Nchimbi, Kimenya waipangua Stars

Muktasari:

  • Lakini kikosi hiko kilichovaa bips jana ndio kilichotajwa kimya kimya katika Hotel ya Grand Villa hapa Sudan.

KAIMU kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amepanga kikosi cha uhakika kuhakikisha wanatoka na matokeo mazuri katika mchezo wa leo Ijumaa dhidi ya Sudan.
Katika kikosi hiko Ndayiragije amefuata kikosi kile kile alichopanga kwenye mazoezi yake ya mwisho waliyoyafanya jana usiku ambapo alikipangua kidogo kikosi kilichocheza na Sudan mchezo wa kwanza nchini Tanzania uliomalizika kwa Stars kufungwa 1-0.
Kikosi cha kwanza ambacho kilivaa bips kwenye mazoezi yake jana, kilikuwa na Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Bakari Mwamnyeto, Gadiel Michael, Salum Kimenya, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Frank Domayo, Idd Nado, Miraj Athuman na Ditram Nchimbi.
Kikosi cha pili kilikuwa na Oscar Masai, Dickson Job, Boniface Maganga, Abdulaziz Makame, Mudathir Yahya, Salum Abubakari, Hassan Dilunga, Shaban  Chilunda na Kelvin John.
Lakini kikosi hicho kilichovaa bips jana ndio kilichotajwa kimya kimya kwenye hoteli waliyofikia ya Grand Villa hapa Sudan.
Ingizo jipya katika kikosi hicho ni Nchimbi ambaye amechukua nafasi ya Ayoub Lyanga, beki wa kulia ameanza Kimenya akichukua nafasi ya Maganga, Mwamnyeto akichukua nafasi ya Kelvin Yondani ambaye ni majeruhi na Domayo aliyechukua nafasi ya Chilunda.