Wanafunzi kuishangilia Stars mwanzo mwisho -VIDEO

Muktasari:

Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma vyuo mbalimbali nchini Sudan wamejiandaa kuipa nguvu Stars usiku wa leo.

WANAFUNZI raia wa Tanzania wanaosoma nchini hapa wameweka wazi kuiunga mkono timu ya Taifa 'Taifa Stars' ambayo itakuwa na kibarua kigumu usiku wa leo Ijumaa uwanja wa El  Merreikh Omdurman.

Salum Abdallah anayesoma chuo cha International University of Afrika amesema wao wamejiandaa kuhakikisha wanajitokeza uwanjani kupiga shangwe.

"Mimi ni rais wa chuo changu, hivyo tumeandaa utaratibu mzuri wa kuingia uwanjani na kuiunga mkono timu yetu ya Tanzania," alisema.

Abdallah alisema kwa muunganiko wa haraka haraka wanaweza kupatikana wanafunzi takribani 600 kwaajili ya kuungana kwa pamoja kuishangilia Stars.

Akizungumzia upande wa usalama kwa upande wao kuishi huku, alisema hakuna changamoto yoyote kama ambavyo watu wengi wanasema.

Wakati huo huo upande wa mwanafunzi mwingine, Mwahija Shaban alisema kitu kikubwa kinachomfanya ajitokeze uwanjani ni kuona Watanzania wenzake.

"Nimeanza kuja mazoezini kwasababu najiskia furaha kuzungumza lugha yangu, huku naweza nikakaa muda mrefu tunaongea lugha za watu tu," alisema.

Akizungumzia usalama alisema kuna muda iliwalazimu kurejea majumbani kwao baada ya kuwa na machafuko.

"Usalama sasa hivi ni mzuri lakini tuliwahi kufunga chuo miezi miwili na kurudishwa nyumbani, kwa wale waliobaki walikuwa chini ya ulinzi mzito chuoni," alisema.

Akizungumzia mchezo alisema wataipa sapoti Stars kwa kuishangilia muda wote.

Stars na Sudan zitacheza mchezo wao uwanja wa El Merreikh Omdurman saa 1:00 usiku kwa huku Sudan (saa 2:00 usiku kwa muda wa Tanzania) mchezo ambao Stars wanahitaji magoli mawili tu ili kusonga mbele.