Simba yaibeba Tanzania kimataifa

Muktasari:

  •  Jumla ya nchi 12 zenye idadi kubwa ya pointi ambazo hutolewa kulingana na ushiriki wa klabu zake kwenye mashindano ya klabu Afrika, hupata nafasi ya kuingiza idadi ya timu nne kwenye msimu mmoja wa mashindano hayo ambapo mbili hushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili hushiriki Kombe la Shirikisho.

Dar es Salaam.Simba inaelekea kutimiza ndoto ya Tanzania kuingiza idadi ya timu mbili katika mashindano ya kimataifa baada ya kufuzu hatua ya robo fainali kuiweka Tanzania kwenya nafasi nzuri ya kuingiza idadi hiyo ya timu kwenye msimu wa 2020/2021.

Kwa ushindi wa juzi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita ambao Simba iliupata, umeifanya ipate pointi tatu ambazo katika msimu huo wa 2020/2021 zitazidishwa kwa alama tano ambazo ni kiashirio cha miaka mitano ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ambacho hutumika kupiga hesabu ya idadi ya pointi ambazo nchi husika inakuwa nazo katika kuamua idadi ya timu zitakazoiwakilisha kimataifa.

Kwa vile Simba wanashiriki mwaka huu, pointi walizovuna hadi sasa zitaanza kuhesabiwa kwenye msimu huo wa 2020/2021 na sio msimu ujao ambapo zikidishwa kwa tano, idadi ya pointi zitakuwa ni 15, lakini zitajumuishwa na pointi tatu zitokanazo na ushiriki wa Yanga kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2016 na 2018 kuifanya Tanzania ifikishe alama 18.

Alama hizo 18 hadi sasa zimeshaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 12 zenye idadi kubwa ya pointi ambazo msimu wa 2020/2021 zitalazimika kuingiza timu.

Hata hivyo bado Tanzania itapaswa kuiombea dua mbaya timu ya Gor Mahia kutoka Kenya iliyofuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ishindwe kupenya na kuingia hatua ya nusu fainali kwani vinginevyo inaweza kupoka nafasi hiyo.

Kenya yenye pointi 14, itafikisha pointi 19 ambazo zitakuwa ni moja zaidi ya zile za Tanzania ikiwa Gor Mahia itaingia nusu fainali ya mashindano hayo msimu huu.

Uhakika zaidi kwa Tanzania utakuwepo ikiwa Simba itafanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Afrika kwani itafikisha pointi 23 zitaiacha Kenya kwa alama nne.