Ushujaa wa Stars wawakosha wadau

Muktasari:

Taifa Stars imekosha mioyo ya wadau wa soka nchini kuonyesha ushujaa wa kushinda ugenini baada ya kupoteza mechi ya nyumbani, jambo waliloliona wachezaji waliuvaa uzalendo.

KUFUZU kwa timu ya Taifa 'Taifa Stars' kucheza fainali za CHAN mwakani kimewaibua wadau ambao wamepongeza kazi kubwa iliofanywa na wachezaji kujitoa mhanga licha ya mashabiki kuukatia tamaa mchezo huo.
Mussa Hassan 'Mgosi' amesema ifikie hatua wachezaji wasiwe wanasikiliza maneno ya mashabiki ya kuwakatisha tamaa badala yake wafanye kazi kwa kujitolea akiamini ndio itakayowajengea heshima.
"Unapotamkwa uzalendo una maana ya kujitoa pasipo kutaka fadhira, unafanya kitu kwa hali na mali ili mladi kifanikiwe ndicho wamekifanya Stars dhidi ya Sudan,"
"Haikuwa rahisi baada ya kupoteza mechi jijini Dar es Salaam kwenda kushinda ugenini na hilo ndilo lililowakatisha tamaa mashabiki, wachezaji wameamua kujitofautisha na mawazo yao, wanastahili pongezi pamoja na kocha wao,"amesema.
Mtazamo wake kuhusiana na maandalizi ya CHAN 2020 amesema inahitajika nguvu ya umoja na kujiandaa zaidi kutokana na ugumu ambao watakutana nao.
"Ugumu utakuwa zaidi kuliko walivyocheza na Sudan, wajipange naamini wataendelea kufanya makubwa zaidi, kocha aendelee na mbinu zake naamini ameonyesha kitu,"amesema.
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amesema Taifa Stars wameonyesha ushujaa kufanya maajabu ugenini licha ya kupoteza nyumbani.
"Si kazi ndogo kwenda kushinda ugenini, hii inaonyesha ni kiasi gani kocha amekuwa mzuri wa kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake kuamini katika kujituma kwa bidii,"amesema.