Mwakipaki: Kikapu pesa ipo, ishu kiwango tu

Muktasari:
- Mwakipaki alisema timu inayoshinda, mchezaji na benchi la ufundi kila mmoja anapata Sh87,500 jambo linalowapa hamasa zaidi ya kujituma wakijua baada ya kutoka uwanjani wanakifuta jasho.
KATIBU wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Mpoki Mwakipaki amesema msisimko na ubora wa ligi ya msimu huu ni mfumo wa udhamini unaowagusa wachezaji moja kwa moja, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, na sasa ni ishu ya kiwango tu kwa kila mchezaji.
Mwakipaki alisema timu inayoshinda, mchezaji na benchi la ufundi kila mmoja anapata Sh87,500 jambo linalowapa hamasa zaidi ya kujituma wakijua baada ya kutoka uwanjani wanakifuta jasho.
“Mfano wachezaji 12, katika benchi la ufundi kuna kocha mkuu, msaidizi, daktari na mtunza vifaa timu yao inaposhinda baada ya mechi kila mmoja baada ya mchezo anaona pesa ikiingia katika simu yake, mfumo huo haukuwapo miaka ya nyuma,” alisema Mwakipaki na kuongeza;
“Hali hiyo imeongeza ushindani mkubwa uwanjani, huo ni mwanzo tunatarajia kufanya makubwa zaidi kuhakikisha wachezaji wa kikapu wanafaidika na vipaji vyao, hivyo tunawashukuru wadhamini wetu ambao wamekuja kuupa thamani kubwa mchezo huo ambao utafanya maisha ya wachezaji kiuchumi yanakuwa mazuri.”
Kitu kingine alichokitaja kuongeza msisimko wa ligi hiyo timu ya wanawake na wanaume itakayochukua ubingwa kila moja itapata Sh10 milioni.
“Ligi inakwenda kusimama wikiendi hii kwa sababu ya kwenda kushiriki mashindano ya Taifa Cup yatakayofanyika kuanzia Juni 24 hadi Julai 4 ambapo kila mkoa utatoa timu. Kwa upande wetu kama mkoa wa Dar es Salaam tunapeleka timu ya wanawake na wanaume na tunajipanga kuhakikisha tunakwenda kuchukua ubingwa,” alisema na kuongeza;
“Ukiachana na hayo kama mkoa tunatamani kuwa na uwanja wetu wa kuchezea mpira wa kikapu, naamini ipo siku tutakuja kulifanikisha hilo.”
Kwa upande wa kocha wa Mgulani, Frank Kusiga alisema: “Ushindani wa ligi ni mgumu hilo linatokana na udhamini na pesa atakayopata bingwa, sisi tumeshinda mechi mbili kati ya tano tulizocheza.”
Msimamo ulivyo
Kabla ya mechi za jana, kwa upande wa wanaume, Dar City ilikuwa kileleni ikimiliki pointi 14 sawa na ilizokuwa nazo, ABC na Stein Warriors iliyokuwa na mchezo mmoja mbele ikicheza nane tofauti na hizo mbili zilizocheza saba kila moja.
Timu hizo tatu zilitenganishwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Savio ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 12 kupitia mechi nane.
Dar City na ABC kila moja imecheza mechi saba na kushinda zote, lakini Dar Citry imefunga 653 na kufungwe 329 dhidi ya 493 za ABC iliyofungwa 385, ilihali Stein imefunga 594 na kufungwa 514.
Kwa upande wa timu za wanawake, zinazoshika nafasi nne za juu kabla ya mechi za jana ilikuwa ni; Don Bosco Lioness iliyokuwa kileleni ikicheza mechi saba na kushinda sita, ikipoteza moja, ikifunga 522, ikifungwa 291 na kukusanya pointi 12 kama ilizonazo Tausi Royals, Jeshi Stars na Don Bosco Troncantti zilizotofautiana tu vikapu ilivyofunga na kufungwa.
Tausi na Jeshi hata hivo zimecheza mechi sita, tofauti na Troncantti iliyocheza michezo saba kama vinara, Don Bosco Lioness.
Kwa timu zilizokuwa mkiano kwa wanaume nafasi tatu za mwisho zilikuwa zikimilikiwa na Mgulani JKT, Polisi na Chui wakati kwa wanawake, Mgulani Stars, Ukonga Queens na City Queens zilikuwa nafasi tatu za mwisho zikiwa na wastani wa pointi kati ya 6-8, japo zilitofautiana mechi ilizocheza.