NINACHOKIAMINI: Hii kali, TFF kila mtu anakaimu au anajitolea, tumekwisha
Muktasari:
Uchaguzi unapoisha huwa hakuna nafasi ya kufanya maendeleo, kwani fitina na majungu ya uchaguzi wa miaka mitano ijayo huwa unaanza.
KATIKA kitu ambacho sijawahi kukielewa nchini kwetu ni kuona jinsi viongozi wanavyotafutana wao kwa wao kwa lengo ya kubomoana.
Uchaguzi unapoisha huwa hakuna nafasi ya kufanya maendeleo, kwani fitina na majungu ya uchaguzi wa miaka mitano ijayo huwa unaanza.
Katika karne ya 21, bado tunashindwa kujiongoza, tunapopewa nafasi tunashindwa kuitumia fursa hiyo, badala yake tunataka kugombana asubuhi mpaka jioni.
Unashangaa zaidi unapokutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), unaona kila mmoja ameshika njia yake.
Wakienda ofisini pale Uwanja wa Karume, kila mmoja yupo na njia yake, hakuna kusalimiana, kila mmoja yupo na malengo yake.
Uongozi huu wa TFF hauna hata mwaka moja, lakini mambo hayaendi, kila kitu kimekwama, hakuna mbele, hakuna mwelekeo, kuna giza nene, hakuna anayejua tunakokwenda. Tumekwisha.
Katika mazingira hayo, unadhani Taifa Stars haiwezi kufungwa mabao 4-1 na Algeria? Ilikuwa lazima ifungwe, kwa sababu viongozi hawana malengo na timu hiyo, hakuna anayefurahia maendeleo ya timu hiyo.
Wanachofurahia pale TFF ni nani amemkomoa nani. Rais anafurahia Makamu wake akifungiwa kifungo cha maisha kujihusisha na soka, Katibu naye anafurahia Ofisa Habari akiondolewa, Kamati ya Utendaji inachoangalia ni posho, hakuna anayejali soka linakwendaje. Hawajadili soka tena, ni posho tu.
Yote hayo yamesababisha kuwepo kwa viongozi wote wanaokaimu au wanaojitolea jambo ambalo halijawahi kutokea ndani ya TFF zaidi ya miaka thelathini iliyopita.
Kwa utaratibu wa TFF, Rais huwa halipwi mshahara, kwa lugha nyepesi ni kwamba anafanya kazi kwa kujitolea tu. Kwa hiyo anajitolea.
Tumeona hivi karibuni Makamu wa Rais, Michael Wambura amefungiwa maisha kutojihusisha na soka.
Na harakaharaka, Kamati ya Utendaji iliyokuwa inawahi posho ikakutana na kumteua Athuman Nyamlani kukaimu nafasi hiyo. Naye huyu huwa halipwi mshahara.
Kwa maana nyingine, ni kuwa hata nafasi ya Makamu wa Rais haina mwenyewe, aliyepo anakaimu tu na pia anajitolea kwa sababu hana mshahara.
Haikushia hapo, tangu uchaguzi wa TFF ufanyike miezi minane iliyopita, shirikisho hilo halijapata Katibu Mkuu na ndio maana tunaona Wilfred Kidao anakaimu nafasi hiyo.
TFF haijawahi kutangaza popote kutafuta Katibu Mkuu na pengine kwa kuona aibu wakaamua kumpa Kidao kukaimu nafasi hiyo.
Kiutaratibu nafasi ya Katibu Mkuu hutakiwa kufuata mchakato maalumu wa ajira, hapewi tu kwa sababu anajua kupiga porojo.
Sinema ikaendelea, viongozi wakuu wa TFF wakaona haitoshi, wakamfukuza kazi kimyakimya, Alfred Lucas kwa makosa ambayo hayajawahi kuwekwa wazi mpaka sasa. Fitina za soka letu acha tu.
Inadaiwa kuwa alifukuzwa kazi kwa sababu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita mjini Dodoma alionekana akimsalimia mgombea urais, Shija Richard jambo ambalo ni kosa kubwa katika soka letu la mizengwe.
Shija na Lucas, wote ni waandishi wa habari, ni marafiki wa siku nyingi, lakini wakati wa uchaguzi ilikuwa ni kosa kwa Ofisa Habari huyo wa TFF kumsalimu Shija.
Nafasi hiyo nayo kapewa mtu mwingine, Clifford Ndimbo ambaye yeye mwenyewe amesema anajitolea.
Kujitolea ina maana kuwa halipwi chochote na kama halipwi chochote, tunajiuliza bajeti ya mshahara wa ofisa habari wa shirikisho hilo inatumikaje?
Ukiangalia mlolongo huo, utagundua kuwa Rais wa TFF anajitolea (hana mshahara), Makamu wa Rais anakaimu, Katibu Mkuu anakaimu na Ofisa Habari anajitolea.
Hii inamaanisha kuwa hakuna mtu anayefanya kazi hapo, kila mtu anakwenda hapo kama kijiwe tu cha kuangalia mambo yake na ilimradi siku ipite.
Huwezi kuwa na viongozi na watendaji wa shirikisho la soka ambalo kila mtu anajitolea au anakaimu. Huwezi kuwa na maendeleo ya soka ya aina yoyote.
Uchaguzi wa mwaka jana Dodoma ulikuwa na matarajio makubwa kwa Watanzania, tulidhani tumepata viongozi ambao wangekaribia angalau nusu ya uongozi wa Leodegar Tenga, lakini madudu ambayo tunayaona ni aibu tupu hata ukisafiri kwenda nchi za jirani.