Yule kocha kiboko ya Yanga anatua Simba unaambiwa

Muktasari:

Matola alipoulizwa juu ya kutimkia Msimbazi alisema: “Naomba uniache mpaka jioni (jana Ijumaa) nadhani ukinitafuta nitakuwa na jibu kamili la kukujibu, lakini kwa sasa sitaweza kukuambila lolote kuhusu suala hilo.”

TAARIFA za Simba kumtaka Kocha wa Polisi Tanzania, Suleiman Matola zimekuwa faraja kwa uongozi wa maafande hao ambao kwa sasa wanasubiri taarifa rasmi iwafikie mezani ili wamalizane.

Kocha huyo ambaye amekuwa akiisumbua Yanga tangu akiwa Lipuli, anatarajiwa kuongeza chachu ya mafanikio ndani ya Simba, kutokana na kuifahamu kwa undani. Katika msimu uliopita aliiondoa Yanga kwenye michuano ya FA katika hatua ya robo fainali. Pia, msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara, Polisi Tanzania ilitoka sare ya mabao 3-3 na Yanga Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munis alisema hawana tatizo na kocha huyo wala Simba, na hilo litakuwa limewapa heshima kubwa kocha kuondoka kwa amani kwa sababu timu nyingine zimekuwa zikiwafukuza makocha wao.

“Bado tuna mkataba na Matola, hivyo kama anatakiwa na timu nyingine hakuna tatizo, aangalie mkataba unasemaje nasi tutamtakia heri aendako maana hiyo ni kazi yake,” alisema.

“Na kocha anapofanya vizuri hufungua milango mingine, hivyo hatuna sababu ya kumzuia maana tumefanya naye kazi vizuri na tunaishi safi.

“Kwa sasa hatuna taarifa rasmi kwani tunasikia kwenye vyombo vya habari, hata Matola hajaliongea hilo na litakapotufika mezani tutamalizana kwa upande mmoja kumlipa mwenzake kama mkataba unavyoeleza.” Kuhusu kuagana na wachezaji, Munis alipinga hilo akieleza wachezaji wamepewa mapumziko ya wiki moja baada ya mchezo dhidi ya Namungo FC na Poilisi kulala bao 1-0 Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa, Lindi na wanatarajia kuingia kambini wiki ijayo kujiandaa na michezo ya ligi.

Matola alipoulizwa juu ya kutimkia Msimbazi alisema: “Naomba uniache mpaka jioni (jana Ijumaa) nadhani ukinitafuta nitakuwa na jibu kamili la kukujibu, lakini kwa sasa sitaweza kukuambila lolote kuhusu suala hilo.”

Wakati akisaini Polisi Tanzania, Matola alisema falsafa yake haitabalidilika kwa kuwapa kipaumbele wachezaji wazawa kuliko wageni kutokana na mfumo wa soka la Tanzania lilivyo na hilo limeonekana kwani hakuna mchezaji wa kigeni kwenye kikosi hicho.

“Nilipokuwa Lipuli FC wachezaji wangu walitoka hapa nchini, hivyo hakuna mabadiliko kwenye hilo, ndio maana tunahitaji kuanza kazi mapema kuwaweka wachezaji pamoja kabla ya ligi kuanza,” alisema Matola wakati akisaini mkataba kwa maafande hao.

MATOLA NI NANI

Alizaliwa Aprili 24, 1978 ambapo alizitumikia timu mbalimbali wakati akicheza mpira akianza Simba kabla ya kutimkia SuperSport United ya Afrika Kusini mwaka 2006.

Kisha kiungo huyo wa zamani alirejea tena Msimbazi na kustaafu hapo mwaka 2009.

Katika ukocha alianza kufundisha kikosi cha vijana cha Simba kabla ya kuifundisha timu ya wakubwa akiwa msadizi wa makocha Patrick Phiri, Goran Kopunovic na Zdravko Logarusic kwa nyakati tofauti baadaye alitimkia Geita Gold FC, Lipuli FC kabla ya kutua Polisi Tanzania.