Nyika : Manji, Bin Kleb, Seif Magari waliivuruga vibaya Simba- 2

Muktasari:

Jinsi alivyojigeuza kinyozi ili kupata ruhusa ya kuingia katika chumba cha hoteli waliyofikia JKU ili kuongea na kiungo huyo na namna walivyoondoka kikomandoo na mchezaji huyo na kuwaacha watu wa Simba wakifukuzia kwa nyuma gari yao iliyokuwa na vioo vyeusi kabla ya kuwaacha kona wafuatiliaji hao. Endelea.

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya ya kiongozi wa zamani wa Yanga, Hussein Nyika, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, alifunguka umafia uliofanyika kuiliza Simba katika dili la kumsajili Fei Toto.

Jinsi alivyojigeuza kinyozi ili kupata ruhusa ya kuingia katika chumba cha hoteli waliyofikia JKU ili kuongea na kiungo huyo na namna walivyoondoka kikomandoo na mchezaji huyo na kuwaacha watu wa Simba wakifukuzia kwa nyuma gari yao iliyokuwa na vioo vyeusi kabla ya kuwaacha kona wafuatiliaji hao. Endelea.

Alikoanza Nyika

Mdau huyu mkubwa wa Yanga, anasema: “Mimi kama ilivyo ada kwamba kila mtu anakuwa na mapenzi yake kwa timu fulani kwahiyo hata mimi tangu nilipokuwa kijana mdogo nilianza kuipenda Yanga na hiyo mimi ni kama nilirithi kutoka kwa mzee wangu ambaye tangu nakuwa nilikuta anaipenda Yanga na mimi kufuata nyayo zake. Niliendelea kuipenda Yanga mpaka nilipokuja kuwa na maisha yangu nikajikuta nimeingia moja kwa moja ndani ya timu.”

Nyika alihudumu katika Kamati ya Mashindano na ile ya Usajili baada ya kushinda kiti cha Mjumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi wa klabu hiyo wa mwaka 2014.

“Nakumbuka mwaka 2012 ndiyo ulikuwa mwanzo wangu kuingia ndani ya kamati na nilianza kupewa majukumu katika kamati ya mashindano nikiwa kama mjumbe wa kuteuliwa.”

Binkleb, Seif Magari wamvuta

“Baada ya kuingia Kamati ya Mashindano baadaye nilijumuishwa katika Kamati ya Usajili, bahati mbaya wengi walikuwa hawanijui kwa kuwa wakati huo Kamati ya Usajili waliokuwa mbele ya pazia ni Mwenyekiti na Makamu wake Abdallah Bin Kleb na Seif ‘Magari’ Ahmeid.

“Majukumu mengi wakati huo nilikuwa naagizwa tu na viongozi wakuu wa kamati. Nakumbuka mfano mzuri wakati huo jukumu langu kubwa lilikuwa katika usajili wa Mahadhi (Juma) wakati anatoka Coastal Union. Nakumbuka ilikuwa ni usajili uliokuwa na vurugu kwa vile alikuwa akigombewa na klabu nyingi. Hadi anafika hapa na kusajiliwa, alihamishwa katika hoteli kama tatu mpaka nne, yote ni kukwepa hujuma baada ya kuwa na timu ambazo zilikuwa zinataka kumchukua.

“Niseme tu kupitia uzoefu wa kusajili nilijifunza mengi sana kupitia Seif na BinKleb lakini nisimsahau Mhandisi Isack Chanji ambaye naye baada kuwa naye chini yangu katika kamati yake alinisaidia sana. Wale jamaa walikuwa moto mwingine katika vurugu za kusajili na hasa jambo ambalo lina maslahi ya Yanga. Akili yao inakuwa ni ya hali ya juu sana. nakumbuka hata upande wa pili (Simba) walikuwa wakisikia majina yao hawa watu wawili alafu juu yao yuko Manji walikuwa wanapata homa.”

Aingia na Manji,amchomolea Nchunga

“Kuingia ndani ya uongozi nafikiri kwa mara ya kwanza ningeingia katika uongozi wa mwenyekiti wa wakati huo Lloyd Nchunga ambaye alitaka kuniteua kuingia katika uongozi kama mjumbe wa kuteuliwa baada ya wajumbe wengi kujiuzulu.

