Taifa Stars yatanguliwa Sudan

KIPINDI cha kwanza kimemalizika kwenye mechi ya marudiano kusaka nafasi ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) huku Taifa Stars ikiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Sudan.
Hata hivyo, kwa sura ya mchezo na kiwango kilichoonyeshwa bado Taifa Stars ina nafasi ya kupata mabao mawili kama safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Ditram Nchimbi, itatulia na kuzitumia vyema nafasi inazotengeneza.
Katika mchezo huo, Taifa Stars ilikianza kipindi cha kwanza kwa kasi huku ikionekana kuwa na kiu ya kupata mabao, lakini tatizo limeonekana kuwa kwa washambuliaji kutokana na kukosa mabao ya wazi.
Sudan ikiwatumia zaidi mawinga kusukuma mashambulizi yake huku ikisumbua zaidi upande wa beki Salum Kimenya, ilipata bao la kuongoza dakika ya 30 ya mchezo wakitumia makosa mabeki wa Stars kushindwa kuwa makini ndani ya eneo lao.
Hata hivyo, Kimenya alikuwa na changamoto kubwa kwenye upande wake kutokana na mawinga mawili wa Sudan kucheza zaidi upande wake.

Lakini, kwa upande wa Sudan safu yake ya ulinzi haikuwaruhusu Stars kuingia ndani ya eneo lake la hatari hivyo, kuwafanya Miraji Athuman, Nchimbi na Nado kutumia mbinu mbadala kusaka mabao.
Dakika 22 ya mchezo, Stars ilifanya shambulizi la piga nikupige langoni mwa Sudan, lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa bao.
Dakika 24 Domayo aligongeana vyema pasi za haraka na Mzamiru Yassin ambaye aliachia shuti kali lililokwenda juu ya lango.
Kutokana na ngome ya Sudan kuwa ngumu kuingilika, viungo wa Stars waliamua kupiga mashuti makali nje ya 18, lakini Sudan walikuwa makini kulinda lango.
Taifa Stars pia nusura ipate bao la kusawazisha, lakini Miraji alishindwa kuunganisha vyema mpira wa krosi uliopigwa upande wa kulia, ambapo alitakiwa kuunganisha tu kuzamisha wavuni lakini akaupiga vibaya na kurudi uwanjani.