Simba, kituo kinachofuata ni CAF, pandisha abiria

Tuesday July 7 2020

 

By Edo Kumwembe

SIJAIELEWA vema Simba hii. Wakati mwingine najiuliza Simba hii ni bora kuliko ile ya msimu uliopita? Jibu lake ni gumu kiasi. Kwanini? Kwa sababu wametwaa tena ubingwa kwa tofauti ya pointi nyingi. Na wamefungwa mabao machache.

Ukianza kuangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja unajiuliza kama watafika katika kituo kinachofuata. Michuano ya ya CAF. Wanahitaji kuongeza mastaa wengine. Subiri kidogo tujadiliane. Nadhani inabidi waupuuzee ubingwa huu na kuanza kujipanga kivingine.

Kutwaa ubingwa wa Ligi kuu ni kitu tofauti na kufanya vizuri michuano ya CAF. Simba wamejiwekea viwango gani? tujiulize. Meddie Kagere ni yule yule wa msimu uliopita? Wengine tunaona tofauti ingawa namba zinatusuta.

Kagere ndiye mfungaji bora mpaka sasa ana mabao 19. Kuna uwezekano mkubwa akamaliza kuwa mfungaji bora. Hata hivyo macho yetu yanatuambia kitu tofauti. Kwamba Kagere huyu amepungua kidogo tofauti na msimu uliopita.

Mpaka sasa kocha wake anamtumia zaidi John Bocco kama mshambuliaji mmoja pale mbele. Wakati msimu unaanza alikuwa anamtumia mshambuliaji mmoja. Baadaye mashabiki wakalalamika. Akaanza kuwatumia wote wawili na timu ikafanya vizuri.

Kwa sasa kocha amerudi katika mfumo wake na kumtumia mshambuliaji mmoja. Mshambuliaji mwenyewe ni Bocco na sio Meddie Kagere. Miezi 24 iliyopita ungewauliza Simba nani aanze katika nafasi moja pale mbele ungesema Kagere. Sasa hivi anaanza Bocco na wanaridhika. Kumbe inawezekana hata Simba wenyewe wanajua kwamba Kagere ameshuka licha ya kuongoza kwa kufunga mabao mengi.

Advertisement

Hii ina maana kwamba Simba wanahitaji mshambuliaji mwingine wa nguvu. Mshambuliaji huyo anapatikana nchini? Sidhani. Kama angekuwa anapatikana nchini basi Kagere asingekuwa anaongoza kwa kufunga mabao mengi licha ya kuanza kukalia benchi Simba.

Linakuja swali jingine kuhusu wale walinzi wa kati, Serge Wawa na kipa wao, Erasto Nyoni. Hawa wawili wa kati wanaonekana kuzidiwa na umri. Siamini katika umri. Naamini katika kiwango. Lakini linapokuja suala la kasi basi Wawa na Nyoni inaoenekana kama vile umri unawatupa mkono.

Hapo hapo kumbuka kipa wao, Aishi Manula kuna wakati alishutumiwa sana na mashabiki wa klabu hiyo kwa kutokuwa makini. Lawama zilizidi katika pambano dhidi ya Yanga raundi ya kwanza baada ya kuruhusu bao la Mapinduzi Balama.

Unajiuliza, Nyoni na Wawa umri umekwenda. Aishi naye anashutumiwa langoni. Kwanini sasa Simba imeruhusu mabao machache msimu huu? Hapa ama mashabiki na viongozi wajidanganye kwamba timu yao ni imara au wapinzani ni dhaifu sana.

Advertisement