Tonombe: Nina kesi na Simba

Kuna staa mmoja tu ndani ya Yanga ambaye katika kundi la wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu ameuanza na moto mkali kiasi cha kukubalika haraka kwa kazi yake.

Nafasi anayocheza ni kiungo, lakini mpaka sasa jamaa ameshatupia mabao matatu huku uwezo wake ukiwa gumzo. Huyo ni Mukoko Tonombe.

Yanga ilimsajili kutoka AS Vita ya DR Congo ikimnunua kwa fedha za kutosha kuziba nafasi ya aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Papy Tshishimbi aliyegomewa kuongezwa mkataba mpya.

Jeuri ya Yanga kumuacha Tshishimbi ilianza baada ya kujihakikishia kumpata Tonombe.

Mwanaspoti lilimtafuta kiungo huyo raia wa DR Congo kujua mambo mbalimbali yanayohusiana na soka. Fuatilia hapa umjue Tonombe ni mtu wa aina gani.

Staa huyo anasema soka la Tanzania linatazamwa - lipo chini kuliko la DRC, lakini amejiunga na Yanga kwa kuwa anatamani kucheza Ulaya, hivyo kupitia Ligi Kuu Bara anaamini atafanikisha ndoto yake, “ndoto yangu kubwa ni kucheza Ulaya, lakini baada ya kuona kuna nafasi ya kuja kuichezea Yanga, nikaona ni fursa ya kuonyesha uwezo wangu ili kufikia kile ninachokitamani muda wote.”

“Kitendo cha kutoka nje ya Congo, kinanijenga kukutana na changamoto tofauti na zile ambazo nimezizoea katika ligi ya nchini kwetu, pia naamini ligi ya hapa inatazamwa sehemu mbalimbali, jambo linalonirahisishia kuonekana na mataifa tofauti,” anasema Mukoko na kusisitiza kwamba ana furaha kuwa ndani ya Yanga na ameshapata marafiki kibao.

TIMU YA TAIFA

Mukoko anasema alianza kuichezea timu ya taifa ya vijana ya U-23 nchini mwao, lakini baadaye alicheza iliyocheza michuano ya Chan, ila ile ambayo inakuwa na wachezaji ambao wanacheza Ulaya bado hajapata nafasi kutokana na wingi wa wachezaji waliopo nje ya Afrika. “Naona watu wengi wanajiuliza kwa nini sijaitwa Congo wanaamini soka la Tanzania lipo chini, lakini kocha aliniambia nenda kapambane anaamini nitapata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha taifa, hilo limenipa moyo wa kupambana zaidi ili niwe sehemu ya kikosi hicho,” anasema Mukoko.

“Akili yangu inawaza mambo ya soka tu, pia kauli ya kocha wa timu ya taifa imenipa morali ya kutaka kuonyesha kwamba licha yakuchukulia soka la Tanzania lipo chini kuliko Congo, uwezo wangu binafsi unibebe na hata kabla ya kutangaza kikosi alinipigia na kuniambia hatanijumuisha na nimemuelewa sababu alizonipa.”

Mukoko anasema Kocha Msaidizi wa DR Congo, Mwinyi Zahera anasema kwamba hawajamuita kutokana na hazina ya wachezaji walionao barani Ulaya.

KUMBE SIMBA WALIMTAKA

Anasema mabingwa wa soka, Simba, ndio waliokuwa wa kwanza kuhitaji saini yake, lakini baada ya kutokea ugonjwa wa corona meza ilipinduliwa na Yanga wakamuita faragha wakala wake.

“Ni kweli nilikuwa najua nakwenda kuichezea Simba, ndio klabu ya kwanza kuambiwa inanihitaji, binafsi nilianza kujiandaa kuja Simba na hata kujua mambo mbalimbali, lakini baadaye ikaja covid 19 mambo yakapungua kasi.

“Baadaye meneja wangu Nestor akaniambia mambo yamebadilika natakiwa kwenda Yanga, nilipoifuatilia nikaona nayo ni klabu kubwa tu, lakini niseme kitu nimefurahi jinsi Hersi Said anavyojua kumshawishi mchezaji alinipa heshima sana kuja kule na kuongea na mimi tofauti na Simba ambao nilikuwa nawasikia kwenye simu tu,” anasema.

JEZI ZA YANGA

Kuhusu jezi za Yanga, Mukoko anasema: “Sasa nina furaha sana hapa Yanga, unajua kuna wakati najiona kama bado nipo Vita angalia jezi ambazo Yanga inatumia ni kama za Vita, pia mashabiki wake wana upendo wanapenda mafanikio, haya ni mambo yamenipa imani kubwa, najiona kama bado nipo nyumbani tu ila nimehama nchi, hivyo nina furaha kwa sababu hata jezi wanazozitumia As Vita zimefanana na za Yanga. ”

SIMBA WANA KESI NAYE

Tono- mbe amefichua kwamba ana hasira kubwa na Simba hasa pale walipoitoa timu yake ya zamani, Vita kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika misimu miwili iliyopita.

Kesi hiyo inamfanya kusubiri kwa hamu mchezo baina ya timu hizo lakini pia kuhakikisha Yanga inatamba mbele ya watani zao hao. “Nakumbuka Simba ndio ilitufunga Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 2-1 hapa Tanzania, nakumbuka mechi hiyo sikucheza wala ile ya kule (DR Congo) lakini niliumia sana, sasa ni muda wangu sahihi kuondoa maumivu hayo, najua kuna siku nitakutana na Simba, tutakutana nao kwenye ligi lakini kikubwa nataka kuona Yanga inafanikiwa hapa na kuizidi Simba,” anasema.

