Nyota watano Yanga wapewa wiki 2 tu

UONGOZI wa Yanga umejiridhisha na uwezo wa mastaa wao watano wapya wa kigeni na kusisitiza wakiimarika ndani ya siku 20 zijazo timu zitaumia.

Mwenyekiti wa Yanga ambaye pia kitaaluma ni Kocha, Daktari wa falsafa, Mshindo Msolla amesema usajili wao msimu huu uko vizuri.

Msolla alisema katika wachezaji wao watano wa kigeni hakuna mtu mwenye mashaka na vifaa hivyo kwani pesa zilizotumiwa na wadhamini wao GSM zimekwenda kihalali.

“Usajili huu ni mkubwa sana na kiukweli tangu niingie ndani ya uongozi safari hii naweza kusema tuna kikosi ambacho kitarudisha heshima yetu,” alisema Msolla ambaye ni Kocha wa zamani wa Taifa Stars na Reli ya Morogoro.

“Tuanze kwa kuangalia hawa wachezaji wa kigeni tumewaona katika mechi yao ya kwanza hawa waliocheza tu utaona kwamba walistahili kusajiliwa ni wachezaji wenye ubora mkubwa, pia wanakiu wakijua wanadeni kubwa katika klabu,” alisema Msolla.

Yanga msimu huu imewasajili washambuliaji Tuisila Kisinda, Yacouba Sogne, Michael Sarpong, viungo Mukoko Tonombe, Carlos Fernandez ‘Carlinhos’.

Kuhusu wachezaji wazawa waliosajiliwa alisema nao wamethibitisha ubora wao na kwa ambao hawakupata nafasi ya kuanza wanatakiwa kutambua hiyo ni hatua ya upana wa kikosi na wana nafasi ya kuzidisha mapambano.

“Hawa wazawa nao waliocheza watu wamewaona wana ubora mkubwa, tunajua wapo waliocheza mchezo wa kwanza lakini pia wapo ambao hawakupata nafasi lakini wote ni bora, ambao hawakupata nafasi katika mchezo uliopita huu sio wakati wa kujiona wanyonge wanatakiwa kuzidisha juhudi mazoezini ili siku makocha wakiona wanaongezeka ubora watapata nafasi.

“Unajua hiyo ndio faida ya kuwa na upana wa kikosi yoyote ana nafasi ya kucheza muhimu ni juhudi zako kwenye mazoezi mpaka kwenye mechi siku ukipata nafasi. Ukiwachukua hawa wapya sasa ukawaunganisha na hawa waliowakuta utagundua msimu huu tuna timu bora sana.

“Niwashukuru wadhamini wetu GSM kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kusimamia usajili wakishirikiana na uongozi na hatimaye sasa tunaona mwanga,” alisema

“Tumepata makocha wazuri lakini wanakutana na kikosi ambacho kama ni kipya tu na bahati mbaya walichelewa kukutana mapema. Wakati huu niwaombe wenzangu tutoe nafasi kwa makocha na wachezaji kukaa pamoja na kazi ya kutengeneza timu ifanyike, huu sio wakati wa kuanza kuwalaumu wachezaji ni mapema mno.

“Nimemsikia kocha anasema anahitaji siku 10 mpaka 15 nafikiri tuwape muda zaidi tusianze kuwaondoa mchezoni wachezaji wetu mapema katika utulivu wa kuipa timu yetu ushindi.