Prime
Walibya wampandia dau Aziz KI

LILE dili la kiungo mshambuliaji Stephane Aziz KI pale Wydad Athletic limeingia mdudu baada ya kocha wa timu hiyo kutaka akatwe na akikatwa anarejea Yanga, lakini kuna jipya limeibuka juu ya nyota huyo raia wa Burkina Faso.
Aziz aliyeondoka Yanga hivi karibuni kwenda kujiunga na Wydad na kuungana na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Seleman Mwalimu 'Gomes' na kupata nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa Klabu 2025 na kushuhudiwa timu hiyo ikitolewa hatua ya makundi bila kupata ushindi.
Sasa unambiwa, wakati Aziz KI akisubiri uamuzi wa mwisho wa mabosi wa Wydad wakati akiwa kwao Ivory Coast, kuna Waarabu wengine wamepigia hodi Yanga wakiongeza dau la kutaka kumbeba juu kwa juu.
Klabu ya Al Ahli Tripoli umepiga simu haraka Yanga, ikisema kama Wydad ikimkataa kiungo huyo basi wajulishwe haraka ili wamsajili, kwani wanamhitaji.
Ahli iliwahi kutuma ofa Yanga juu ya Aziz KI, lakini Wydad ikawahi kuweka fedha ndefu kisha kumshawishi msimamizi wa mchezaji huyo kwamba atashiriki Fainali za Kombe la Dunia la Klabu.
Katika dili la Wydad, klabu ya Yanga ilipewa kiasi cha dola 350,000 kama malipo ya awali kumwezesha kiungo huyo kucheza fainali hizo zinazoendelea Marekani, huku kocha wa timu hiyo Amine Benhachem akiwa anapima ubora wake.
Benhachem, raia wa Morocco amekataa kumpa muda zaidi Aziz KI wakati mabosi wa timu yake wakimpa mtihani wa kukata jina moja katika orodha ya wachezaji wa kigeni alionao kikosini.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Tripoli wameshajulishwa watume rasmi ofa ya kimaandishi kumnunua Aziz KI.
Ingawa mabosi wa Yanga wanafanya siri, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba Tripoli ipo tayari kutoa dola 1.5 Milioni kumpata kiungo ambaye msimu uliopita alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 21, wakati kwa ligi iliyomalizika hivi karibuni alifunga mabao tisa.