Niyonzima! Hebu msikilize Juma Abdul hapa

Muktasari:

Huyu hapa beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul ambaye ni shabiki mkubwa wa krosi za Niyonzima, akifunguka mazito.

UNADHANI zile krosi, friikiki na pasi za maudhi zinazopigwa na kiungo fundi wa Simba, Haruna Niyonzima huwa zinawapagawisha mashabiki pekee? Basi unaambiwa hadi wachezaji wenzake uwanjani hupatwa mzuka na wengine kutamani kuwa na uwezo wa kupiga krosi zenye madhara kama zake.
Huyu hapa beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul ambaye ni shabiki mkubwa wa krosi za Niyonzima, akifunguka mazito.
Abdul kwa sasa amepoteza nafasi yake kwa Paul Godfrey a.k.a Boxer kwenye kikosi cha Yanga, lakini hapo awali mpira haiwezi kumalizika bila kupiga makrosi matata ambayo huipa Yanga mabao. Lakini, kitu ambacho hufahamu ni kuwa Abdul, ambaye msimu wa 2015-16, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu kutokana na mchango wake, amevuna maujuzi hayo kwa Niyonzima.
“Siri ya kupiga krosi kwa washambuliaji nilijifunza kutoka kwa Niyonzima (Haruna), ambaye ndiye amechangia sana kunifanya niwe hivyo.
“Nilikuwa napiga krosi lakini za kawaida na siku moja tukiwa mazoezini nilimfuata na kumuomba anielekeze ufundi wake wa kupiga krosi zenye madhara kwa wapinzani.
“Alinifundisha na nilipoelewa kazi ikaanzia hapo, huwa sijisikii furaha kama nitatoka uwanjani bila kupiga krosi iliyozaa bao na mara nyingi huwa natenga muda wa kutosha kufanya mazoezi binafsi ya kupiga krosi ili kuimarika,” alisema Abdul ambaye kocha Jamhuri Kihwelu alimfananisha Dani Alves.