Prime
Kinachoibeba Yanga Kariakoo Dabi

Muktasari:
- Hadi tunapokwenda kushuhudia mchezo wa Dabi ya Kariakoo utakaochezwa leo kati ya Yanga dhidi ya Simba, Yanga ndio vinara wa ligi ikiongoza kwa pointi 79, ikicheza mechi 29, ikishinda 26, imepoteza mbili na sare moja.
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga haipo mbali kufukuzia taji hilo kwa mara ya nne mfululizo ambapo licha ya changamoto mbalimbali ilizopitia, kikosi hicho bado kipo njia kuu kikitaka kulinda heshima.
Hadi tunapokwenda kushuhudia mchezo wa Dabi ya Kariakoo utakaochezwa leo kati ya Yanga dhidi ya Simba, Yanga ndio vinara wa ligi ikiongoza kwa pointi 79, ikicheza mechi 29, ikishinda 26, imepoteza mbili na sare moja.
Mwendo mzuri wa Yanga katika kuwania ubingwa unatokana na Simba ambao wako nafasi ya pili kuzidi kuwapa upinzani mkali msimu huu katika kuwania taji hilo.
Mbali na hilo, kuna mambo kadhaa yanayoibeba Yanga hadi kufikia hapo ikiwemo ubora wa wachezaji, mbinu na umoja.
KIKOSI
Msimu huu Yanga bado iko bora na mziki wa kikosi chao ni kama umeongezewa nakshi baada ya kuingiza wachezaji wachache wenye makali ambao wanaendelea kuipa thamani kubwa timu hiyo uwanjani.
Msimu huu Yanga iliwaongeza mshambuliaji Prince Dube, viungo Clatous Chama, Duke Abuya, Aziz Andambwile na kipa Khomeini Abubakar ambao waliingia dirisha kubwa la usajili lakini katikati ya msimu ikawaongeza beki mmoja Israel Mwenda na winga Jonathan Ikangalombo.
Wachezaji hao kila mmoja amekuwa na mchango wake ndani ya kikosi hicho kwa kiwango tofauti.
MABADILIKO YA MAKOCHA
Huenda msimu huu hata mashabiki wa Yanga walishtushwa na namna kikosi chao kilipopitia kufundishwa na makocha watatu tofauti yasiyoepukika, wakianza msimu na kocha aliyewapa ubingwa msimu uliopita Miguel Gamondi ambaye baada ya kupoteza mechi mbili dhidi ya Azam (1-0) kisha Tabora United (3-1) ajira yake iliishia hapo.
Kuondoka kwa Gamondi, akashushwa kocha Mjerumani Sead Ramovic ambaye naye hakukaa muda mrefu, Yanga ilipoishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na presha kuanza kumkumba, akafanya uamuzi mgumu wa kutimkia CR Belouizdad ya Algeria iliyokuwa inamuwinda.
Kuondoka kwa Ramovic, Yanga ikamchukua kocha Mfaransa mwenye asili ya Algeria, Miloud Hamdi ambaye ndiye anaendelea na maisha ya kukiongoza kikosi hicho mpaka sasa akielekea kuumaliza msimu na matumaini ya kubeba ubingwa.
MASTAA
Yanga msimu huu inabebwa na mastaa watatu wakiwemo washambuliaji wawili Dube na Clement Mzize ambao wote ndio vinara wa ufungaji wakifunga mabao 13 kila mmoja wakizidiwa matatu na kinara wa ufungaji kwenye ligi ambaye ni kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua (16).
Washambuliaji hao wanaonekana kumpokea kijiti kiungo Stephane Aziz KI ambaye ndiye alikuwa staa muhimu msimu uliopita akiibuka mfungaji bora kwenye ligi akifunga mabao 21 lakini pia akibeba tuzo ya mchezaji bora wa msimu kwenye ligi. Aziz Ki ameondoka Yanga Aprili mwaka huu na kutimkia Wydad Casablanca ya Morocco ambapo wakati anaondoka alikuwa amefunga mabao tisa na asisti saba.
Nyuma ya Dube na Mzize, yupo kiungo Pacome Zouzoua ambaye ana mabao 11 na asisti tisa, moto wake kwenye mechi za timu hiyo ni mkubwa kutokana na ubora wa kutengeneza mashambulizi makali akiwa na ufundi mkubwa miguuni.
MSIMU ULIOPITA ILIKUWAJE?
