Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: Hakuna raha yoyote kumuaga huyu Amri Kiemba

Muktasari:

Mwaka 2006, Asante Kotoko ya Ghana ilikuja Uwanja wa Taifa kucheza na Yanga katika mechi ya kirafiki.

MAHALA fulani nilisoma Amri Kiemba akicheza mechi yake ya mwisho ya kuwaaga mashabiki. Nikasikitika kiasi.

Nikavuta kumbukumbu mbalimbali kuhusu Amri. Kipaji ambacho hakikufikia malengo yake hata kama atajidanganya kwamba alifikia malengo.

Mwaka 2006, Asante Kotoko ya Ghana ilikuja Uwanja wa Taifa kucheza na Yanga katika mechi ya kirafiki. Kocha wa Kotoko, Emmanuel Kwasi Afranie, ambaye kwa sasa ni marehemu alionekana kutokubali ukweli kwamba Kiemba alikuwa hajawahi kucheza Ulaya.

Afranie pamoja na nyota wa Kotoko walionekana kupagawa na Kiemba. Hawakujua wamkabili vipi. Aliulainisha mpira katika eneo la katikati. Aliufanya uonekane kitu rahisi. Afranie alidai Kiemba hakustahili kuichezea Yanga. Alistahili kucheza Ulaya.

Hivi ndivyo Kiemba alivyopoteza kipaji chake hapa. Kocha kama Afranie alifundisha Hearts of Oak, Asante Kotoko na timu ya Taifa ya Ghana anaposhangazwa na kipaji cha namna hii ujue anamaanisha anachosema. Wachezaji wengi wa Ghana wamepita katika mikono yake.

Mwaka 2012, nilikwenda pale Abidjan na kikosi cha Taifa Stars katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia 2014. Katikati ya uwanja, kocha Kim Poulsen aliwapanga, Kiemba, Sure Boy, Frank Domayo na Mwinyi Kazimoto.

Wote walikuwa katika ubora wao. Ulimi uliwatoka viungo wa Ivory Coast. Ndio, walitufunga, lakini viungo wa Stars wakiongozwa na Kiemba waliwahenyesha kina Cheickh Tiote ambaye kwa sasa ni marehemu kama ilivyo kwa Afranie.

Mwisho wa siku mashabiki wa Ivory Coast walijikuta wakiwapigia makofi wachezaji wa Taifa Stars. Hawakuamini sana walichokiona. Walidhani ingekuwa mechi nyepesi na walidhani katika upande wetu hakukuwa na watu ambao wangeweza hata kutuliza mpira na kugeuka achilia mbali mambo makubwa waliyokuwa wanafanya kina Kiemba.

Mwaka 2013, klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco ilikuwa inamtaka na ilishafanya mazungumzo na Simba kwa ajili ya kumchukua. Sijui nini kilitokea, lakini baadaye nilinong’onezwa kulikuwa na roho mbaya fulani ilitembea Kiemba asiende Morocco kwa sababu Simba walikuwa wanamtegemea sana.

Huyu ndiye Kiemba aliyeagwa juzi. Mafanikio yake makubwa yanabakia kuchezea timu tatu kubwa nchini, Yanga, Simba na Azam, halafu basi. Timu nyingine alizochezea ni ndogondogo tu ambazo hazikuwa za hadhi yake.

Kuna makosa mawili yamefanyika kwa Kiemba. Wakati anajiunga na Yanga akitokea Miembeni tayari alikuwa ameshachezea klabu kadhaa nchini. Kifupi ni kwamba alikuwa amepoteza muda mwingi kwa kuzurura huku na kule kabla ya kipaji chake kuaminika. Alikwenda Yanga akiwa mtu mzima kiasi.

Ni kosa ambalo tulifanya kwa marehemu Godfrey Bonny. Hii inatokana na tatizo letu la kushindwa kuskauti vipaji mapema. Sidhani kama tatizo hili litamalizika kwa sasa kwa vile klabu zetu zinapenda zaidi kugombania wachezaji kuliko kusaka vipaji.

Lakini hapo hapo kuna tatizo jingine kwa upande wa klabu na wachezaji wetu. Hata kama wamechelewa lakini huwa hawataki kuachana kwa wakati mwafaka. Mchezaji huwa hana hamu ya kuondoka kwa wakati mwafaka na hata klabu haitaki kumuachia kwa wakati mwafaka.

Kwa mfano, kwa nyakati zile, licha ya Kotoko kuonyesha nia ya kumtaka Kiemba lakini Yanga walikuwa hawagusiki kabisa ukijumlisha kwamba Kiemba alikuwa kiungo wao mpya. Ni kama lilipokuja suala la Wydad Casablanca, Simba ilihitaji pesa nyingi iliyopitiliza.

Matokeo yake leo tunamuaga Kiemba ambaye hajakitendea haki kipaji chake. Alipaswa kufika mbali zaidi kwa sababu mbili. Kwanza ni kwa sababu alikuwa na kipaji maridhawa, lakini pia alikuwa na nidhamu nzuri ndani na nje ya uwanja.

Kushindwa kwake kucheza mbali zaidi walikofika kina Mbwana Samatta na Simon Msuva ni aibu nyingine ambayo inatufanya tuinamishe vichwa wakati tunamuaga.

Sio kitu cha kujivunia sana kama wengine wanavyofikiria. Angeweza kufanya zaidi au jamii yetu ingeweza kufanya zaidi.

Tusiwe tunaona raha zaidi kuwaaga wachezaji wa aina yake. Tunapaswa kutafakari zaidi. Kama Kiemba leo akijaribu kuwaambia vijana wadogo alitumia vipaji kipaji chake sidhani kama inatosha kusema alicheza Simba, Yanga na Azam kabla ya kuzurura kwa kina Stand na Kagera Sugar. Kuna kitu cha kumbukumbu zaidi alipaswa kutuachia.