Sven atema nyota sita kikosini

Muktasari:

Simba itacheza na Tanzania Prisons baada ya kukaa kwa zaidi ya wiki mbili bila mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Sven Vanderbroeck amewatema nyota sita katika kikosi kitakachosafiri kuifuata Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu utakaofanyika Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.
Mara baada ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege, Sven aliwapa wachezaji wake mapumziko ya siku moja, na jana usiku waliripoti kambini kwa ajili ya kuanza safari ya Rukwa.
Sven alisema kwa kuwa wanakwenda kucheza mechi moja, atasafiri na wachezaji 22, huku wengine sita wakishindwa kuwa miongoni mwao kwa sababu mbalimbali.
“Kuna baadhi ya wachezaji kati ya hao sita hawapo nchini, kuna wanaoumwa na wengine matatizo ya kifamilia,” alisema Sven.

Miongoni mwa wachezaji ambao wameachwa katika msafara huo ni Clatous Chama na Pascal Wawa ambao kila mmoja yupo nchini kwao akifatilia hati mpya ya kusafiria.

Wengine John Bocco, Ibrahim Ame na Fraga, ambao wote inaelezwa wapo na majeruhi.

Mechi za ugenini ngumu

Katika hatua nyingine Sven, ameelezea ugumu ambao watakwenda kukutana nao katika mechi ya Tanzania Prison pamoja na nyingine ambazo wanacheza kwenye viwanja vya ugenini.

Sven alisema mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mlandege ilikuwa yenye faida kwao kuelekea katika mechi za ligi kwani wapinzani walitoa ushindani wa kutosha kama ambavyo alikuwa anahitaji.

“Tunaenda kucheza mechi ngumu dhidi ya Tanzania Prison ambao hata mazingira ya Uwanja wa Nelson mandelea utakuwa unatubana tofauti na ambavyo tutacheza Dar es Salaam,” alisema.

“Kila mechi ambayo tunakwenda kucheza ugenini ni ngumu si Prison tu hata tukikutana na Mbeya City, Ihefu na nyinginezo ambacho tutakifanya ni kuongeza motisha kwa wachezaji zaidi ya asilimia 200, ili tufanye vizuri,” alisema.

“Kukosekana kwa wachezaji hao wengine katika mechi na Prison wala si tatizo kwetu kwani Simba inawachezaji wengi ambao wanaweza kucheza na wakafanya vizuri.
“Kikubwa tunaendelea na maandalizi yetu ya mwisho kabla ya mechi na kubwa ambalo tunahitaji ni kupata pointi tatu kama ilivyokuwa katika michezo iliyopita,” alisema Sven.

Simba, Azam wakutana
Katika hatua nyingine kikosi cha Simba na Azam watakutana Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julias Nyerere na kusafiri kwa ndege moja.

Simba na Azam bila kujua wote wataondoka leo Jumatatu saa 12:30 asubuhi na shirika la ndege la Precision Airways wote kuelekea Mbeya.

Simba mara baada ya kufika Uwanja wa ndege wa Mbeya Songwe watatumia gari kufika Rukwa kuwafuata Tanzania Prison wakati Azam watabaki mkoani humo kuwakabiri Ihefu.
Mratibu wa Simba, Abasi Selemani alisema wao wataondoka Jumatatu saa 12:30 asubuhi kwenda Mbeya na watachukua usafiri mwingine wa gari ili kufika Rukwa na huenda jioni wakafanya mazoezi awamu moja.

“Taratibu zote za kusafiri zipo tayari kama ambavyo tulikuwa tumepanga,” alisema Selemani.
Ofisa habari wa Azam, Thabit Zakaria alisema wanaondoka Jumatatu asubuhi kuelekea Mbeya kuwakabiri Ihefu.

“Tunaenda kucheza mechi ngumu kutokana na wapinzani kutokuonekana kuanza vizuri msimu huu na wanaweza Kutoka kuinuka kuanzia kwetu,” alisema Zakaria.