Prime
Musonda avunja ukimya Yanga

HAKUNA ubishi kwamba maisha ya mshambuliaji wa Kennedy Musonda ndani ya Yanga yamefikia tamati baada ya kuitumikia timu hiyo kwa misimu miwili na nusu, lakini mwenyewe ameamua kuvunja ukimya kwa kuzungumza kwa mara ya kwanza na Mwanaspoti.
Nyota huyo wa kimataifa wa Zambia, alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la msimu wa 2022-2023 akitokea Power Dynamos amemaliza mkataba wa kuitumikia timu hiyo tangu Juni 30 mwaka huu, ikielezwa mabosi wa klabu hiyo ni kama wamemchunia kutaka kumuongezea.
Hata hivyo, Musonda amefunguka kwa kusema ameikamilisha kazi aliyopewa ndani ya kikosi hicho na sasa yupo huru kutafuta changamoto nyingine baada ya uongozi wa timu hiyo kutomuita mezani kwa ajili ya mazungumzo mapya.
Msambuliaji huyo ameiotumikia Yanga kwa mkataba wa miaka miwili na nusu amefunga mabao 34 na kutoa asisti 13 akitwaa mataji matatu ya ligi na FA matatu na ngao za jamii mbili.
Akizungumza na Mwanaspoti, alisema amemalizana na Yanga baada ya kumaliza mkataba wake na hakuna mazungumzo mengine kwaajili ya kusaini mkataba mpya hivyo yupo tayari kujaribu changamoto nyingine kwa timu yoyote ambayo itaonyesha nia ya kumtaka.
"Mkataba wangu na Yanga umeisha na hakuna mazungumzo yoyote ya kusaini mkataba mpya hivyo ni wazi mimi sio mchezaji wa timu hiyo," alisema na kuongeza;
"Nilikuwa na misimu miwili na nusu mizuri kwa sababu nimeweza kutwaa mataji matatu ya ligi, FA na ngao mbili sio jambo dogo kwangu ni mafanikio makubwa nikivaa na medali moja ya CAF baada ya kucheza hatua ya fainali."
Alipoulizwa juu ya ofa alizozipokea hadi sasa baada ya kuwa nje ya uwanja kutokana na kumaliza mkataba na Yanga alisema hawezi kuzungumzia masuala ya ofa atazungumza atakapofikia makubaliano ya kusaini mkataba na moja ya timu zilizompa ofa ya mazungumzo.
"Mimi ni mchezaji na mpira ndio kazi yangu hivyo klitu chochote kikikamilika kwa ajili yangu juu ya msimu ujao ntacheza wapi utafahamu kwa sababu mchezo ninaoucheza ni wa wazi na umekuwa ukizungumzwa sana sijajua kama nitaendelea kusalia ligi kuu au nitajaribu changamoto nyingine nje ya Tanzania lakini ofa zipo."
Musonda akiwa na Yanga amepata nafasi ya kucheza na washambuliaji mbalimbali ambao walishaondoka ikiwa ni pamoja na Fiston Mayele, Jean Baleke ambao hawapotena Yanga wengine ni Clement Mzize na Prince Dube.
Kuthibitisha kwake kuwa hatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu ujao ni wazi kuwa amekuwa mchezaji wa kwanza kujiweka kando ikiwa timu hiyo bado haijaanza kutoa taarifa za 'Thanks You'.