TFF ijichunge, sakata la Michael Wambura lisije likawavuruga

Muktasari:
- Kamati ya Utendaji imemteua Athuman Nyamlani, mmoja ya watu wa karibu wa Rais Wallace Karia kushika cheo hicho.
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefanya uteuzi wa Kaimu Makamu wa Rais, ikiwa ni wiki chache tangu wamfungie maisha Makamu wa Rais wake, Michael Wambura kwa tuhuma za kughushi na kujipatia fedha kinyume na taratibu.
Kamati ya Utendaji imemteua Athuman Nyamlani, mmoja ya watu wa karibu wa Rais Wallace Karia kushika cheo hicho.
Nyamlani sio mgeni ndani ya TFF kwani alishawahi kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa TFF enzi za utawala wa Leodgar Tenga, hivyo ni mzoefu wa masuala ya uongozi ndani ya shirikisho hilo.
Hata hivyo, uteuzi wake umekuja siku chache tangu Wambura akate rufaa yake kupinga adhabu aliyopewa na katika mkutano wake wa wanahabari mara baada ya kuadhibiwa alilitaja jina la Nyamlani na Kaimu Katibu Mkuu Wilfred Kidao.
Mwanaspoti hatuna tatizo lolote la uteuzi wa Nyamlani, ni mwanamichezo mzoefu na mwenye kulijua soka la Tanzania, maadamu tu ameteuliwa kwa kuzingatia taraibu na Katiba ya TFF, pia hatuwezi kuyaamini moja kwa moja madai ya Wambura katika utetezi wake kwa kuwaainisha wawili hao.
Tunajua Nyamlani analijua soka la Tanzania tangu alipokuwa kiongozi wa Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (TEFA) kabla ya kupanda ngazi Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na hatimaye kutua TFF, hivyo huenda akafiti katika nafasi aliyopewa.
Hata hivyo, tatizo ni namna uteuzi huo ulivyokuja ghafla na tayari kukiwa na tuhuma za Wambura kuwa tatizo la kuadhibiwa kwake ni suala zima la cheo anachokishikilia yaani Umakamu wa Rais, pia ukaribu wa Karia na Nyamlani ndio tatizo linapoanzia.
Wadau wa soka wanapooanisha mambo hayo kwa pamoja wanaweza kupata jibu kulikuwa na mpango nyuma ya pazia hata kabla ya kufungiwa kwa Wambura kwani alishamtaja mhusika na sakata zima la ajira ya Kidao ndani ya TFF.
Pia inaelezwa eti uteuzi huo ulifanywa kwa usiri mkubwa kiasi baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaotajwa wanaomuunga mkono Wambura na kusaidia kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 12, 2017 kushtukizwa.
Pia uteuzi huo umekuja kipindi ambacho Baraza la Michezo la Taifa (BMT) likiliandikia barua TFF kutaka kupata ufafanuzi juu ya adhabu ya Wambura na ajira ya Kidao ndani ya TFF.
Hofu yetu ni kwamba suala hili la agizo la BMT na suala zima la kifungo cha Wambura lisije likasababisha kuibua mgogoro ambao utakuja kuiingiza TFF matatani mbele ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).
Fifa iliamua kuelekeza vyama wanachama wake kutengeneza katiba ambayo haitaweza kuingiliwa na serikali katika maamuzi yake ya kisheria ikiwamo kuundwa kwa kamati za kisheria, kama serikali ikiamua kukomalia sakata hili kuna mambo yanayoweza kulivuruga soka la Tanzania.
Mwanaspoti linadhani imefika wakati sakata hili lililoibuka wakati Watanzania wakiwa na kiu ya kuona maendeleo ya soka la Tanzania na klabu zake katika anga za kimataifa lichukuliwe kwa tahadhari ili lisiathiri soka letu.
Tusingependa kuona yale yaliyowahi kutokea miaka ya nyuma enzi za uongozi wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) lililosababisha Tanzania kukaribia kufungiwa na Fifa yakirejea tena katika zama hizi za sasa.
Tunachokitaka ni kuona sakata hili la Wambura, agizo la BMT na kinachoendelea ndani ya TFF kinamalizwa kiungwana bila kuoneana au kukandamizana kwa maendeleo ya soka letu.
Mambo ya migogoro na ujanja ujanja wa kubebana ndani ya asasi hiyo, imepitwa na wakati ndio maana ilikuwa vigumu chini ya utawala wa Tenga kushuhudia mambo kama hayo kwa vile utawala huo ulisimamia misingi ya katiba na taratibu zilizopo.
Tunaamini viongozi na wajumbe wa TFF ni watu wenye weledi na wanaofahamu kiu ya Watanzania ipo wapi katika soka kwa jumla, hivyo wajikite katika kuwapa raha wanayoitarajia kutoka kwao.
Hata kama kuna suala ambalo wanaliona halipo sawa wasimamie kwenye katiba yao na kutumia mikutano waliyonayo kufanya mambo ili kila kitu kiwe sawa na pale kuna haja ya hatua za kisheria kuchukuliwa wazichukue bila kumwonea mtu.
Bahati nzuri Nyamlani ni Mwanasheria mzuri, hivyo kwa nafasi aliyopewa ndani ya TFF, japo tayari alishakuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji itampa nafasi nzuri ya kusimamia, kushauri na kusaidia mambo ya kisheria kwa manufaa ya soka letu.