Uzito wamtibulia Juma Abdul

Muktasari:

Beki huyo alisema, aliongezeka kilo 12, alipokuwa fiti alikuwa na kati ya 64 na 65 na aliporudi kutoka kwenye majeruhi, alikuwa na 76 ambazo kwa sasa amezikamua na kurudi kwenye hali yake.

BEKI wa kulia, Juma Abdul, ameweka wazi majeruhi yaliyomsababishia aongezeke kilo 12, ndio yalimwaribia akashindwa kufanya vizuri ndani ya klabu yake ya Yanga na timu ya taifa, lakini baada ya kurudishwa kwenye kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, amesisitiza gari ndio limewaka, lazima watamtaka.

Abdul aliyetangazwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-2016, akiwashinda Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba na Shiza Kichuya alipokuwa Mtibwa Sugar, akapotea jumla na mpaka sasa anarudishwa timu ya taifa na Kocha Mrundi Etienne Ndayiragije, imepita miaka minne.

“ Kitu kikubwa ambacho kilinipoteza kwenye soka ni kwa sababu ya maumivu. Nilikuwa kwenye majeruhi kwa kipindi kirefu, niliporudi uzito mkubwa uliongezeka hivyo ikawa changamoto kubwa kupambania nafasi na wenzangu ambao niliwakuta wako tayari.”

Beki huyo alisema, aliongezeka kilo 12, alipokuwa fiti alikuwa na kati ya 64 na 65 na aliporudi kutoka kwenye majeruhi, alikuwa na 76 ambazo kwa sasa amezikamua na kurudi kwenye hali yake.

“Kama nilivyosema, majeruhi na uzito ndio sababu kubwa iliyonipoteza mimi kwenye ramani ya soka na baada ya kuligundua hilo, nilipofanyia kazi, nimerudi kwenye hali yangu,” alisema Abdul.

“Ukiachana na changamoto hizo, kwenye kazi mimi najiamini ni mchezaji mzuri. Ninachotakiwa ni kufanya mazoezi na kucheza kwa bidii ili niweze kuisaidia timu na mimi mwenyewe.

“Nashukuru mwalimu kuona uwezo wangu na kuniita kwenye kikosi chake, upande wangu sitamwangusha, namwahidi yeye pamoja na Watanzania wote ni mapambano na kuwapa raha wanayohitaji, kikubwa ushirikiano,” alifafanua.

Alisema anakwenda kutumia mashindano ya Chalenji ambayo Kilimanjaro Stars inakwenda kushiriki vizuri ili awe fiti kwa sababu ya kucheza.