Nyika afungukia kuipiga Yanga-6

Muktasari:

Leo katika kuhitimisha, Nyika anafunguka kuhusutuhuma kwamba walikuwa wakipiga fedha Yanga, huku akifungukia ishu nzima ya usajili wa Heritier Makambo. Tiririka naye...!

TANGU mapema wiki iliyopita tumekuwa na mfululizo wa makala za aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, Hussein Nyika akifunguka mambo kadhaa tangu aingie madarakani.

Jana Jumapili tuliona jamaa alivyofunguka sababu ya kusajili kwa Ibrahim Ajibu miaka miwili iliyopita akidai ili ni kisasi cha kunyakuliwa kwa kiungo wao fundi kipindi hicho, Haruna Niyonzima.

Leo katika kuhitimisha, Nyika anafunguka kuhusutuhuma kwamba walikuwa wakipiga fedha Yanga, huku akifungukia ishu nzima ya usajili wa Heritier Makambo. Tiririka naye...!

KASHFA YA KUPIGA PESA

Wakati Nyika akimalizia uongozi wake, moja ya tuhuma zilizoelekezwa kwa kamati yao ni kwamba ilikuwa inapiga pesa za usajili. Hapa anafunguka kila kitu.

“Ni kweli hizo kelele zilikuwa nyingi, unajua huwezi kuwazuia binadamu hasa watu wa sasa kuzungumza, dunia imekuwa kama kijiji kupitia teknolojia. Mtu ananunua kifurushi cha Sh 500 tu anatumia kuchafua watu na sio kutafuta maendeleo ya maisha yake. Ukishakuwa kiongozi unatakiwa kujiandaa na mazuri na mabaya na bado nitaendelea kuwashukuru watangulizi wangu Abdallah BinKleb, Seif Magari, Mhandisi Isaac Chanji ambao walishaniandaa katika hayo.

“Yanga haikuwa na fedha ambazo unaweza kuiba, klabu haina fedha sisi ndiyo tuliokuwa tunaisitiri klabu kwa kusajili kuhangaika na mpaka tunataka kupigwa ngumi ili tu tusajili wachezaji halafu mtu anakuja kukwambia unaiba.

“Wakati wa kamati yangu, katika kusajili hakukuwa na muda hata wa saa moja kukaa na fedha za usajili, nafikiri nimekuelezea vizuri, tulikuwa tunamwita mchezaji mezani na sote tunachangishana huku mwenyewe akiona mpaka fedha zinakamilika. Hapo labda nikuulize wewe unaibaje? Kumbuka hapo klabu haijatoa hata Sh 100.”

Ukija katika klabu mimi sikuwa mweka saini kutoa fedha za Yanga. Yanga ilikosa mwenyekiti lakini ilikuwa na makamu, katibu na hata mhasibu hebu niambie Nyika anaiba wapi?” anahoji na kuongeza;

“Sikuwa nasumbuka na hilo siku zote nilipokuwa nasikia kelele hizo nilipuuza na kuendelea kufanya kazi. Nilikuja kugundua pia kuna baadhi ya viongozi wenzangu katika kamati ya utendaji ndio waliokuwa wako nyuma ya kashfa hii ili tu kunichafua zingeniumiza kama Sanga (Clement) au makamu wangu wakati huo marehemu Mustafa Urungo angesema nafanya uchafu, lakini kwa kuwa yalikuwa maneno ya watu wasiojua niliwasamehe na wengine walikuwa wanakuja kuniomba samahani na mpaka sasa wapo ambao wanakuja kuniomba radhi.”

MAFANIKIO YA KAMATI YAKE

“Nikiwa kama mwenyekiti wa kamati ya mashindano hatukufanikiwa kuchukua ubingwa wowote hapa ndani labda niseme kushika nafasi ya pili msimu uliopita pengine ni mafanikio kwa maana nafasi hiyo, ndiyo inaifanya Yanga sasa kuwa katika mashindano ya Afrika,” anasema na kuongeza;

“Pengine bila juhudi zetu kwa kuamua kuteseka na kutokukubali kirahisi kuhujumiwa leo Yanga isingekuwa katika ramani hii ya sasa. Mafanikio makubwa zaidi ilikuwa ni kuingia hatua ya makundi baada ya kuwang’oa Welaiyta Dicha ya Ethiopia. Nakumbuka yalikuwa ni mapambano makubwa kwa mchezo ule wa ugenini baada ya ushindi wa nyumbani wa 2-0, nawashukuru makocha wa wakati huo na wachezaji.”

“Tulifika Ethiopia na kukuta maandalizi makubwa ya wapinzani wetu. Tukaambiwa hapa kuna mpango mkubwa kama nchi kuhakikisha tunafungwa na kutolewa,” anasema.

“Nakumbuka kiongozi aliyetangulia na timu alikuwa Hamad Islam. Alipambana sana na hujuma baadaye tukaongezeka na kufanya kikao kizito, sisi kwanza kisha tukakutana na wachezaji ambao tuliwaambia uongozi tunataka kuona timu inafuzu na wao wanataka nini? Akasimama Kamusoko (Thabani) akasema wao wanachotaka katika fedha za kuingia makundi tuwape kama zawadi Sh 100 milioni,” anaongeza.

“Tukawasiliana na Sanga akakubali. Wachezaji wakahamasika wakapambana sana ingawa mpaka mapumziko tulikuwa nyuma kwa bao 1-0, kipindi cha pili wakaomba waongee wao wenyewe na baadaye Kocha Mwandila (Noel) na Nsajigwa (Shadrack) wakaongea yao, nasi tukawasisitiza. Hatimaye matokeo yalibaki yalivyo na kufuzu.”