AKIFUNGWA HALI

Staa huyu anaumizwa sana pale inapotokea chama lake limepoteza matoke. “Nilichojiwekea katika maisha yangu, timu iliyotufunga inanipa uchungu wa kujituma ili tukirudiana nahakikisha tunaifunga, hata kama nisingecheza Yanga niliamini ipo siku tutakutana na Simba Ligi ya Mabingwa Afrika nitawafunga, lakini ashukuriwe Mungu ninakutana nao kwenye ligi yao, lakini kikubwa sipendi kupoteza mechi nikifungwa naweza hata kukosa kula, huwa naumia sana,” anasema.

UWEZO BINAFSI UTAMBEBA

Mchezaji huyo anasema kabla ya kuitegemea klabu imbebe, kwanza anaamini katika kazi yake popote anapoajiriwa ni lazima aonyeshe uwezo binafsi ambao utakuwa na manufaa kwa timu yake, ndipo mengine yafuate kama kupendwa na mashabiki.

“Naamini katika bidii, si mchezaji wa kutegemea timu kwamba kwa sababu kubwa ndio nibweteke, kwa sababu nitakuwa nimepata mteremko wa umaarufu, nilisajiliwa Yanga ili kwa huduma yangu kusaidiana na wachezaji wenzangu tuweze kuziweka ndoto zenye fikra katika matendo, ndicho kinachosubiriwa na mashabiki wetu,” anasema Mukoko.

YANGA INANYAKUA TAJI

Mukoko anawahakikishia mashabiki wa Yanga kuwa huu ni mwaka wao, na lazima ndoo itue pale Jangwani. “Yanga ikiwa na muunganiko mzuri haitakuwa inafunga bao moja moja kama sasa hivi, naamini katika mechi moja tutakuwa tunavuna mabao ya kutosha na hiyo ndiyo thamani ya klabu ya Yanga.”

“Kikosi cha Yanga ni kizuri sana, kikubwa uvumilivu unatakiwa kwani hiki ni kipindi ambacho wachezaji tunajuana, tunahitaji muunganiko, likitimia hilo hakuna timu ambayo itakuwa salama mbele yetu, hivyo inawezekana kabisa kuchukua ubingwa - tena kwa kufunga mabao mengi kwa kila mechi,” anasema.

DENI KWA MASHABIKI

Akizungumzia mapokezi yaliyofanyika kwake na winga Tuisila Kisinda wakati anatua Yanga, anaona kuna deni kubwa kwake kuhakikisha anawalipa mashabiki hao kupitia mguu wake uwanjani. “Kila nikifikiria umati wa mashabiki wa Yanga uliotufuata uwanja wa ndege na bosi Hersi anabebwa kifalme, kwanza nilishtuka sana lakini ilinifungua macho kujua ukubwa wa kazi ambayo ipo mbele yetu na jinsi ambavyo Tanzania wanapenda soka.”

Anasema: “Najiona nina deni kubwa kwa mashabiki wa Yanga la kuhahakikisha nafanya zaidi ya kile wanachokitarajia kutoka kwangu, kikubwa namuomba Mungu anipe afya ili kutimiza kile ninachokitamani kukifanya kwa msimu huu.”

njooni UWANJANI

Mchezaji huyo anawaita mashabiki wa Yanga wasikose uwanjani kila timu yao inapokuwa na mechi.

“Nikiona mashabiki wengi wanakuja uwanjani, huwa inanipa changamoto ya kuthamini muda wanaojitoa kuja kutuunga mkono, nimejiunga na Yanga ambayo siku ya kwanza tu niliona wafuasi wapo wengi sana,” anasema.

“Hilo limeniongezea umakini wa kazi zangu, ndio maana mnaona kila wakati nawahimiza wenzangu kufanya kazi kwa nguvu, haifurahishi mashabiki waache kazi zao waje kutuangalia uwanjani halafu waondoke na huzuni.”

hataki kuVURUGwa

Kitu ambacho anatamani mashabiki wa Yanga wakijue ni kwamba bado wachezaji hawajawa na muunganiko mzuri, hivyo wawavumilie na siyo kuanza kuwakatisha tamaa.

“Kuna wakati mchezaji anaweza akashuka kiwango, hivyo (mashabiki) wanatakiwa kumtia moyo na siyo kuanza kumsema vibaya ama kumzomea,” anasema.

“Tabia hiyo inaweza kumtoa kwenye mstari na itakuwa ndio mwisho wa ndoto zetu, utakuta wengine wanakwambia mbona As Vita alikuwa anacheza vizuri imekuwaje anashindwa kuonyesha uwezo, jibu la hilo waishi vizuri na sisi kwenye mpira huwezi kuwa juu kila wakati hili linatokea hata Ulaya nitafurahi kama kuna wakati wachezaji tutavumuliwa.”

AKICHEZA NAMBA 6

Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic katika mechi yao na Mtibwa Sugar waliyoshinda bao 1-0, alimpanga kucheza namba 10, lakini yeye anasema anajisikia vizuri kucheza namba sita.

“Ujue kuna wakati alikuwa anatoa maelekezo nilikuwa sielewani naye, kwa sababu natumia lugha ya Kilingala na Kifaransa, kocha anazungumza Kingereza, hivyo kuna wakati nilikuwa nashindwa kuelewa nini ananielekeza,” anasema Mukoko.

“Napenda kucheza namba sita kwa sababu nakuwa nashambulia na kukaba, lakini mwisho wa siku natakiwa kufanya kazi, kocha ana uamuzi wa kunipanga kokote anakotaka labda ameona kitu cha tofauti kwangu ambacho anaona kina faida na timu kwa wakati huo,” anasema Mukoko