Nasikia ukitaka uondoke haraka kwenye mpira basi simamia hiyo hoja ni Imani yangu Kasongo amejiandaa na vita hiyo.

Kasongo inawezekana kwamba wapo ambao walisimamia ujio wake katika bodi hiyo hasa kushika nafasi hiyo, lakini anatakiwa kutambua kwamba sasa anakwenda kusimamia maendeleo ya mpira na sio waliomshika mkono.

Katika nyakati ambazo malalamiko ya uendeshaji wa ligi yamekuwa mengi sitegemei kumuona Kasongo akiwa na wakati rahisi katika kunyoosha mambo, maradhi ambayo mpira wetu unaugua yanatibika kwa kuacha urafiki pembeni wala kujuana.

Kama akifanya kosa la kumuangalia mtu usoni katika kuamua mambo yake ya kikazi jahazi hili kwake litazama kirahisi anachotakiwa ni kunyooka bila kumpendelea mtu au kumuonea mtu jambo ambalo linawezekana.

Tunategemea makubwa hasa katika mabadiliko chanya ya bodi na mpira kwa ujumla kutoka kwake na sio kuendelea kusikia malalamiko ya matatizo ambayo yanatatulika kirahisi.

Ukifuatilia mechi za Ligi Daraja la Kwanza utagundua ligi hiyo ni kama imesahaulika hakuna msukumo wa kuifanya iwe ligi muhimu tena kama zamani huko kuna matatizo mengi ya usimamizi na dhuluma za kutosha hasa timu zinapotaka kupanda ligi.

Bahati mbaya zaidi ni kwamba haya yatachukua hatamu zaidi mwaka huu wakati ambao nchi itaingia katika uchaguzi mkuu kama Bodi ya Ligi itaendelea kusinzia tunaweza kujikuta tunapandisha timu kwa malengo ya kisiasa na ushawishi tofauti na ushindani wa uwanjani.

Kasongo mfupa huu ni wake akishirikiana na mzee wangu Stephen Mnguto ambaye atakuwa juu yake.

Ukija katika Ligi Kuu nako mambo ni yaleyale ingawa huko kidogo kuna unafuu kutokana na jicho lake liko wazi kwa mechi zake kuonyeshwa moja kwa moja runingani.

Changamoto za usimamizi zipo nyingi ambazo huku sitaki kumkumbusha, kwani amekuwa mhudhuriaji mzuri wa mechi mbalimbali za ndani ya mkoa na hata nje ya mkoa.

Alichotakiwa ni kuyafanyia kazi mapema hata kabla ya kuingia kazini, kwani changamoto zote hizi zilikuwa zinajulikana muda mrefu hakuna jipya.

Hatutarajii kuona changamoto hizi zikitanuka na kuwa kubwa katika utawala wake kama mtendaji mkuu, Kasongo atawapa faraja wadau wa soka endapo changamoto hizi walau zitakuwa zikipungua wakati ukisogea taratibu. Tumtakie kila la heri katika majukumu yake, karibu Kasongo.