“Sasa aliponiomba nijumuike naye, familia yangu hasa mzee wangu walinizuia kwa kuwa wakati huo vurugu za kupingwa uongozi zilikuwa kubwa. Nikamuomba radhi Nchunga, nashukuru alinielewa kwa kuwa aliona nina nafasi ya kumsaidia na kuisaidia klabu baadaye. Uchaguzi uliitishwa mwaka 2014 na nikagombea nafasi ya ujumbe nikashinda, nikaingia madarakani mwenyekiti akiwa Yusuf Manji makamu akiwa Clement Sanga.”

Aliingiaje Kamati ya Mashindano

“Tulipoingia madarakani baada ya muda baadaye ikatokea shida mwenyekiti wetu (Manji) alijiuzulu na ikabidi Mhandisi Sanga achukue nafasi yake kama Kaimu Mwenyekiti, sasa wakati huo Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano alikuwa Majid (Seleman) akaomba atoke kwa muda kutokana na kubanwa na majukumu, hivyo Kikao cha Kamati ya Utendaji kikanipa mimi jukumu la kuongoza kamati hiyo. Msimu huo ulipomalizika baada ya kuanza vizuri majukumu yangu kwenye Kamati ya Mashindano nikaongezewa majukumu mengine kwenye Kamati ya Usajili.”

Ukata Jangwani

“Safari ya kuongoza kamati hizo haikuwa nyepesi, ilikuwa na changamoto nyingi ambazo kadiri muda ulivyosogea nazo ziliongezeka. Kama utakumbuka wakati huo klabu ilikuwa haina mwenyekiti (Manji) ambaye uwepo wake ulihitajika sana kutokana na nguvu yake ya fedha, na unapoongea kuongoza kamati hizo ndiyo zilikuwa roho ya timu nzima, timu inapotaka kusafiri au kusajili ramani nzima inatakiwa kutoka hapo.

“Naweza kusema kwamba kulikuwa hakuna kufurahia kuwa kiongozi tena mambo yalikuwa mengi na magumu, kila ukisikia timu inatakiwa kusafiri kwenda sehemu fulani inakuwa hakuna kulala mnapambana hadi mnafanikisha. Hata timu ilipokuwa inashinda, unafurahi kwa dakika kadhaa tu, baada ya hapo shida inarudi.

“Kuna wakati mnaweza kushinda mechi, wakati mna furaha, unapigiwa simu kuwa timu imezuiwa kutoka au kuingia hotelini pesa zinahitajika, kiufupi safari ilikuwa ngumu sana. Nawashukuru na kuwapa pole wajumbe wenzangu wa Kamati ya Utendaji wakati huo kuanzia Sanga mpaka wale niliokuwa nao katika harakati, tulikuwa na wakati mgumu sana.

Walifanikishaje majukumu?

“Baada ya mambo kuwa magumu ilibidi tuwe wabunifu. Nakumbuka wakati huo katibu alikuwa kaka Mkwasa (Charles Boniface). Aliniita nikafanya naye kikao akaniuliza tunafanikishaje haya majukumu? Tukajadiliana na kukubaliana kutengeneza wigo mpana wanachama na wadau mbalimbali kuisaidia klabu yao.

“Tukakaa na kukubaliana kwamba ni wakati Wanayanga ndio waibebe klabu yao. Tukakutana na viongozi wa matawi na makundi ya mitandao ya kijamiii (WhatsApp) kupitia viongozi wao na nashukuru walikuwa tayari kusaidiana na klabu yao kuficha aibu. Walihamasika kwa kuchanga fedha na kugharamia mambo mengi na fedha hizo hazikuwa zinakuja kwangu wala uongozi zilienda moja kwa moja katika majukumu na hata kuwapa fedha wachezaji.

“Hilo lilikuwa eneo moja. Sehemu nyingine tukasema pia timu inahitaji ulinzi kila inakokwenda. Nako tukaunda kundi maalum ambalo tulilipa jina la Yanga Task Force. Hawa walikuwa wanaenda sehemu yoyote kwa gharama zao na nawashukuru sana walijituma walisafiri kabla ya timu kwenda kuweka mambo sawa mapema.”

Usikose Mwanaspoti kesho Ijumaa upate simulizi nyingi.