Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya Mayanga na Mahrez isingewezekana

Muktasari:

  • Ile mechi ya Algeria ilikuwa ya Goliath dhidi ya Daudi. Hakuna ambacho tungeweza kufanya zaidi. Sio kocha, wala wachezaji. Kuna mazungumzo ya uchambuzi wa mtaani hapa na pale yanatawala lakini kuna mambo ya msingi nyuma yake.

UNATAZAMA mechi na unapiga makofi unafungwa. Kwa chochote kilichoitokea Taifa Stars dhidi ya Algeria unapaswa kutabasamu na kuukubali ukweli. Tusubiri kuona itakavyocheza dhidi ya DR Congo kesho.

Ile mechi ya Algeria ilikuwa ya Goliath dhidi ya Daudi. Hakuna ambacho tungeweza kufanya zaidi. Sio kocha, wala wachezaji. Kuna mazungumzo ya uchambuzi wa mtaani hapa na pale yanatawala lakini kuna mambo ya msingi nyuma yake.

Sielewi vizuri kwa Lugha ya Kiswahili tunawezaje kutumia neno intensity. Labda kwa haraka haraka tunaweza kutumia neno hili katika soka kwa maana ya kucheza kwa nguvu, kasi, maarifa na haraka. Hiki ndicho ambacho Waalgeria walitufanyia.

Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga alikuwa na makosa yake lakini bado asingemudu kukabiliana na hicho kitu kutoka kwa Algeria. Ndio, kwa nini Mayanga alimwacha uwanjani dakika zote Himid Mao ambaye hakuwa fiti kwa ajili ya pambano lile?

Katika wachezaji wote wa Taifa Stars, kama kuna mchezaji unayeweza kwenda naye vitani akiwa fiti basi ni Himid. Mwingine anaweza kuwa Thomas Ulimwengu. Sijui Mayanga alikuwa anawaza nini kwa Himid lakini ukweli, asingeweza kupambana Intensity ya Algeria.

Kuna mambo mawili matatu ya kufikiria. Kwanza kabisa Algeria ina wachezaji kamili. Sisi tuna wachezaji nusu nusu. Tuna wachezaji wengi ambao wanacheza ligi ya ndani. Algeria ina wachezaji wengi wanaocheza Ulaya na wengine wengi wamezaliwa Ulaya.

Kama ukiichukua Timu ya Taifa ya Tanzania ikacheza na klabu kama USM ya Algeria bado tunaweza kupata matokeo haya haya ambayo tumepata dhidi ya timu yao ya taifa. Jaribu kufikiri inakuwaje pindi tunapocheza na kina Mahrez. Kumbuka Algeria inaweza kutumia wachezaji wanaocheza ndani tu na tukabaki katika hali mbaya.

Wachezaji wa Taifa wa Algeria wanaocheza ndani na ugenini wameandaliwa kuwa wanasoka kamili. Jaribu kuyatazama maamuzi ya wachezaji wao na uwezo wao binafsi. Jaribu kuangalia mabao waliyotufunga achilia mbali lile la kujifunga la Shomari Kapombe.

Wachezaji wetu hawajaandaliwa kucheza katika viwango vile. Mpaka sasa hawaandaliwi kucheza katika kiwango kile. Tunajua maisha ya klabu zetu yalivyo. Shughuli ya Waalgeria ilianzia utotoni na katika malezi ya kiwango cha juu. Wengine waliandaliwa Ufaransa, wengine waliandaliwa Algeria.

Ungetazama mechi kwa makini, walau Mbwana Samatta na Simon Msuva walipoupata mpira walijaribu kuupaka rangi kwa kujiamini kwa sababu huyu mmoja anacheza Ulaya na mwingine anacheza na Waarabu wa upande uleule wa Afrika Kaskazini.

Pia, ndani ya majaribu haya tunayopitia bado timu yetu inafundishwa na kocha mzawa ambaye hana uzoefu. Kocha Mayanga ana jitihada na amebebeshwa gunia la misumari. Anajitahidi kadiri ya uwezo wake kufundisha na kuwatia moyo vijana lakini inashindikana.

Kocha wetu hajawahi kusimamia timu yoyote kubwa nchini ambayo imeshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho au ile ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika. Kitu kizuri ni kwamba anaendelea kupata uzoefu ndani ya mechi hizi kiasi akirudi katika soka la klabu anaweza kuwa bora kuliko alivyokuwa awali. Tatizo, Taifa Stars sio sehemu ya majaribio. Kwake ni kitu safi na sahihi, lakini kwa Taifa sio jambo la afya njema.

Tumeshuhudia makocha wa Kizungu wenye uzoefu ambao wanaisimamia Taifa Stars katika mechi kama hizi na bado hali inakuwa ngumu. Vipi kwa Kocha Mayanga? Hapo hapo kumbuka kocha amepewa mzigo huu akiwa na wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu nyumbani. Kama tungeweza kuwa na wachezaji kutoka Ufaransa, Ubelgiji, England, Italia, Ujerumani na kwingineko kama Algeria, basi wangeweza kumsaidia kocha wetu.

Kwa sasa kombinesheni hii ya kocha wetu na wachezaji waliopo ni ngumu kushinda vita dhidi ya Mahrez.

TFF ifanye haraka ya kuchagua kocha wa kigeni mwenye uzoefu kabla hatujaenda katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2019. Tusizidanganye nafsi zetu. Kama tuna uwezo wa kifedha basi kocha huyo aje na msaidizi wake, kama hatuna uwezo huo, basi Kocha Mayanga awe msaidizi kwa sababu tayari Taifa limewekeza kwake kwa kumpatia uzoefu kama huu.

Wala kocha mzungu mzoefu anaweza kutupa mbinu za kukabiliana walau na Algeria kijanjajanja kama ambavyo zamani kina Marcio Maximo na Kim Poulsen walikuwa wanafanya. Kwa Kocha Mayanga nadhani tumembebesha mzigo ambao sio wake kwa sasa.

Nimejaribu pia kutazama kikosi cha DR Congo ambacho kinakuja kucheza na Taifa Stars ukweli pia unabakia pale pale, bado ni ndoto kwetu kuwa katika kiwango sawa na wao. Tunaweza kushinda, sawa, lakini hayawezi kuwa matokeo ya kujivunia na kutufanya tuamini tunaweza kufika mbali katika michuano mbalimbali.

Bado utakuwa mwendo wa kubahatisha.