Nyika: Zahera alishakataliwa

Muktasari:

Baada ya Zahera kutulia na kuanza kazi baadaye aliibuka katika vyombo vya habari na kulalamika juu ya kukwama kwa usajili wa Shikhalo na wachezaji wengine

Dar es Salaam. Katika mfululizo wa makala ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, tuliona jinsi sakata la usajili wa beki Kelvin Yondani lilivyoibua kizaazaa na ishu za ngumi kuwa nje nje.
Pia alifichua namna walivyokuwa wakiiendesha Yanga iliyokuwa kwenye hali mbaya ya kiuchumi. Nyika anaendelea kuelezea mambo mbalimbali wakati akiwa kiongozi wa timu hiyo.

USAJILI YANGA ULIHITAJI KIASI GANI?
“Kwanza lazima ujue Yanga ni timu kubwa na usajili wake lazima ufanyike kwa umakini, nakumbuka kuna watu walitubeza sana katika usajili wetu wakati huo hasa kile kipindi ambacho tulikuwa hatuna fedha na tulilazimika kutulia sana. Nakumbuka wakati tunaanza kumtafuta Shikhalo (Farouk) nilimfuata kwao Kenya akiwa na Bandari wakati huo alikuwa bado ana mkataba mrefu na klabu yake wa miaka miwili, tulipowagusa walihitaji Dola 50,000.
“Kilikuwa ni kiasi kikubwa sana, kweli alikuwa kipa mzuri tukasema hapana, tukarudi nyuma kutokana na wakati huo hatukuwa na fedha hiyo. Kama fedha hizo zingekuwepo bora tungelipa mishahara ya vijana, tukalazimika kumchukua Kindoki (Klause) kwani kipa namba moja alikuwa Kakolanya (Benno), tukasema huyu aje awe kipa wa tatu na alikuwa kipa mzuri na rekodi nzuri tu,” anasema.
“Kilichomtatiza na wakati wote makipa walikuwa wanalalamika hawakuwa wanapata mazoezi mazuri, hivyo hata ile hali ya kujiamini waliipoteza. Hivyo unaponiuliza Yanga ili isajili inahitaji kiasi gani naweza kusema kwanza inategemea na mahitaji ya kipindi husika makocha wanataka nini.
“Pia kwa uzoefu wangu kama unahitaji kuijenga timu nzuri ili ufanye usajili mzuri hutakiwi kukosa mfukoni kiasi cha Sh800 milioni au zaidi, lakini si pesa tu uwe na maamuzi mazuri ya kuchukua wachezaji kwa kuangalia ubora sahihi, maana unaweza kuwa na pesa lakini ukakosa maamuzi sahihi.”

UJIO WA ZAHERA
“Ujio wa Zahera nakumbuka ulikuja wakati ambao tulikuwa tumekimbiwa na Kocha Lwandamina (George), sasa kutokana na hali yetu ngumu tukasema tutafute kocha ambaye anatoka Afrika na mvumilivu, na namshukuru sana mjumbe wangu na kaka yangu wakati huo, Ndama, alinipigia simu usiku akaniambia mdogo wangu Hussein nimefanikiwa kumtorosha mwalimu mzuri anayeweza kutusaidia.
“Zahera alikuwa Zambia akisubiri kusaini na klabu moja ya huko, Ndama alichofanya akaongea na mdogo wake Zahera aliyekuwa hapa nchini. Ni rafiki yake mkubwa, kweli baada ya siku mbili Zahera alitua hapa na tukakutana naye, wakati huo tayari tulichokuwa tunafanya kilikuwa na baraka kwa makamu mwenyekiti wa klabu Sanga (Clement).”

