Tshabalala aachwa kambini Simba

Tuesday July 7 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN NA CLEZENCIA TRYPHONE

BEKI wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliachwa hotelini na basi la timu hiyo Jumamosi jioni walipokuwa wanakwenda Uwanja wa Nangwanda Sijaona kufanya mazoezi mepesi ya kujiandaa dhidi ya na Ndanda FC.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck aliwataka wachezaji wote kuwa ndani ya basi kabla ya saa 9:40 alasiri, na baada ya hapo wataanza safari ya kwenda katika uwanja wa mazoezi.

Tshabalala alitoka katika chumba chake ndani ya hoteli waliyofikia Simba na kufika katika basi saa 9:40, lakini Sven alikataa asifunguliwe mlango huku akiamrisha basi hilo liondoke na kumuacha nahodha huyo msaidizi nje akishangaa.

Taarifa ambazo Mwanaspoti lilizipata ni kuwa baadhi ya wachezaji walimwambia Tshabalala apande bodaboda awafuate, lakini alikataa na kurudi katika chumba chake kulala na hata kwenye mechi Sven alimtupa jukwaani.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema saa 9:40 ni muda uliopangwa basi kuondoka kambini kuwapeleka wachezaji mazoezini, lakini mpaka muda wa gari kuondoka mchezaji huyo alikuwa hajaingia.

Advertisement

“Kwanza muda wa basi kuondoka (kambini) ni saa 9:40 na sio muda wa kuingia katika basi, wachezaji wote wanajua hivyo, ambaye anakuwa hajaingia gari haliwezi kumsubiri yeye,” alisema.

“Simba inafanya mambo kwa taratibu, hivyo mchezaji akichelewa kwa sababu zake binafsi anatakiwa kutafuta namna ya kufika mazoezini kuungana na wenzake.

“Ukichwa na basi kwa kushindwa kufika kwa wakati unatakiwa kutafuta namna ya kuwafuata wenzako kwa gharama zako, ukifika walipo kwa maana ya kwenye uwanja wa mazoezi huwezi kuzuiwa kufanya mazoezi.”

Habari za ndani zinadai kwamba huenda Tshabalala akakatwa Sh300,000 kwenye mshahara wake kutokana na taratibu walizojiwekea mwanzo wa msimu juu ya uchelewaji na kila mchezaji anajua.

Advertisement