ISHU YA USAJILI

“Ukija katika upande wa usajili, nakumbuka wakati tunamleta Makambo (Heritier) kuna baadhi ya wajumbe na hata mashabiki wakambeza sana wakisema tumemleta mchezaji mwanamuziki na wengine wakasema wamefuatilia anatoka ligi ya chini kule Congo,” anasema Nyika na kuongeza;

“Hatukuzingatia hayo makelele, Makambo kila mtu aliona alichofanya katika mwaka mmoja tu ndani ya Yanga na akauzwa na kuingizia fedha klabu na nimeona sasa anakumbukwa. Hali kadhalika kamati yangu ndio ilimsajili Ninja (Abdallah Shaibu) walimuona hana lolote, ila nafarijika kumuona Marekani anacheza na wachezaji wakubwaduniani pia kuna Maka Edward ambaye alikuwa haonekani kama mchezaji na kuna wakati kuna watu walitaka aondolewe sasa yuko Morocco na taarifa nilizonazo muda si mrefu atakuja kulisaidia taifa.”

“Hayo ndiyo mafanikio ninayoweza kusema tuliyapata huku tukipewa kashfa nyingi. Kama tungekuwa na nguvu ya fedha naamini hata ubingwa ungekuwa wetu na kupata mafanikio makubwa zaidi. Tulijua kikosi chetu kilikuwa chembamba lakini umoja wetu na mshikamano wa wanachama ulitusaidia.”

UONGOZI MPYA YANGA

“Kwanza niwapongeze viongozi wapya, ni mara ya kwanza kuwazungumzia, unajua uongozi wetu ulikuwa na changamoto kwa kutokuwa timilifu kwa maana ya kolamu lakini sasa wenzetu wamekamilika, nafikiri wameanza vizuri wanatakiwa kushikamana zaidi na wajitume kwa nguvu sisi wanachama tutawapa nguvu.”

Nyika alipoulizwa madai kwamba amejiweka mbali na uongozi wa sasa wa Yanga, naye alijibu hivi;

“Ndio kama pale nilipokwambia kwamba kuna watu kazi yao ni kutengeneza mambo ya uongo. sijui lengo lao linakuwaga lipi? Si kweli nimejitenga na uongozi. Tunashirikiana sana, asiyeamini amuulize Makamu Mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela anajua ukweli sifanyi mambo kumuonyesha mtu lakini nafanya mambo kwa utashi wa kile ninachokipenda.”

“Kuna muda mrefu sikuwepo nchini nilikuwa nje ya nchi kwa mambo yangu binafsi na tulikuwa tunawasiliana nao tunashauriana vyema na hata sasa nimerudi tunaendeleza mshikamano,” anasisitiza.

TOFAUTI YANGA YA SASA, ZAMANI

“Kuna tofauti kama tatu tu, kwanza uongozi uliopita ulikuwa haujakamilika lakini wenzetu wakiingia katika vikao wanakuwa wamekamilika, tofauti ya pili ni nguvu ya fedha, sisi tuliyumba sana kutokana na kukosa fedha, wenzetu kidogo changamoto ya fedha imekimbia kuna neema na tofauti ya tatu ni kikosi kile chetu kilikuwa ni kikosi cha umasikini ila sasa Wanayanga wameijenga timu yao.”

Juu ya kitu gani ambacho uongozi wa Yanga ufanye ili kuwasaidia, Nyika anasema; “Muhimu ni mshikamano na ukweli. Uongozi unatakiwa kuendelea kuwaunganisha

Wanayanga hawatakiwi kuchoka, wanapaswa kuwatafuta watu waliopita na kuendelea kushikamana nao wakiona inafaa Yanga ni ya wengi.”

Anaongeza; “Pia wanaowasaidia viongozi wetu wanapaswa kuwa wakweli na nia yao ya dhati inatakiwa kwanza kuisaidia timu ipate mafanikio na sio kutanguliza matumbo yao, watu wasiende kwa Mwenyekiti (Dk Mshindo Msolla) au kwa viongozi wengine na kuwapotosha kwamba usishirikiane na flani hapo tutakuwa tunampotosha naye anatakiwa kuwaepuka watu wa namna hiyo.”

ASILOSAHAU ENZI ZAO?

“Tukio nisilolisahau enzi za uongozi wetu ni lile la kaka yake Kelvin Yondani (Sunday) kutaka kunipiga ngumi (anacheka kidogo). Acha nicheke kwa sababu fedha bwana kweli inagombanisha watu, unajua mimi na kina Yondani ni wadogo zangu nimetoka nao Mwanza, ila maslahi yakatutofautisha, nashukuru tuliyamaliza na maisha yanaendelea.”

Juu ya usajili bomba msimu huu, Nyika anafunguka kwa kusema; “Usajili wote sioni kama una tatizo sana, bado tunatakiwa kuendelea kuamini mambo yatabadilika taratibu hii ni timu mpya, lakini nitoe shukrani sana kwa uongozi kwa kuweza kumleta (Farouk) Shikhalo naamini ni kipa atakayetusaidia sana, Lamine (Moro) ni beki mzuri sana ameanza vizuri.

“Mapinduzi Balama nakumbuka wakati tunacheza robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Alliance. Mechi ilipoisha niliongea na na (kocha Mwinyi) Zahera tukamuongelea sana Balama na tukakubaliana atamuongeza na sasa anatupa matunda, pia Makame (Abdulaziz) ni kiungo mzuri atatusaidia zaidi.”