Yanga SC marufuku kwa Ditram Nchimbi

Muktasari:

Mwanaspoti lilimsaka Nchimbi, ambaye alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote hadi muda utakapofika ndipo kila kitu kitakuwa hadharani.

JINA la mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi linatamkwa sana na mabosi wa Yanga kwa sasa. Ni miongoni mwa majina ambayo yameanza kuundiwa mkakati kutokana na kutajwa na makocha na wachambuzi wa soka nchini kwamba, anaweza kuwa tiba kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa butu.

Hata hivyo, uongozi wa Polisi Tanzania umeshtukia mkakati wa straika huyo kusogezwa Mitaa ya Twiga na Jangwani na kuamua kutoa onyo mapema kwa mabosi wa Yanga.

Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munis amesema wamebaini Yanga imeanza mikakati ya chini kwa chini kumnasa Nchimbi na kuwataka kufuata taratibu.

Amesema kitendo hicho hakikubaliki na Yanga wanafahamu utaratibu wa kufuata wanapotaka kusajili mchezaji.

“Tunashangaa kuona watu wanaanza kutangaza mambo yao, wakisahau mchezaji huyo bado tuna mkataba naye ambao ni wa mkopo kutoka Azam FC. Hatuogopi mchezaji kuondoka lakini timu ambazo zinahitaji huduma yake ni lazima ziheshimu taratibu za klabu,” alisema Munisi.

Aliongeza kwa kufanya hivyo ni kumharibu mchezaji wao kiwango na kwamba, hata Polisi kuna wachezaji inawahitaji kutoka Yanga, lakini wanasubiri muda ufike ndipo wajitokeze mezani kufanya mazungumzo nao.

“Yanga wanapaswa kusubiri hadi dirisha la usajili lifunguliwe kama tutakubaliana hatuna sababu ya kumng’ang’ania mchezaji, lakini tunataka heshima kwa sababu wanaonekana hawaheshimu taratibu za mkataba,” aliongeza Munis.

Mwanaspoti lilimsaka Nchimbi, ambaye alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote hadi muda utakapofika ndipo kila kitu kitakuwa hadharani.

Nchimbi alisema akili yake kwa sasa imeielekeza kwenye Timu ya Taifa, Taifa Stars ambayo leo Ijumaa itakipiga na Equatorial Guinea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kusaka tiketi ya kucheza AFCON 2021.

“Kwa sasa nipo kambini Stars kujiandaa na mchezo wa kesho (leo), hayo mambo mengine tuyaache yapite kwanza kisha tutajua nini kinafuata kwa kuwa yamezungumzwa mengi,” alisema Nchimbi.

Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alipoulizwa kuhusiana na onyo hilo la Polisi Tanzania, alisema usajili hufanywa na Kamati ya Ufundi kwa kushirikiana na Kamati ya Usajili baada ya kupokea majina yaliyopendekezwa na benchi la ufundi kisha hupelekwa Kamati ya Utendaji kwa hatua zaidi.

“Kamati ya Ufundi bado haijaanza hilo zoezi, hivyo kama kuna mtu anajitambulisha kwa niaba ya Yanga labda kwa sababu ni mdau. Uongozi bado haujafanya mawasiliano ya kiofisi na mchezaji yEyote mpaka hivi sasa,” alisema Bumbuli.

NCHIMBI NI NANI?

Alizaliwa Machi 10, 1997 huko Ruvuma na alianza maisha ya soka kwenye kikosi cha Usalama FC kilichokuwa Ligi Daraja la Nne na baadaye kuibukia Small Boys iliyokuwa Ligi Daraja la tatu, baadaye alitua Mbinga United ambayo ilikuwa Ligi Daraja la Tatu na kubeba ubingwa wa Mkoa wa Ruvuma na kwenda kwenye Ligi ya Kanda (sasa Ligi Mabingwa wa Mikoa (RCL).

Mwaka 2013 baada ya kuipeleka Timu ya Mbinga United RCL, Majimaji FC iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ikamnyakua na hapo alikaa hadi mwaka 2015 timu ilipopanda Ligi Kuu na kufunga jumla ya mabao 15 pamoja na asisti nane.

Baada ya timu kupanda Ligi Kuu na kucheza nusu msimu alitimkia Mbeya City alikodumu kwa msimu mmoja na nusu akifunga mabao MAnane na asisti 12 na alipomaliza mkataba wake msimu wa mwaka 2017/18 alisajiliwa na Njombe Mji iliyokuwa Ligi Kuu.

Akiwa Njombe Mji ndani ya msimu mmoja akifunga mabao saba na asisti sita wakati timu yake ikishuka daraja, Nchimbi alitimkia Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili na mchezaji huyo mpaka sasa mkataba wake na Azam umebaki miezi minane.

Lakini alipotua Azam FC alikuwa kwenye kikosi cha timu kilichobeba ubingwa wa Cecafa mwaka jana kwa kuifunga Simba 2-1, lakini kutokana na ushindani wa namba alitimkia Mwadui FC kwa mkopo ambako alikuwa na mchango mkubwa katika mabao 19 aliyofunga, Salum Aiyee kwa kutoa asisti 11 huku yeye akifunga mabao manne.

Alipomaliza msimu, Azam FC ikampeleka Polisi Tanzania kwa mkopo wa mwaka mmoja. Mpaka sasa amefunga mabao matatu Ligi Kuu ambayo aliifunga Yanga kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3 Uwanja wa Uhuru na kuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga hat trick.

Siku moja baada ya kuifunga Yanga, Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alimwita timu ya taifa katika mchezo wa mwisho wa kufuzu Chan dhidi ya Sudan na katika mchezo huo alihusika kupatikana bao la kwanza lililofungwa na Erasto Nyoni kabla ya kufunga bao la pili lililoipa Stars ushindi wa maba 2-1.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga imetengeneza mabao sita kwenye Ligi Kuu, hivyo safu hiyo inazidiwa nguvu na mabeki katika kufumania nyavu na inaweza kumfanya Kocha, Charles Boniface Mkwasa kusaka washambuliaji wengine.