ZAHERA ALIPINGWA
“Nakumbuka ndani ya kamati yetu ya utendaji tulikuwa tunatofautiana sana, kuna wengine walikuwa na akili ya kuwa kila kitu wao wanapinga tu, kocha alivyofika tukakutana naye, nilikuwa mimi, Ndama, marehemu Urungo (Mustapha) na mdogo wake Zahera, tukazungumza naye na kukubali ubora wake.
“Tukarudisha mrejesho kwa Sanga, akatupongeza sana akatupa maelekezo ya kumkutanisha Zahera na Katibu Mkuu Mkwasa (Boniface), tukafanya hivyo, sasa siku tuliyompeleka kwa Mkwasa ili naye amuonea na kuongea naye kwa kuwa ni kocha mwenzake.
“Nakumbuka pale klabuni kulikuwa na baadhi ya wajumbe wezetu wa kamati ya utendaji, baada ya Mkwasa kuongea na kocha akaridhika na Sanga akatoa maelekezo kwamba tusisubiri apewe mkataba na mengine atajibu yeye.
“Maamuzi ya Sanga yalitokana na wakati huo timu ilikuwa na mechi muhimu na timu haina kocha mkuu, mambo yanazidi kuwa magumu na hata kocha mwenyewe hakuwa na haraka na mkataba kutokana na mechi ambazo zilikuwepo mbele, nakumbuka tulitakiwa kusafiri kwenda Algeria kwenye mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho hatua ya makundi.
“Tuliporudi Sanga aliitisha kikao cha kamati ya utendaji, ndani ya kikao hicho ajenda zote hazikuzungumzwa ikarukiwa ya Zahera, kwa nini tumeleta kocha bila kuwajulisha wao, kocha mwenyewe anaonekana si kocha ni muimbaji muziki na hawamtaki, tukamuachia Sanga ajibu akawaelezea maamuzi yake na wakatulia.
“Kusema kweli Zahera kwa wakati huo ujio wake ulitusaidia sana, alikuwa kama baba kwenye timu, nakumbuka tulimwambia ukweli hali ya klabu juu ya ukata, akaelewa kulikuwa na migomo mingi sana wakati huo, lakini alisimama imara akaweza kuwaunganisha wachezaji na aliisaidia sana timu na malengo yetu sisi kama kamati tulifanikiwa sana.”

MALALAMIKO YA ZAHERA KATIKA USAJILI
Baada ya Zahera kutulia na kuanza kazi baadaye aliibuka katika vyombo vya habari na kulalamika juu ya kukwama kwa usajili wa Shikhalo na wachezaji wengine, Nyika anaeleza kuwa: “Hali (hiyo) ilitokea, lakini ukweli ni kwamba Yanga haikuwa na fedha na kocha alikuwa na sababu zote za kulalamika, hakuna kocha anayependa kupishana na mchezaji mzuri, kuna kundi la watu ambao walikuwa na kazi ya kuchafua viongozi.
“Nakumbuka ulikuwa ni usajili wa Shikhalo tuliporudi mara ya pili na straika mmoja na kiungo.  Awali, tulifanya mazungumzo na pande zote tukakubaliana kila kitu, tukakata tiketi kwa ajili ya safari kwenda kumalizana nao usiku wake, tukapokea simu wale wachezaji wamebadilika wanahitaji fedha zaidi wakidai walipata ofa kubwa kutoka klabu zingine, tukachanganyikiwa.
“Tuliongea nao, lakini muafaka haukufikiwa, fedha zilizohitajika zilikuwa nje ya uwezo wa klabu na hata sisi. Nakumbuka wakati huo tayari kocha tulishamueleza mchana kila kitu kinakwenda vizuri kabla ya kupokea hizo simu, sasa mambo yalivyobadilika kesho yake tulikuwa na mechi ngumu Uwanja wa Taifa tukasema si busara kumueleza kocha hayo usiku huo, tukasema tusubiri amalize mechi tumwambie.
“Kuna watu wakawahi kumwambia Zahera kabla ya sisi kuzungumza naye, hapo ndipo kocha akachukia na kuja kulalamika katika vyombo vya habari alipomaliza kulalamika hali ilikuwa.