Simba wapewa neno usajili uzingatie kimataifa

Muktasari:

Simba imeshauriwa kuweka umakini kwenye usajili wao, kuhakikisha inapata wachezaji wenye uwezo wa kushindana kimataifa, kutokana na majukumu yaliopo mbele yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Dar es Salaam. Simba inaendelea na harakati za usajili, staa wa zamani wa timu hiyo, Zamoyoni Mogella ameshauri viongozi na benchi la ufundi kufanya usajili kwa wachezaji wenye uwezo wa kushindana kimataifa.

Mogella alisema Simba mwaka huu ina majukumu mazito ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo wanalopaswa kuliweka akilini wanapofanya usajili wa wachezaji.

Mogella alisema wachezaji wanaokuwa kuongeza nguvu wawe na uwezo kuliko wale ambao walikuwa na timu msimu uliopita.

"Kama msimu ulioisha walimaliza hatua ya robo fainali katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, basi mwaka huu wanapaswa wawe na mtazamo wa mbali wa kufika fainali.

"Wachezaji wazuri wanaonekana na wala sio wa kificho,  hivyo viongozi wa Simba lazima wawe wanapiga mahesabu ya kutamani mafanikio zaidi ya hayo walionayo kwa sasa," alisema Mogella.