Simon Msuva kusalia Iraq

Muktasari:
- Kiwango bora alichoonyesha Msuva akiisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya nne kwenye mechi 38 za Ligi Kuu, ikishinda 18 sare tisa na kupoteza 11 kwa mabao yake 12 aliyofunga kimewashawishi viongozi wa timu hiyo kuendelea naye.
HUENDA mshambuliaji wa Kitanzania na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Somon Msuva akasalia kwenye kikosi cha Al Talaba msimu ujao.
Kiwango bora alichoonyesha Msuva akiisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya nne kwenye mechi 38 za Ligi Kuu, ikishinda 18 sare tisa na kupoteza 11 kwa mabao yake 12 aliyofunga kimewashawishi viongozi wa timu hiyo kuendelea naye.
Nyota huyo wa zamani wa Wydad AC mkataba na klabu hiyo ulikuwa umeisha mwishoni mwa msimu huu na tayari timu imetoa ofa nono kwa Msuva.
Taarifa tulizozipata ni kuwa klabu imeshatoa ofa kilichobaki ni kwa mchezaji kama atakubaliana na dili hilo ama la.
“Wiki iliyopita alisafiri kwenda Iraq kuna vitu vyake alikwenda kukamilisha ikiwemo hilo la kuongeza mkataba nafikiri huenda akabaki kwani wamemuwekea dili kubwa,” kilisema chanzo.
Mbali na Wydad na Talaba, Msuva alizichezea klabu kama Yanga msimu 2012/17, Difaa El Jadida ya Morocco (2017/20) alicheza mechi 80 na kufunga mabao 28, Al Qadsiah (2022/23) alifunga mabao manane kwenye mechi 28, JS Kabylie (Algeria) 2023 na Al Najma ya Saudia 2024.