Ukistaajabu ya Juma Abdul, utashangazwa na ya Nchimbi

Muktasari:

Ni kama inavyofikirisha hatua ya Kocha Etienne Ndayiragije, kuamua kumuita katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars straika Ditram Nchimbi wa Polisi saa chache baada ya kutupia hat trick kwenye lango la Yanga walipovaana Uwaja wa Uhuru.

ACHANA na ile mikogo yake wakati wa kutaka kupiga faulo, lakini bao alilotupia kambani kiufundi limemfanya straika David Molinga ‘Falcao’ kugeuka shujaa ghafla.
Kabla ya hapo Molinga alikuwa ndiye mchezaji aliyekuwa akipondwa na kuonekana mzigo kati ya nyota wapya waliosajiliwa ndani ya kikosi cha Yanga.
Hata hivyo, baada ya kuondoa gundu jijini Mwanza kwa kufunga mabao matatu kwenye mechi za kirafiki dhidi ya Pamba na Toto Africans iliwafanya mashabiki kujishtukia na hasa Kocha Mwintyi Zahera alipoamua kumpamba ile kipapaa!
Zahera alikaririwa akisema kuwa Molinga ni bonge la mchezaji na anayejua kufunga na ndani ya Ligi Kuu msimu huu atafunga sana na kumkadiria atatupia kambani kati ya mabao 15-20 na asipotimiza idadi hiyo basi yu radhi akatwe mkono wake.
Hata hivyo, juzi kati kwenye mchezo wa Yanga dhidi ya Polisi, Yanga ikiwa yuma kwa mabao 3-1, Molinga alithibitisha kile alichokisema kocha wake, kwani alifunga bao tamu la kichwa akimalizia krosi ya Juma Abdul, kisha kumaliza udhia kwa kusawazisha bao kwa mpira wa faulo.
Bao hilo si tu liliwatuliza mashabiki wa Yanga, lakini limemfanya Molinga kuonekana shujaa ghafla, kwani mzee mzima alikuwa anakaribia kuumbuka kwa mara ya pili katika Ligi Kuu.
Mmesahau kama walitungulia bao 1-0 na Wazee wa Kupapasa, Ruvu Shooting ya Masau Bwire.
Hata hivyo kwa wanaokumbuka, niliwahi kuandika hapa kwamba, Yanga haijauziwa mbuzi kwenye gunia kwa Molinga na mashabiki wampe muda kama waliompa Obery Chirwa Jangwani na kuja kuwa shujaa wa timu hiyo kabla ya kutimkia Arabuni na baada kurejea nchini kukipiga Azam FC.
Kitu ambacho kilichosisimua kwenye mchezo huo wa Yanga na Polisi, ukiachana na mabao mawili ya Miolinga, kuna maajabu mengine yaliyojitokeza na kuwaacha hoi mashabiki wa soka na wadau wengine wa mchezo huo.
Beki Juma Abdul ambaye aliripotiwa na Kocha Zahera kuwa, hakuwa fiti ndio maana amekuwa akimkaushia, alianza na kucheza kwa dakika zote 90 na kuasisiti mabao mawili, moja lililofungwa na Molinga na jingine la kwanza lililofungwa na Mrisho Ngassa.
Mashabiki wamebaki na maswali mengi, mchezaji ambaye hakuwa fiti siku chache tu zilizopita vipi acheze kwa dakika 90 na kuupiga kama ambaye hakuwa na tatizo.
Bila shaka, kuna jambo ambalo Zahera alikificha juu ya beki huyo mzoefu kwa kushindwa kumtumia kwenye mechi dhidi ya Zesco United na inaelezwa baadhi ya wachezaji, walihoji kuchezeshwa Ali Ali na kuachwa kwa Abdul nje.
Binafsi bado naheshimu maamuzi ya Kocha Zahera, kwani yeye ndiye mtu wa mwisho katika kujua nani amtumia na nani amweke benchi, lakini bado inafikirisha mno ghafla tu Abdul kurejea kikosi cha kwanza.
Ni kama inavyofikirisha hatua ya Kocha Etienne Ndayiragije, kuamua kumuita katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars straika Ditram Nchimbi wa Polisi saa chache baada ya kutupia hat trick kwenye lango la Yanga walipovaana Uwaja wa Uhuru.
Nchimbi alikuwa Azam wakati Ndayiragije akitua katika klabu hiyo akitokea KMC na bila shaka alikuwa akijua uwezo wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Njombe Mji.
Hata hivyo Nchimbi alitolewa kwa mkopo kwenda Polisi na hakuwahi kuitwa Stars ya Ndayiragije mpaka juzi baada ya kufanya mambo dhidi ya Yanga ghafla ikatangazwa ameongezwa kikosini kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda.
Sio kitu cha ajabu kwa Nchimbi kuitwa Stars, lakini inashangaza kidogo kwani ni muda mrefu kijana huyo amekuwa akifanya mambo tangu akiwa Majimaji Songea aliyoipandisha daraja tena akiwa mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza msimu 2015.
Hata alipokuwa Njombe kisha kuchukuliwa na Azam waliomtoa kwa mkopo kwa mara ya kwanza Mwadui, bado jamaa alikuwa akionyesha ana kitu miguuni mwake, lakini huko kote hakuonekana, ila mabao yake dhidi ya Yanga yamempaisha.
Ieleweke wazi wala sina tatizo kwa Nchimbi kuitwa Stars na bado nakubaliana na maoni ya utetezi wa Ndayiragije na ya makocha wengine wanaoamini ni sahihi kuitwa kwa mshambuliaji huyo, lakini inafikirisha siku zote mbona hakuonekana?
Pia ni jambo la heri kama Nchimbi atafanya makubwa Stars na kutomuangusha Kocha Ndayiragije, lakini akichemka ni wazi atamweka pabaya kocha huyo, kwani tayari kuna wadau wameanza kuhoji kitendo chake.
Hata hivyo, bado naamini Nchimbi kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa Tanzania wana haki ya kulitumikia taifa lake, tatizo labda ni namna alivyoitwa kwenye timu hiyo na kufanya ifikirishe kama Juma Abdul alivyowafikirisha Wanayanga kwa Zahera.