JAMVI LA KISPOTI : Hatma ya Yanga ipo kwa wanachama wao

Thursday April 25 2019

 

By Khatimu Naheka

YANGA haina pesa kwasasa. Yanga inateswa na anguko la matajiri waliokuwa wanasimama nyuma yake kiuchumi. Ni maisha f’lani ambayo tulikuwa tumeyajenga kutegemea fedha za watu.

Kukosekana kwa fedha kumeiangusha timu hiyo katika kila eneo na kuiondoa katika ubora ulioifanya kutamba awali, nguvu yao sasa ni ya kawaida tofauti na huko nyuma.

Tangu kuondoka kwa bilionea Yusuf Manji na fedha zake, hakuna ambaye ameweza kuvaa viatu vyake. Unaweza kujisemea kwamba ni bora angeondoka Manji lakini fedha zake zikabaki. Lakini changamoto ni kwamba Yanga imeshuhudia vyote viwili vikiyeyuka kwa wakati mmoja.

Bahati mbaya zaidi ni kwamba ukiacha watu wachache ambao tunawaita vigogo ambao wanajitoa sasa kwa klabu hiyo hakuna ambaye angekuja kuziba nafasi ya Manji kirahisi.

Ndani ya anguko hilo akatokea mtu mmoja anaitwa Mwinyi Zahera bila kujulikana alipotokea. Anakuja na akili ya kuirudishia ufalme Yanga akitumia akili ndogo tu ya kuamka asubuhi na kupata akili ya kusafishwa kinywa.

Zahera anaangalia maisha ya Yanga yalivyo mabovu kisha akashangazwa na idadi ya watu ambao wanajiita wanaipenda klabu hiyo ambao anaamini wangeweza kirahisi sana kuunganisha nguvu na kuifanya iwe kubwa zaidi ya hivi ilivyo. Kisha anapiga akili ya haraka ya kurudisha makali.

Advertisement

Zahera anaona kila anapopita anakutana na mashabiki wa Yanga na wengine ni wanachama, lakini klabu hiyo inalia njaa hali ya kuwa ina rasilimali watu ya kutosha na ya kipekee.

Kinachomtatiza Zahera ni kwamba anachokutana nacho Yanga hajawahi kukiona sehemu kubwa aliyopita. Amezoea kuiona TP Mazembe yenye nguvu Lubumbashi pekee nje ya hapo ina watu kumi, amezoea kuiona AS Vita Club yenye nguvu kubwa jijini Kinshasa lakini nje ya hapo ina watu wachache.

Wakati Zahera akipambana na hilo, Yanga sasa iko katika uchaguzi wa kupata viongozi wapya ambao kama mambo yataenda kama yalivyopangwa Mei 5 uongozi utakaupokea utawala wa Manji utaingia madarakani.

Uongozi huo unatafutwa sasa hali ya kuwa timu hiyo ina hali mbaya kifedha kwa wachezaji kutolipwa malipo yao mbalimbali.

Nafasi pekee ambayo Wanayanga wanaweza kuipata sasa juu ya viongozi wanaowahitaji ni kuangalia ni watu gani wanaweza kuwa na ramani nzuri ya kumaliza changamoto zao kwasasa wakati huu ambao timu yao inateseka.

Hakuna ambaye anaoa mwanamke kisha akishaingia naye ndani ya ndoa ndiyo aje alipe mahari ya binti au mwanamke husika. Nguvu ya viongozi ambao wanahitajika sasa ilipaswa kuonekana sasa.Wasiwasi wangu naiona Yanga kama inaweza kuja kuchagua aina ya viongozi ambao baada ya muda wanaweza kutaka kuwang’oa madarakani kama wasipokuwa makini katika kutafuta watu sahihi.

Yanga ya sasa inahitaji mtu ambaye ataziba pengo la viongozi walioondoka na siyo kuhamisha matatizo. Viongozi wa namna hii sioni kama watadumu katika nyumba wanayotaka kupanga.

Inawezekana pia wakapatikana viongozi ambao watakuwa na akili mpya ya kutafuta njia ya kuiondoa klabu hiyo katika mfumo mbovu wa uendeshaji na kuileta katika mfumo wa kisasa ambao klabu hiyo inatakiwa kuingia sasa.

Bado msisitizo wa kupatikana kwa viongozi wa namna hiyo inahitaji akili iliyotulia kutoka kwa watakaobahatika kupiga kura na kuhakikisha wanapata viongozi wenye mtazamo chanya.

Hilo likiendelea pia hata hao wanachama na mashabiki pia hawatakiwi kusahahu kwamba kama kweli wanaumizwa na hali ya maisha ya Yanga ya sasa basi wanatakiwa kuendelea kuichangia klabu yao katika mfumo wa uchangiaji ambao Zahera anaufanya sasa ndani ya klabu hiyo.

Kuendelea kuumizwa na matokeo na timu yako wakat i huna unachochangia, ni udhaifu mkubwa ambao wale ambao hawajafanya lolote kuichangia klabu hiyo hawapaswi kuendelea kupiga kelele kuwa unaipenda klabu husika huku sasa unashindwa kuikomboa.

Advertisement