Msimu uliopita Yanga ilichukua ubingwa wa ligi ikicheza mechi 30, ikishinda 26, ikitoa sare mbili, ikipoteza pia mbili, ikafunga mabao 71 huku ikiruhusu 14 ikimaliza na jumla ya pointi 80, ikiwa ndio timu iliyokuwa na takwimu bora zaidi katika msimu huo ikichukua tuzo ya timu bora, kocha bora, mfungaji bora na mchezaji bora wa msimu.
Msimu huu kama Yanga itaifunga Simba mechi ya leo, maana yake itamaliza na pointi 82 ambazo ni mbili zaidi ya za msimu uliopita.
Mbali na hilo, pia katika mechi 29 ilizocheza Yanga, imeshinda 26, sare moja na kupoteza mbili, huku ikifunga mabao 81 na kuruhusu 10. Ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi na kuruhusu machache zaidi, takwimu hizo za mabao pia ni bora kulinganisha na msimu uliopita ambapo ilifunga mabao 71 na kuruhusu 14.
ILIPOPATIA
Yanga kuwa kwenye ubora huu pongezi nyingi zinatakiwa kwenda kwa uongozi wa klabu hiyo chini ya rais wa klabu hiyo Injinia Hersi Said na kamati yake ya utendaji kutokana na namna walivyokuwa wanakitunza kikosi chao ambacho kimekuwa hakifanyiwi marekebisho makubwa zaidi ya kufanya maboreshi yaliyohitajika.
Huko nyuma Yanga ilikuwa ni kama inafanya usajili wa fasheni kwa kila dirisha kusajili wachezaji wengi kisha dirisha linalofuata wanabadilisha, hulka ambayo kwasasa imeondoka ikiendelea kukiboresha kikosi chao taratibu kulingana na changamoti wanaziona.
MSIKIE HAMDI
Akizungumzia ubora wa kikosi chake na malengo yao, Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi anasema: “Nilipofika hapa wote mnafahamu kwamba niliikuta timu ikiwa kwenye mashindano kwahiyo ilikuwa ngumu kufanya mabadiliko mengi ndani ya muda mfupi, kuna vitu vichache tulibadilisha lakini kuna wakati tuliacha yale mazuri yaendelee ili tuache timu iendelee kufanya vizuri.”
Kuhusu ubora wa kikosi hicho, Hamdi anasema: “Kusema ukweli hapa Yanga kuna kikosi kinachoundwa na wachezaji bora, unaona kwasasa hatuna majeruhi wengi, hili linatoa changamoto namna ya kuchagua nani acheze, nani asubiri na nani akose mechi hii, sio kitu rahisi kwa kuwa kila mchezaji anatamani kucheza kuisaidia timu lakini pia kwa faida yake.
“Nimewaambia wachezaji wale ambao wanafanya vizuri wazidishe juhudi kwa kuwa timu inaruhusu ukiona kule mbele tumeendelea kufunga mabao mengi lakini pia wakati nafika hapa tulikuta timu inaruhusu mabao mara kwa mara, tumeweka mbinu zetu sawa na hali hiyo inazidi kuondoka.
“Nataka kuwa na kikosi kinachocheza mpira wa kuvutia lakini pia ishinde vizuri mashabiki wetu wafurahi.”
Katika hatua nyingine, Hamdi anasema Yanga bado itaendelea kupigania mataji yote mawili yaliyosalia ambayo pia wanayatetea ukiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) ambapo Jumapili ijayo itacheza fainali dhidi ya Singida Black Stars.
“Tuna jukumu la kutetea ubingwa wa ligi, hiki ni kitu ambacho hakiepukiki, tunajituma ili kuhakikisha ubingwa huu tunaendelea kuushikilia, nafahamu ligi ni ngumu lakini kama Yanga hatutakiwi kuogopa kwa kuwa nia na ubora wa kufanya hayo tunao, tutafanya kila linalowezekana kuchukua ubingwa huu na lile Kombe la FA.
“Nawashukuru sana viongozi wangu wako karibu sana na timu lakini muhimu kuliko wote ni mashabiki wetu, kila unapopita sehemu au tunapoingia uwanjani ukiona ule umati uliovaa jezi za njano na kijani akili yako inausukuma moyo kwamba una deni kwa hawa watu waliokuja kuwapa nguvu.
“Nimefundisha timu nyingi Ulaya na hapa Afrika lakini sijawahi kuona mashabiki wanaovutia kama hawa wa hapa Yanga, unakwenda sehemu nyingine unakutana na watu wanaoipenda hii timu kama wale kule ulipotoka, hii sio kitu ambacho unaweza kupuuzia lazima ujitume ili kuwafurahisha lakini pia uweke sawa malengo ya timu.”