Yanga vs Polisi : Maswali ni mengi bila majibu

Muktasari:

Unapofikiria kiwango kilichoonyeshwa na Juma Abdul kisha ukatazama na uamuzi wa Kocha Zahera kutompanga unaweza kujikuta na maswali mengi kichwani yanayokosa majibu ya maaana.

LICHA ya wengi kutoridhishwa na kiwango chake, David Molinga ameanza kazi ya kuifungia mabao Yanga, baada ya juzi Alhamisi kupachika mawili katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania ambao, ulimalizika kwa sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Matokeo ya juzi yameonekana kutowafurahisha Yanga, lakini kwa Molinga kufunga mabao mawili kunawapa faraja na matumaini kwamba, mshambuliaji huyo atawasaidia kwenye mashindano mbalimbali yaliyo mbele yao siku za usoni.

Jicho la Mwanaspoti lilitazama dakika 90 za mchezo huo wa Ligi Kuu juzi pamoja na ule wa Azam dhidi ya Ndanda FC na likang’amua mambo kadhaa yanayoainishwa hapo chini.

Juma Abdul anazua maswali

Kocha Mwinyi Zahera amekuwa hampi nafasi beki wa kulia, Juma Abdul katika michezo ambayo Yanga imekuwa ikicheza kwenye mashindano mbalimbali akidai hayupo fiti huku akilazimisha kuwapanga wachezaji ambao, kiasili hawachezi kwenye nafasi hiyo.

Juzi Alhamisi beki huyo alipewa nafasi na alionyesha kiwango bora kati safu ya ulinzi, lakini kubwa zaidi alipandisha mashambulizi ya mara kwa mara kama alivyozoeleka na kwa kuthibitisha hilo, alizalisha mabao mawili ya Yanga yaliyofungwa na Mrisho Ngassa na David Molinga kutokana na krosi zake.

Unapofikiria kiwango kilichoonyeshwa na Juma Abdul kisha ukatazama na uamuzi wa Kocha Zahera kutompanga unaweza kujikuta na maswali mengi kichwani yanayokosa majibu ya maaana.

Kujiamini kuliwaponza Polisi

Baada ya kuongoza kwa mabao 3-1, wachezaji wa Polisi Tanzania walionekana kucheza kwa kuridhika na kupunguza kasi yao ya mashambulizi waliyokuwa nayo mwanzoni kabla hawajaongoza wakionekana kujiamini kupita kiasi na kushindwa kuipa heshima stahiki Yanga kama timu kubwa na inayocheza katika uwanja wake wa nyumbani.

Hilo liliwafanya wapoteze nidhamu ya mchezo na kujikuta wakiruhusu mabao mawili yaliyoifanya mechi iishe kwa sare ya mabao 3-3 na hivyo, kushindwa kuandika historia ya kuwa miongoni mwa timu chache zilizoweza kupata ushindi mnono ugenini dhidi ya Yanga kwenye Ligi Kuu.

Kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa Polisi Tanzania kuibuka na ushindi ikiwa wangeipa heshima Yanga na kucheza kwa nidhamu huku wakifanyia kazi mbinu za kiufundi.

Makame ameendeleza alipoishia

Kiungo wa Yanga, Abdulaziz Makame alionyesha kiwango bora kwenye mchezo baina ya Yanga na Zesco United ingawa mechi iliisha vibaya kwa upande wake, baada ya kujifunga na kuifanya timu hiyo itolewe kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, ndani ya muda mfupi ameonekana kulisahau hilo na kutazama mbele na hilo limejidhihirisha katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania juzi ambapo, alionyesha kiwango bora kwa kutibua mipango na mashambulizi ya wapinzani wao, kuchezesha timu na kuiunganisha vyema hasa pale walipokuwa wakisaka mabao ya kusawazisha.

Nchimbi ameimarika

Ni mshambuliaji mwenye nguvu na stamina, lakini kwa muda mrefu alikuwa anakosa utulivu pindi anapokuwa na mpira kwenye eneo la timu pinzani.

Hata hivyo, anaonekana kuwa wa tofauti msimu huu kwani amekuwa hana pupa pindi akiwa karibu na lango na anakaa kwenye nafasi sahihi jambo ambalo alilionyesha kwenye mechi ya juzi na kudhihirisha hilo, alipachika mabao yote matatu ya Polisi Tanzania.

Usibeti kwa Molinga

Kwa wale wataalamu wa michezo ya kubashiri matokeo ‘kubeti’ wanaweza kulielewa hili zaidi.

Kwa vyovyote vile hupaswi kubeti chochote kuhusu Molinga kwani, anaweza kusababisha mkeka wako kuchanika mapema tu. Ni mchezaji, ambaye kiwango chake kimekuwa hakieleweki kwani kuna nyakati anaweza kufanya vizuri kisha nyingine akaharibu.

Mfano katika mechi ya juzi, alianza kwa kucheza vibaya huku akikosa mabao takribani matatu ya wazi hadi kuwafanya mashabiki wa Yanga kushinikiza benchi la ufundi kumfanyia mabadiliko.

Hata hivyo, baadaye alipachika mabao mawili muhimu kwa Yanga jambo lililoamsha ndelemo na vifijo.

Azam wamejitathmini

Hawakuonyesha kiwango bora kwenye mchezo dhidi ya KMC ingawa walipata ushindi wa bao 1-0 kisha wakaja kutupwa nje kwenye Kombe la Shirikisho kwa kufungwa jumla ya mabao 2-0 kwenye mechi za nyumbani na ugenini dhidi ya Triangle United ya Zimbabwe. Lakini, katika mchezo dhidi ya Ndanda FC Jumatano iliyopita, walionyesha kiwango kizuri kwa kutengeneza nafasi za kutosha na kumiliki mpira huku wakipachika mabao mawili yaliyowafanya waibuke na ushindi katika mchezo huo.